Bosi Yanga afichua ndoto yake kumrudisha Herritier Makambo

Muktasari:

Hafidh alisema kama kuna straika ambaye Wanayanga bado hajawatoka akilini ni Makambo, akitaja sababu kuwa alifahamu kufunga na Yanga ilikuwa ngumu kutoka uwanjani bila kupata bao kitu ambacho kwa sasa ni tofauti.

MZIMU wa Herritier Makambo bado unaitesa Yanga. Sikia alichozungumza mratibu wa klabu hiyo, Hafidh Saleh kwamba kama angekuwa na pesa basi angemrudisha Jangwani kwa gharama zake.

Makambo aliyeichezea Yanga kwa mwaka mmoja kwa mafanikio, alipachika mabao 17 katika msimu uliopita kabla ya kuuzwa kwenda Horoya FC ya Guinea.

Hafidh alisema kama kuna straika ambaye Wanayanga bado hajawatoka akilini ni Makambo, akitaja sababu kuwa alifahamu kufunga na Yanga ilikuwa ngumu kutoka uwanjani bila kupata bao kitu ambacho kwa sasa ni tofauti.

Alisema umuhimu wa mchezaji wa kimataifa unatakiwa kuwa tofauti na wazawa na ndio sababu wametumia fedha nyingi kuwapata kitu ambacho wanaamini endapo Makambo angekuwepo basi watu wangeteseka sana.

“Yanga imesajili nyota wengi wa kigeni ambao walikuwa bora na waliisaidia timu kufikia malengo wakiwemo kina Hamis Kiiza, David Mwape, Kenneth Asamoah na wengine wengi kila mmoja anakumbukwa kwa mazuri yake, lakini kwa Makambo ameondoka kipindi ambacho timu bado inamuhitaji,” alisema na kuongeza:

“Makambo alikuwa mpambanaji na hakubali kushindwa hadi dakika za mwisho. Kipindi hiki bado timu imekosa mtu kama yeye kutokana na kushindwa kupata matokeo jambo ambalo naamini ni la muda tu.”

Hafidh alisema moja ya nyota ambao anatamani kuwaona Yanga, Makambo ni mmojawapo na anaamini si kwake tu ni mtu ambaye anazungumzwa sana Jangwani.