Mkomola arejea kuongeza nguvu Yanga

Muktasari:

Mshambuliaji huyo aliyeiongoza Serengeti Boys kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana U17 nchini Gabon

Dar es Salaam. Baada ya kukakaa nje kwa muda mrefu, mshambuliaji wa Yanga, Yohana Mkomola amesema ndoto yake ya kucheza mashindano ya kimataifa inatimia.

Mkomola aliumia kifundo cha mguu katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting na kulazimika kukaa nje kwa muda mrefu, lakini sasa ameanza mazoezi na kikosi cha Yanga.

Mkomola alisema kwa sasa anafanya mazoezi ya nguvu tofauti na awali ambapo yalikuwa mepesi, hatua hiyo inampa imani ya kucheza mechi ijayo ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Welayta Dicha ya Ehiopia.

"Hakuna mchezaji asiyetamani kuchangia mafanikio ya timu yake, nilikuwa naumia kuikosa mashindano hayo wakati timu yangu, ikicheza mechi ya Ligi Mabingwa Afrika, angalau napata moyo naweza nikacheza shirikisho,"

"Michuano hiyo inamsaidia mchezaji kuonekana nje, ni fursa ya kupanua ajira yangu, kwa umri wangu naona ni wakati mwafaka wa kujituma ili niweze kucheza soka la kulipwa," alisema.

Mbali na kutamani kucheza mashindano ya kimataifa ,alisema ndoto yake ni kuona Yanga inatwaa ubingwa akiwa na kikosi hicho, ili aweze kuwa katika rekodi ya kukumbukwa na wachezaji watakaokuja nyuma yake.

"Hata sisi tumekuta rekodi za wachezaji wakongwe, naamini walikuwa kama sisi ndio maana natamani kufanya kitu kwa nafasi hii niliopata kucheza klabu ya Yanga," alisema chipukizi huyo.