Aussems apania pointi tatu Ijumaa

Muktasari:

Simba itashuka dimbani Ijumaa, Uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam   kucheza na Mtibwa Sugar mchezo wa raundi ya pili  ya  Ligi Kuu Bara.

Dar  es  Salaam. Kocha  wa Simba, Mbelgiji   Patrick Aussems amepanga  kuvuna pointi   tatu katika mchezo wao wa Ligi Kuu Bara, utakaochezwa  Ijumaa, uwanja wa Uhuru   dhidi ya Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kumaliza mazoezi leo asubuhi, Aussems alisema akili yake amegeuzia kuhakikisha anafanya vizuri katika Ligi baada ya kutolewa katika Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

"Tunahitaji matokeo katika mchezo dhidi ya Mtibwa, naamini kabisa hili lipo katika uwezo wetu kama timu kuhakikisha tunafanikisha hili, naelewa Mtibwa wana timu ngumu lakini tunataka kuendeleza matokeo mazuri ambayo tumeanza nayo," alisema.

Aussems aliongeza kurejea kwa wachezaji Beno Kakolanya, Hassan Dilunga,Erasto Nyoni, Gadiel Michael na Mohamed Hussein ambao walikuwa katika majukumu ya timu ya Taifa kumezidi kufanya kikosi chake kikamilike.

"Nashukuru wachezaji wa Tanzania wamerejea, bado Kahata ambaye nazani anaweza kuingia karibuni kuanzia leo usiku ili ajiunge na wenzake kwaajili ya mchezo ujao, lakini Kagere yeye anaweza kuingia kesho," alisema.

Akizungumzia kuhusu mshambuliaji wake John Bocco, alisema mchezaji huyo bado hajawa fiti licha ya kuanza  mazoezi.

"Tunajua kabisa kwamba Bocco alikuwa nje takribani wiki tatu, bado hajawa fiti na anahitaji muda kidogo kwasababu bado ana maumivu," alisema.

Aussems aliweka wazi anamuhiaji zaidi mshambuliaji wake Meddie Kagere katika mchezo wake ujao dhidi ya Mtibwa.

Alisema washambuliaji wake Wilker Da Silva na John Bocco bado hawajawa fiti na mshambuliaji pekee aliyebaki ni Kagere.