Simba yamaliza kazi CAF ikiifuata Yanga
Muktasari:
Ushindi huo umeifanya Simba kufuzu hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla ya mabao 9-1, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa uwanjani hapo, Oktoba 21, 2026.
SIMBA SC imemaliza kwa kishindo hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa 15 de Agosto ya Guinea ya Ikweta mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Simba kufuzu hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla ya mabao 9-1, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa uwanjani hapo, Oktoba 21, 2026.
Simba ilitawala mchezo huo katika vipindi vyote viwili, ingawa ilishindwa kutumia vyema nafasi kadhaa za wazi ilizozitengeneza katika kipindi cha kwanza, hali iliyozifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana.
Mshambuliaji Ibrahim Doumbia, aliyefunga mabao mawili katika mchezo wa kwanza, alikuwa miongoni mwa wachezaji waliopata nafasi za wazi lakini akashindwa kuzitumia ikiwemo tatu za kipindi cha kwanza.
Kocha wa Simba, Steve Barker, alifanya mabadiliko kadhaa kipindi cha pili baada ya kuona timu inahitaji kuongeza makali ya ushambuliaji. Mabadiliko hayo yalihusisha kuwatoa Doumbia, Nickson Kibabage, Libasse Gueye na Rushine De Reuck, huku nafasi zao zikichukuliwa na Elie Mpanzu, Ismail Toure, Nathaniel Chilambo na Anicet Oura.
Mabadiliko hayo yaliongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji na Simba ikapata bao la kwanza kupitia Oura dakika ya 57, kabla ya Mpanzu kuongeza la pili dakika ya 68. Keletso Makgalwa alikamilisha ushindi huo kwa kufunga bao la tatu dakika ya 76.
Matokeo hayo yanaendeleza historia ya Simba katika mashindano ya CAF, ambako imekuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika na kufika hatua za juu.
Miongoni mwa mafanikio yake ya kihistoria ni kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1974.