Yondani aituliza Yanga, Zahera kicheko tu

Dar es Salaam. Kocha Mwinyi Zahera atakuwa ametabasamu baada ya beki wake kisiki, Kelvin Yondani kurejea kikosini tayari kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana utakaofanyika Agosti 23 ugenini.

Tangu Ligi ilipomalizika Yondani hakuwahi kuwa katika kikosi cha Yanga kutokana na awali kukabiliwa na majukumu ya timu ya Taifa iliyokuwa ikishiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Misri.

Hata hivyo licha ya mashindano hayo kumalizika na wachezaji wa Yanga kutakiwa kujiunga na timu, mchezaji huyo hakutokea mazoezini pamoja na mabeki wengine Juma Abdul na Adrew Vincent ‘Dante’ huku taarifa zilidai kuwa walikuwa wamegoma mpaka walipwe fedha zao za usajili.

Inadaiwa wachezaji hao waligoma kutokana na kuchukizwa na kitendo cha viongozi wa kuwalipa wachezaji wageni iliowajili msimu huu huku wao wakisotea fedha zao za usajili za tangu msimu uliopita.

Yondani alitumia kambi ya timu ya Taifa kama sababu kwa mashabiki wa klabu yake kuamini hakuwa na tatizo lolote na Yanga lakini nyuma ya pazia ilidaiwa mchezaji huyo aliweka mgomo hatatua ndani ya timu yake mpaka alipwe fedha zake.

Mchezaji huyo amekosa michezo na nane ya kirafiki ikiwemo Yanga ilipoifunga Tanzanite ya Morogoro mabao 10-1, Moro Academy mabao 7-1, Mlandege ya Znazibar mabao 4-1 na ilipotoka sare na Malindi ya bao 1-1.

Pia alikosa mchezo wa kimataifa wa kimataifa wa kirafiki wa kuadhimisha Wiki ya Wananchi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 na pia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Yondani ambaye ndiye nguzo kubwa ya safu ya ulinzi ya Yanga kukosekana kwake uwanjani kumekuwa kama pengo katika kikosi hicho kwani hata katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers safu ya ulizni ya timu hiyo ilionekana kuyumba.

Katika mchezo huo safu ya ulinzi ya Yanga iliongozwa na Mghana Lamine Moro na Ally Mtoni ‘Sonso’  ambao mara kwa mara walikuwa hawana  maelewano mazuri hasa katika kujipanga na kukaba kwa nafasi na kujikuta wakiruhusu bao  kwa wageni.

Tayari Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amethibitisha kumalizana na mchezaji huyo pamoja na Abdul  huku wakiendelea na mazungumzo na Dante.

 “Tunatambua  umuhimu wa wachezaji  hao katika kikosi chetu hivyo tayari  Yondani na Abdul  tumeshamalizana nao na wanarejea mara moja na kuongeza nguvu kabla ya mchezo wa marudiano dhidi ya Township Rollers utakaofanyika  Agosti 23 nchini Botswama.

 “ Dante leo(jana) tumezungumza nae na kesho (leo Jumatano) tunakutana nae kumalizia mazungumzo ili  tuone suala lake tunalimaliza vipi ili arejee kama ambavyo wenzake wamerejea," alisema”Mwakalebela.

 Dante alipouliza kwa nini hajajiunga na wenzake mpaka sasa alijibu”Mungu akipenda nitajiunga wakisharudi kwenye mchezo dhidi ya Township Rollers hilo ndilo naweza kusema na kuhusu kama nimelipwa hela zangu au sijalipwa siwezi kuliongelea kwa sasa.

Mchambuzi Ally Mayay alisema licha ya kwamba mabeki Lamine Moro na Ally Mtoni ‘Sonso’ walijitahidi  katika mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers lakini bado Yondani ataendelea kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Yanga.

“Bado Yondani ni muhimu na ana mchango mkubwa katika kikosi cha Yanga hivyo asipokuwepo unaona kabisa safu ya ulinzi ina mapungufu.

“Ukiangalia hata lile goli dhidi ya Township Rollers ambalo Yanga ilifungwa lilitokana na mabeki kutojipanga vizuri na mara nyingi walikuwa wakicheza hivyo  na pengine angekuwepo Yondani lisingefungwa kwa sababu anajua kukaba katika nafasi. Mechi ijayo ya marudiano Yondani anahitajika sana na ni vizuri kama amerejea kikosini,”alisema Mayay.  

Faroukh na wenzake wapigiwa hesabu kali 

Katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika,Yanga iliwakosa nyota wake Faroukh Shikhalo, Falcao na Maybin Kalengo.

Uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa wameongeza nguvu ya mawasiliano na shirikisho la soka Afrika kupata leseni zakucheza mchezo wa pili.

Mwakalebela alisema mazungumzo hayo yanekwenda vizuri na wanaamini kabisa wachezaji hao watakuwepo sehemu ya mchezo ujao.

 Mkataba GSM bado siri

Yanga wameonekana katika jezi zao kukiwa na mabango ya wadhamini huku wadau na wanachama wakihoji mikataba waliyosaini ni ya miaka mingapi.

Gazeti hili  lilipombana  Mwakalebela kutaka kufahamu ukweli wa mikataba hiyo na ndipo alisema, mpaka wadhamini hao wanaka kwenye jezi yao tayari walishakubaliana baadhi ya vitu ambavyo wameridhika navyo.

"Kwa asilimia kubwa tayari  tumeshakubaliana, mfano watu wa jezi tumekubaliana nao katika kila jezi kupata labda 1300, wao wauze lakini sisi kwenye kila jezi tunapesa yetu, hayo yote yapo alisema.