TFF yamjibu Zahera taji la ubingwa Simba kukabidhiwa mechi ya Sevilla

Muktasari:

Kupitia msemaji wa TFF,  Clifford Marion Ndimbo aliliweka sawa jambo hilo kwamba hakuna kanuni ya shirikisho inayoruhusu bingwa akabidhiwa kombe nje na mechi ya Ligi Kuu Bara.

 

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeamua kumuondoa wasiwasi kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye alikerwa na maneno ya msemaji wa Simba Haji Manara kwamba ubingwa watakabidhiwi wakati wa mechi yao na Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu nchini Hispania (La Liga).

Kupitia msemaji wa TFF,  Clifford Marion Ndimbo aliliweka sawa jambo hilo kwamba hakuna kanuni ya shirikisho inayoruhusu bingwa akabidhiwa kombe nje na mechi ya Ligi Kuu Bara.

"TFF ina kanuni zake hata Simba wakiandika barua kama alivyosema msemaji wao Manara kwamba endapo wangeshinda mechi zao wakabidhiwe taji la ubingwa kwenye mechi yao na Sevilla hakuna kitu kama hicho na hakitafanyika.

"Kama Zahera ana wasiwasi na hilo basi ajue kabisa kwamba TFF ina kanuni zake hata wakiandika barua hiyo, majibu yao ni rahisi kuwa kanuni haziruhusu mambo hayo"anasema.

Kuna video inayomuonyesha Zahera kwamba Simba watakabidhiwa ubingwa wakati sio mabingwa baada ya kusikia kauli ya msemaji wa Simba, Manara kuwa wataiomba TFF wawakabidhiwa wakati wa mchezo wao na Sevilla.

"Simba wanapewa ubingwa na TFF, ndio maaana msemaji wao Manara anasema wakabidhiwe siku ya mchezo wao ambao sio wa ligi na Sevilla" mwisho wa kunukuu kauli ya Zahera.