INAWEZEKANA: Kizazi kipya cha Hispania kitafanya makubwa Russia!
Muktasari:
Hii ni nafasi kubwa kwa timu za taifa kujipanga vizuri kwa ajili ya kushiriki kucheza fainali za Kombe la Dunia Urusi na kupima viwango vyao.
MSOMAJI wiki iliyopita na wiki hii mechi za kirafiki za kimataifa zimechezwa na kuendelea kuchezwa.
Hii ni nafasi kubwa kwa timu za taifa kujipanga vizuri kwa ajili ya kushiriki kucheza fainali za Kombe la Dunia Urusi na kupima viwango vyao.
Kwa mtazamo wangu Kombe la Dunia litakuwa na ladha nzuri sana kwa kuwa timu nyingi zipo katika mchakato wa kubadilisha kizazi na hivyo naamini mastaa wapya watazaliwa Urusi.
Naamini ni timu zenye mchanganyiko mzuri wa kizazi kipya na wachezaji wenye uzoefu mkubwa watakaokuja kufanya makubwa kwenye Kombe la Dunia. Na moja kati ya timu zenye sifa hiyo ni Hispania.
Bila shaka Timu ya Taifa ya Hispania ni timu ambayo imepata mafanikio makubwa sana.
Tangu mwaka 2008 Hispania imeshinda mashindano ya Euro mara mbili na Kombe la Dunia mara moja.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni dalili zote zimeonyesha kuwa timu hiyo inahitaji mabadiliko.
Katika mashindano mawili mfululizo, Hispania haijafikia mafanikio ya karibu kabisa ya kushinda taji.
Katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil mwaka 2014 Hispania ilitolewa katika hatua za awali na katika mashindano ya Euro mwaka jana ilitolewa katika hatua ya pili.
Kocha mkongwe wa Hispania, Vincent Del Bosque alijiuzulu baada ya mashindano ya Euro mwaka 2016.
Na Julen Lopetegui aliteuliwa kuwa kocha mpya wa timu hiyo. Kocha huyu ana jukumu kubwa la kuirudisha Hispania katika ubora wake.
Imebaki chini ya miezi mitatu hadi kufanyika kwa michuano ya fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa Urusi.
Lakini katika mechi za kufuzu mashindano hayo Hispania ilionyesha dalili kuwa ipo njiani kurudi katika ubora wake.
Ilicheza mpira wa kushambulia na haikupoteza hata mechi moja.
Ni imani yangu Hispania imepata matokeo kutokana na kuwapa nafasi wachezaji wa kizazi kipya katika timu ya taifa.
Hakika wachezaji kama Iniesta, Silva, na Xabi Alonso wameibeba Hispania kwa muda mrefu.
Lakini, wachezaji hawa wameshafikia umri mkubwa, Xabi Alonso amestaafu na fainali za Kombe la Dunia zitakapochezwa Urusi, mchezaji kama Iniesta atakuwa amechafikia umri wa miaka 34.
Bahati kwa Hispania ni kwamba kizazi kipya cha timu hiyo kimeshaonyesha uwezo wa kuziba pengo la kina Iniesta.
Ni wachezaji kama Isco na Asensio ambao wote wanaichezea Real Madrid, pamoja na Thiago Alcantra ambaye anachezea Bayern Munich, na Alvaro Morata kutoka Chelsea.
Hispania inacheza mfumo wa mpira unaotumia viungo wengi wenye kiwango kikubwa.
Isco na Thiago Alcantra wote ni viungo wenye umri mdogo lakini wana vipaji vikubwa.
Hata hivyo, chini ya kocha wa zamani wa Hispania, Vincent Del Bosque, wachezji hawa hawakupata nafasi kubwa katika kikosi cha kwanza kutokana kuwepo na upinzani mkali.
Lakini Kocha Lopetegui anataka kukiendeleza kikosi cha Hispania na kuwapa wachezaji wenye umri mdogo nafasi katika timu ya taifa.
Wachezaji kama Isco na Thiago hawajawahi kushinda taji na timu yao ya taifa na wana njaa ya kupata mafanikio katika timu hiyo.
Wiki iliyopita Hispania ilitoka sare na mabingwa wa Kombe la Dunia, Ujerumani huku Isco na Thiago wote wakiwa katika kikosi cha kwanza.
Ni ishara kuwa huenda Hispania itakuwa timu hatari katika michuano ya Kombe la Dunia.
Bila shaka kikosi hicho kina kizazi kipya ambacho kina uwezo mkubwa kwa kuwachanganya pamoja na wachezaji wakongwe wa timu hiyo naamini wataipeleka Hispania mbali sana katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.