Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yamal aendeleza utawala ‘Kopa Trophy’

YAMAL Pict

Muktasari:

  • Tuzo hiyo hutolewa na jarida la soka la Ufaransa, France Football, huku majaji wake wakijumuisha washindi wa tuzo ya Ballon d'Or.

BARCELONA, HISPANIA: NYOTA chipukizi wa Barcelona, Lamine Yamal, ameendelea kuandika historia katika soka la dunia baada ya kutwaa tuzo ya Kopa Trophy 2026, inayotolewa kwa mchezaji bora duniani mwenye umri chini ya miaka 21, kwa mara ya tatu mfululizo.

Yamal, ambaye ana umri wa miaka 19, amekuwa mchezaji wa kwanza kuendeleza utawala wake katika tuzo hiyo kwa kuibuka mshindi mwaka 2024, 2025 na sasa 2026, akithibitisha kipaji chake kikubwa licha ya umri wake mdogo.

Tuzo hiyo hutolewa na jarida la soka la Ufaransa, France Football, huku majaji wake wakijumuisha washindi wa tuzo ya Ballon d'Or.

Mafanikio hayo yanaendeleza utawala wa Barcelona katika tuzo hiyo, ambayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 imeshuhudia nyota mbalimbali wakiitwaa, akiwamo Kylian Mbappé mwaka 2018, Matthijs de Ligt mwaka 2019, Pedri mwaka 2021, Gavi mwaka 2022 na Jude Bellingham mwaka 2023. Tuzo hiyo haikutolewa mwaka 2020 kutokana na janga la COVID-19.

YAM 01

Hata hivyo, licha ya kutwaa tuzo hiyo kwa mara nyingine, Yamal alionyesha unyenyekevu kwa kusema anatamani ingekwenda kwa mwenzake wa Barcelona, Pau Cubarsí, ambaye pia alikuwa akiwania tuzo hiyo.

“Natamani Cubarsí, mwenzangu, angekuwa hapa. Tuzo hii ilipaswa kuwa yake. Natamani yeye ndiye angeishinda,” amesema Yamal baada ya kutangazwa mshindi.

Kauli hiyo imeonyesha namna nyota huyo anavyowathamini wachezaji wenzake, licha ya yeye kuendelea kung'ara katika kiwango cha juu ndani ya Barcelona na timu ya taifa ya Hispania.

Yamal pia alitumia nafasi hiyo kuishukuru klabu yake pamoja na timu ya taifa kwa mchango wao katika maendeleo yake, akisisitiza kuwa bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kuendelea kutwaa mataji ya timu na tuzo binafsi.

YAM 02

“Ninataka kuishukuru klabu yangu na timu yangu ya taifa. Lazima niendelee kufanya kazi kwa bidii ili kushinda mataji ya pamoja na tuzo binafsi kama hii,” aliongeza.

Yamal amekuwa mhimili muhimu katika kikosi cha Barcelona, akifanya vizuri katika msimu wa 2025/26. Katika mechi 45 alizocheza, alifunga mabao 24 na kutoa pasi 18 zilizozaa mabao.

Katika msimu wa sasa, tayari alikuwa amecheza mechi 13, akifunga mabao 10 na kutoa pasi 10 za mabao, takwimu zinazoonyesha mchango wake mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya miamba hiyo ya Hispania.

Katika kipindi hicho, Barcelona ilitwaa taji la La Liga pamoja na Spanish Super Cup mwaka 2026, huku Yamal akiwa miongoni mwa wachezaji waliochangia mafanikio hayo.

YAM 03

Vilevile, amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania kinachonolewa na Luis de la Fuente. Licha ya umri wake mdogo, Yamal alikuwa ameichezea Hispania mechi 37 na kufunga mabao 11.

Katika Kombe la Dunia lililochezwa majira ya kiangazi mwaka huu, Yamal alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochangia mafanikio ya Hispania, akishiriki katika mechi zote nane na kuanza saba.

Mbali na Kopa Trophy, Yamal pia alitwaa tuzo ya Golden Boy mwaka 2024, inayotolewa na gazeti la michezo la Italia, Tuttosport, kwa mchezaji bora wa soka la Ulaya mwenye umri chini ya miaka 21.

YAM 04

Kwa kutwaa Kopa Trophy kwa mara ya tatu mfululizo, Yamal ameendelea kuimarisha nafasi yake miongoni mwa vipaji vikubwa zaidi duniani.

Na kwa kuwa bado ana umri wa miaka 19, nyota huyo wa Barcelona ana nafasi ya kuwania tuzo hiyo tena katika miaka ijayo, endapo ataendelea kutimiza vigezo vya umri na kudumisha kiwango chake cha juu.

Kwa sasa, ujumbe wake ni wazi: licha ya mafanikio binafsi, bado anaamini wachezaji wenzake wanastahili kutambuliwa pia, huku akimtaja Cubarsí kama mtu ambaye alitamani kuona akitwaa tuzo hiyo mwaka huu.