Dodoma Jiji yaungana na Gwambina Ligi kuu

Muktasari:

Dodoma Jiji imefanikiwa kupanda ligi kuu licha ya wapinzani wao Ihefu nao kushinda mchezo wao dhidi ya Cosmopolitan.

Mabao mawili ya Anuary Jabir na Mcha Khamis yalifanikisha kuipeleka ligi kuu timu ya Dodoma Jiji jioni la leo Jumamosi Julai 11, 2020 katika uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Iliwachukua dakika tano tu Dodoma Jiji kupata bao la kwanza kupitia Anuary Jabiri, ambaye bao lake la leo ni la 11 msimu huu, huku Mcha bao lake likiwa la saba msimu huu.

Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ulishuhudiwa na mashabiki wengi wa Dodoma ambao walikuwa na hamu ya kuona timu hiyo inapanda ligi kuu baada ya kukosa timu yao halisi ya Dodoma tangu iliposhuka Polisi Dodoma mwaka 2011.

Dodoma Jiji ambayo kwa misimu miwili nyuma ilikuwa inaitwa Dodoma FC, jitihada zao zilishindikana misimu yote miwili na sasa imekata kiu ya wananchi wa mkoa huu ambao wamesubiri kwa miaka tisa kuona timu yao ikipanda na kucheza ligi kuu.

Ushindi huo umeifanya Dodoma Jiji imalize kwa alama 51 kama ilivyo kwa Ihefu ambao nao waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Cosmopolitan, mchezo uliochezwa uwanja wa Highlands Estates, Ubaruku wilayani Mbarali.

Mabao manne ndio yaliyoitofautisha Dodoma Jiji wakiwa na jumla ya mabao 26 ukiondoa ya kufunga na kufungwa, huku Ihefu wakiwa na mabao 22.