Wemby aiangusha Spurs, Knicks ikibakiza hatua mbili za ubingwa NBA
Muktasari:
- Jalen Brunson alifunga mkwaju wa adhabu uliowapa Knicks uongozi zikiwa zimesalia sekunde 9.5 kabla ya mchezo kumalizika, baada ya Victor Wembanyama kupoteza mpira katika dakika za mwisho.
SAN ANTONIO, MAREKANI: MASHABIKI wa New York Knicks wana sababu zaidi ya kusherehekea baada ya timu yao kuendelea kung’ara katika fainali za NBA na sasa wanahitaji kushinda mechi mbili ili kutwaa ubingwa ambao jiji hilo limeusubiri kwa miongo kadhaa.
Jalen Brunson alifunga mkwaju wa adhabu uliowapa Knicks uongozi zikiwa zimesalia sekunde 9.5 kabla ya mchezo kumalizika, baada ya Victor Wembanyama kupoteza mpira katika dakika za mwisho.
Kisha Wembanyama akakosa mtupio wa mwisho ambao ungeipa ushindi San Antonio Spurs na hivyo Knicks kuibuka na ushindi wa pointi 105-104 usiku wa kuamkia jana, Jumamosi kwa Afrika Mashariki.
Ushindi huo umeifanya New York kuongoza mfululizo wa fainali kwa michezo miwili kwa sifuri (2-0), ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo kupata uongozi wa aina hiyo kwenye Fainali za NBA.
“Mchezo ulikuwa wa ajabu,” anasema kocha wa Knicks, Mike Brown. Karl-Anthony Towns alikuwa nyota mwingine wa Knicks baada ya kufunga pointi 21 na kuokota ‘rebounds’ 13 huku Brunson na Mikal Bridges kila mmoja akifunga pointi 20.
Knicks sasa wamefikisha ushindi wa 13 mfululizo kwenye hatua ya mtoano, rekodi ambayo ni ya pili katika historia ya NBA Playoffs. “Jiji la New York limejitokeza. Mashabiki wamejitokeza. Hamasa imejitokeza na tumepata njia ya kushinda,” anasema Towns.
Kwa ushindi huo, Knicks wamekuwa timu ya tatu pekee katika historia ya NBA kushinda michezo miwili ya kwanza ya Fainali wakiwa ugenini. Wameungana na Chicago Bulls ya Michael Jordan iliyofanya hivyo mwaka 1993 pamoja na Houston Rockets ya Hakeem Olajuwon mwaka 1995.
Timu hizo zote mbili zilimaliza kwa kutwaa ubingwa. Bulls waliwashinda Phoenix Suns katika michezo sita huku Rockets wakiifagia Orlando Magic kwa ushindi wa 4-0. Knicks, ambao wanasaka ubingwa wao wa kwanza tangu mwaka 1973, sasa wako katika nafasi nzuri ya kufuata nyayo hizo. Kwa upande wa Spurs, Wembanyama aliamka katika kipindi cha pili baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu na kumaliza mchezo akiwa na pointi 29. De’Aaron Fox naye alichangia pointi 20. “Hatuwezi kubadilisha yaliyopita. Tayari tunafikiria Mchezo wa Tatu,” anasema Wembanyama. Sasa mfululizo huo unahamia New York ambapo Mchezo wa tatu utapigwa Jumatatu usiku katika ukumbi maarufu wa Madison Square Garden.
Kutokana na hamasa kubwa ya mashabiki, tiketi za viti vya bei nafuu zaidi katika soko la pili zilikuwa zikizidi dola 11,000 za Marekani (zaidi ya Shilingi 29 milioni), ishara kwamba mashabiki wa Knicks wako tayari kulipa gharama yoyote kushuhudia timu yao ikikaribia ubingwa wa kwanza baada ya miaka 53.
Spurs walionyesha mapambano makubwa katika robo ya mwisho baada ya kuwa nyuma kwa pointi 14. Walifunga pointi 14 mfululizo na kusawazisha mchezo kabla ya Wembanyama kufanikisha mchezo wa pointi tatu uliowapa uongozi wa 104-102 zikiwa zimesalia sekunde 57.
“Tulionyesha ari kubwa, uharaka na ushindani wa hali ya juu. Tunahitaji kuendeleza kiwango hicho katika mchezo unaofuata,” anasema kocha wa Spurs, Mitch Johnson.
Hata hivyo, Knicks walimalizia kwa nguvu. Brunson ambaye pia alikuwa shujaa wa ushindi katika mchezo wa Kwanza, alifunga pointi tatu za mwisho za timu yake. Baada ya kusawazisha mchezo, Knicks walipata nafasi nyingine ya kushambulia. Spurs walifanikiwa kuzuia shambulizi hilo lakini Wembanyama akapoteza mpira muhimu. Brunson akafanyiwa madhambi na kufunga mikwaju ya adhabu iliyoirudisha Knicks mbele.
Spurs waliomba muda wa mapumziko zikiwa zimesalia sekunde 7.5. Fox alipokea mpira kutoka pembeni na kumtengenezea Wembanyama nafasi ya mtupio wa ushindi. Lakini mtupio huo uligonga pete na kutoka nje na ndoto za Spurs za kusawazisha mfululizo zikayeyuka papo hapo.
“Tulihitaji kuzuia shambulizi moja tu. Hatukuwa tumefanikiwa kufanya hivyo robo nzima ya mwisho,” anasema Towns baada ya ushindi huo muhimu.
Sasa Knicks wanarejea nyumbani wakiwa na uongozi wa 2-0 na wakibakiwa na ushindi wa mechi mbili pekee kutwaa ubingwa wa kwanza wa NBA tangu mwaka 1973.