Yamal apeleka vita ya Camp Nou mtaani
Muktasari:
- Hata hivyo, mbali na furaha ya kutwaa taji hilo baada ya kufikisha pointi 91 katika michezo 35, gumzo nchini Hispania limehamia kwa kinda tegemeo, Lamine Yamal ambaye ametumia fursa hiyo kuendeleza "vita" yake ya maneno dhidi ya Real Madrid.
Mitaa ya jiji la Barcelona jana iligeuka kuwa ya rangi nyekundu na bluu wakati klabu ya FC Barcelona ikisherehekea ubingwa wake wa 29 wa La Liga.
Hata hivyo, mbali na furaha ya kutwaa taji hilo baada ya kufikisha pointi 91 katika michezo 35, gumzo nchini Hispania limehamia kwa kinda tegemeo, Lamine Yamal ambaye ametumia fursa hiyo kuendeleza "vita" yake ya maneno dhidi ya Real Madrid.
Katika msafara wa basi la wazi uliopita katika maeneo ya kihistoria ya jiji hilo, Yamal alionekana akiwa ameshikilia jezi ya Barcelona yenye ujumbe mzito “Namshukuru Mungu sipo Madrid”.
Kitendo hicho kimefasiriwa kama kilele cha uchokozi wake kwa mashabiki wa Los Blancos, kikiashiria kuwa yeye si mchezaji tu, bali ni shabiki lialia wa Barcelona asiyependa hata kusikia jina la mahasimu wao.
Hii si mara ya kwanza kwa Yamal, ambaye ana umri wa miaka 18 kuingia kwenye mzozo dhidi ya Madrid.
Mapema msimu huu, kabla ya mchezo wa El Clásico, Yamal alitoa kauli kali iliyodaiwa kuwakera wachezaji wakongwe wa Real Madrid akiwemo Dani Carvajal.
Ripoti zilisema kuwa chumba cha kubadilishia nguo cha Madrid hakikufurahishwa na kile walichokiita "ukosefu wa heshima" kutoka kwa kinda huyo.
Aidha, Yamal amekuwa akitumia mitandao yake ya kijamii, hususani Instagram kuposti jumbe tata na picha zinazowashushia hadhi wapinzani wake mara baada ya mechi kubwa.
Katika mchezo uliopita, alionekana akishangilia kwa namna ya kuwanyamazisha mashabiki wa Madrid, jambo lililosababisha baadhi ya wachambuzi kumuita "villain" (adui) mpya wa soka la Hispania.
Ubingwa huu wa Barcelona umekuja baada ya ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Real Madrid katika mchezo wa hivi karibuni wa ligi uliopigwa Spotify Camp Nou.
Katika mchezo huo, mabao ya Marcus Rashford na Ferran Torres yalitosha kuwapa Barca pointi tatu muhimu na kuwapa ubingwa huo kwa kuwa michezo iliyobaki Madrid hawawezi kufikia idadi ya pointi ambazo mahasimu wao wamekusanya.
Yamal amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya kocha Hansi Flick msimu huu akiwa tayari ameshabeba mataji matatu ya ligi, ingawa vitendo vyake vya jana vimezua mijadala mikali, kwa mashabiki wa Barcelona Yamal ni kielelezo cha kizazi kipya chenye ujasiri wa kupambana kwa ajili ya nembo ya klabu yao, bila kujali ukubwa wa mpinzani.