Tshishimbi abariki Gadiel kuondoka Yanga

Muktasari:

Tshishimbi kila mchezaji anaumuhimu kikosini anapokuwa katika timu, lakini akiondoka hana umuhimu tena atakayezungumziwa ni mbadala wa nafasi hiyo.

Dar es Salaam. Baada ya taarifa za beki wa Yanga, Gadiel Michael kuhusishwa kutua Simba, kiungo Papy Tshishimbi ameibuka na kusema kuondoka kwake siyo tatizo kwa miamba hiyo ya mtaa wa Jangwani na Twiga.

Gadiel alikuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Yanga kilichomaliza ligi katika nafasi ya pili msimu uliopita amemaliza mkataba na Wanajangwani na taarifa za ndani zimebainisha kuwa tayari amemwaga wino Msimbazi.

Tshishimbi alisema Gadiel alikuwa na umuhimu kikosini alipokuwepo, lakini mara baada ya kuondoka umuhimu wake unakuwa haupo na wachezaji wengine watafanya majukumu hayo.

"Yanga ina wachezaji wengi na mchezaji kuhama katika klabu moja kwenda nyingine hilo suala lipo wala halijaanza leo hivyo kwakuwa kaondoka mapema usajili ukiwa bado unaendelea naamini viongozi watafanyia kazi hilo,"

"Hakuna mchezaji muhimu zaidi kwenye klabu ambayo inasajili anaweza akaondoka na akasajiliwa mwingine bora zaidi na mchezaji huyo ambaye wengi waliona ni pengo hakawa hakumbuki hata kwa sekunde," alisema.

Tshishimbi ni rafiki wa karibu na mchezaji huyo alisema hawezi kuzungumzia nafasi ya mchezaji huyo katika kikosi chake kipya kwa sababu hana uzoefu na timu nyingine.