Sababu za Eymael kutimuliwa Yanga

YAMETIMIA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mabosi wa Yanga kuamua kumfuta kazi Kocha wao, Luc Eymael.

Awali, Mwanaspoti lilikudokeza kwamba, mabosi wa Yanga walipanga kumtimua kocha wao huyo kama angepoteza mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo waliambulia sare.

Tofauti na mechi za nyuma, kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa na baadaye Lipuli uliopigwa jana Jumapili, mabosi wazito wa Yanga walikuwa uwanjani wakiwa tayari wamenoa panga wakisubiri ajichanganye tu.

Mchezo huo dhidi ya Lipuli ulibeba sura ya mwisho ya hatma ya benchi la ufundi la Yanga na hata nusu ya kikosi hicho pindi msimu mpya utakapoanza.

Tayari, makocha wawili wameshajiweka kando, wazawa Charles Mkwasa na kocha wa makipa Peter Manyika ambao inaelezwa kwamba, walishindwa kufanya kazi na bosi wao Eymael.

Katika toleo lake la Ijumaa, Julai 24, 2020 Mwanaspoti lilikufunulia sababu saba ambazo zinaweza kumng’oa Eymael Jangwani. Sasa zikiwa zimepita siku tatu, mabosi wa wajumbe wa Yanga wakamfyeka. Sasa tiririka kuzijua sababu hizo.

 

Vita ya Mkwasa, Manyika v Eymael

Inaelezwa kwamba Eymael katika mazoezi ya mwisho kabla ya Yanga haijaifuata Mtibwa Sugar nusura wazichape na Manyika na inaelezwa kocha huyo wa makipa alishindwa kuvumilia kauli moja kutoka kwa Mbelgiji huyo ingawa haikufafanuliwa ni ipi.

Wasaidizi wake walikuwa hawamsaidii sana sasa wanachotaka kufanya mabosi wa klabu hiyo ni kuwaondoa wote kisha maisha yaanze upya.

Nidhamu ya kikosi

Yanga inaonekana wazi suala la nidhamu ni changamoto kubwa huku makocha nao wakiwagawanya wachezaji kutokana na wao kutoimba wimbo mmoja. Tayari makocha wote wanaonekana kutokubaliana katika baadhi ya mambo na sasa afya pekee katika kurudisha nidhamu ni kuwaondoa wote.

Habari kutoka ndani ya kikosi hicho ni kwamba wapo wachezaji wamekuwa wakichagua nani acheze na nani asicheze.

Morrison amemponza Eymael

Wachezaji wa Yanga nao wananung’unika kwamba kuna mchango mkubwa wa Eymael katika anguko la Morrison wakidai kumbe hata hatua ya Morrison kutaka kuomba radhi wachezaji wenzake ilikuwa ni akili ya kocha huyo na hata Morrison alivyorejea kundini baada ya mgomo wa kwanza akitokea katika kesi yake na TFF Mghana huyo hakuwa na mpango huo.

Uswahiba wa Morrison na Eymael umewakera wachezaji wengi na kuona kama kocha huyo aliegemea kwa mchezaji huyo aliyekuja naye Yanga.

Mazoezi Yanga laini mno

Mabosi wa Yanga nao kumbe wanafuatilia kwa karibu hata mazoezi ya timu hiyo na kikubwa walichogundua vijana wao hawana mazoezi ya kutosha huku wakiwa wanakula vyema na kulala hoteli safi.

Inaelezwa kocha mmoja mzawa (jina tunalo) ambaye yupo timu pinzani aliishuhudia timu hiyo mara moja ikifanya mazoezi baada ya kumaliza mechi yao kisha akawaambia mabosi wa Yanga kwamba kwa mazoezi hayo na wachezaji wa Kitanzania basi anguko la Yanga uwanjani ni sahihi.

Kumbe kocha huyo aliwaambia mapema kwamba kama watakutana na Simba kwa mazoezi aliyoyaona basi kipindi cha pili wataomba poo, na hicho ndicho kilichotokea kwa Yanga katika mchezo uliopita ambao kipindi cha pili kuruhusu mabao matatu wakipigwa 4-1 na Simba.

Kuna mchezaji wake mmoja wa kigeni naye amewaambia mabosi wa Yanga kwamba mazoezi wanayopewa ni laini sana kama vipi wamwambie kocha aongeze lakini wenzake hawawezi kusema kwa kuwa wanaona poa tu.

Lugha inamponza Eymael

Yanga ina kikosi chepesi lakini wachezaji nao inadaiwa hawana furaha na Eymael, wanakwenda naye basi tu na wasichokikubali ni kwamba Mbelgiji huyo amekuwa na kauli kali kwa wachezaji wake kiasi cha kugawanyika huku pia kuna baadhi akiwaona kama watu muhimu kwake. Habari zinasema kwamba wachezaji wengi hususani wazawa hawajazoea kupelekwa kibabe kama ilivyo staili ya utendaji wa Eymael.

Eymael kupigwa na makopo Jamhuri

Hakuna kocha aliyewahi kurushiwa chupa za maji nchini halafu akapona, anzia kwa Patrick Aussems (Simba), Mwinyi Zahera (Yanga) na hata Juma Mwambusi (Mbeya City) wote baada ya muda vibarua vyao viliota nyasi kwa nyakati tofauti.

Juzi pale Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, Eymael yamemkuta wakati akimtoa kiungo Abdulaziz Makame ambaye alikuwa na mchezo mzuri huku mashabiki wakiona mshambuliaji wao Yikpe Gnamien ndiye anayewanyima ushindi.

Hatua hiyo ikawafanya mashabiki kushindwa kuvumilia na kumrushia chupa za maji kocha wao na hatua mbaya zaidi naye akawajibu kwa ishara ya vidole akiwaonyesha kichwani kwamba hakuna wanalojua.

Habari za ndani ya Yanga zinaeleza kuwa hilo litamweka katika wakati mgumu Eymael ambaye katika mchezo huo mabosi wake Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla na hata Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambaye ndiye aliyemleta kocha huyo Mhandisi Hersi Said naye alikuwa jukwaani akifuatilia tukio hilo.

GSM inaelezwa mkataba ambao walimpa Eymael ni wa mtego zaidi akitakiwa ndani ya miezi sita kuthibitisha ubora wake na hatua mbaya kwa kocha huyo mpaka sasa hana uhakika wa kombe lolote huku akiitafuta kwa mbinde nafasi ya pili katika Ligi na kama mambo yataenda hivi mkataba huo utamng’oa kirahisi.

Eymael ana ofa zake

Habari zaidi zinasema Eymael naye amechoka shida za Yanga na amepokea ofa mbili akitakiwa kurejea Ligi Kuu ya Afrika Kusini na anachosubiri ni kumaliza msimu kisha afanye uamuzi.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinaeleza kocha wao huyo anawindwa na timu mbili kutoka katika nchi tofauti ambazo zimeweka wazi nia ya kumtaka kama watakuwa tayari kumuachia muda wowote.

Taarifa hiyo inaeleza timu ya kwanza ambayo imeonyesha kumhitaji Eymael ni Free State Stars ya Afrika Kusini ambayo msimu uliopita ilishuka kutoka Ligi Kuu na kwenda Ligi Daraja la Kwanza na mabosi wa timu hiyo wanapambana kukisuka kikosi chao ili kuona inarudi juu.

Timu nyingine inayomhitaji Eymael ni Waarabu wa Kuwait kikosi cha Kazma SC, ambao kabla ya kumtaka kocha huyo walishaonyesha nia ya kumuhitaji mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison lakini dili lao lipo kimya hadi wakati huu.

Eymael alipoulizwa kuhusiana na ofa zake alisema; “Mkataba wangu na Yanga unaonyesha kuwepo na mipango miwili kuhakikisha timu inapata mafanikio kwa muda mfupi na ule mpango wa muda mrefu kwa maana hiyo akili yangu ipo hapa kwa sasa kuhakikisha nafanikisha yale ambayo natakiwa kuyafanya.”

“Sijapokea taarifa rasmi kutoka kwa timu yoyote inayonihitaji, lakini wanatakiwa kutambua bado nipo na mkataba wa muda mrefu na Yanga ambao ndio kwanza nimeutumikia miezi sita na sijaifikisha pale ambapo natamani kuona imefika au niliahidi nilipowasili hapa nchini,” alisema.