Wakongwe waliotisha klabu bingwa ya Dunia

Muktasari:
- Michuano hii iliyoanzishwa mwaka 2000 ina rekodi nyingi ambazo ziliwahi kuwekwa na zile zinazotarajiwa kuwekwa.
FLORIDA, MAREKANI: SIKU zinazidi kukatika kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia la Klabu linalotarajiwa kupigwa huko Marekani, Juni 15 mwaka huu.
Michuano hii iliyoanzishwa mwaka 2000 ina rekodi nyingi ambazo ziliwahi kuwekwa na zile zinazotarajiwa kuwekwa.
Leo tumekusogezea wachezaji wenye umri mkubwa zaidi kuwahi kucheza michuano hii.
11. Emiliano Tade (Argentina)
Umri: Miaka 36
Timu: Auckland City
Mwaka: 2017
Tade alikuwa mshambuliaji tegemeo wa Auckland City, alishiriki mashindano haya kwa miaka saba mfululizo kuanzia mwaka 2011 hadi 2017. Alifunga mabao muhimu kwa timu yake, akiweka alama kubwa kwenye historia ya Kombe la Dunia la Klabu kwa timu za Oceania. Licha ya kupoteza dhidi ya Al Jazira katika mchezo wa raundi ya kwanza mwaka 2017, mchango wake katika kikosi cha Auckland City ulikuwa wa kipekee na hadi sasa anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi kwa timu hiyo kwenye michuano ya dunia.
10. Luka Modric (Croatia)
Umri: Miaka 37
Timu: Real Madrid
Mwaka: 2022 (michuano ilichezwa Februari 2023)
Luka Modric alikuwa sehemu ya kikosi kilichoisaidia Real Madrid kutwaa taji la tano la michuano hii mwaka 2022.
Katika michuano ya mwaka huu anatarajiwa kuweka rekodi nyingine ya kuwa miongoni mwa wachezaji wa umri mkubwa zaidi kucheza michuano hiyo kwani mara ya mwisho alikuwa na miaka 37 na sasa ana miaka 39. Klabu yake imeshamuaga kwamba msimu ujao hatakuwapo Bernabeu.
9. Lee Dong-gook (Korea Kusini)
Umri: Miaka 37
Timu: Jeonbuk Hyundai Motors
Mwaka: 2016
Lee alikuwa na historia ndefu ya kushiriki mashindano makubwa, ikiwa ni pamoja na Kombe la Dunia 1998 na 2010. Katika Kombe la Dunia la Klabu, licha ya umri wake, aliendelea kuwa tishio katika safu ya ushambuliaji. Alifunga mabao zaidi ya 200 katika ligi ya Korea na ni mchezaji mwenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya timu ya Jeonbuk. Mara ya mwisho kuonekana katika michuano hii ilikuwa mwaka 2016 ambapo alicheza mechi ya robo fainali dhidi ya Club America na wakapoteza kwa mabao 2-1.
8. Daniel Koprivcic (New Zealand)
Umri: Miaka 37
Timu: Auckland City
Mwaka: 2014
Ni miongoni mwa mastaa walioshiriki michuano hii mara nyingi zaidi. Ameweka rekodi ya kuonekana mara sita na mara ya mwisho mwaka 2014 aliingia pia katika historia ya wachezaji 'wazee' zaidi kuwahi kucheza michuano hii.
Alikuwa kiungo wa kati aliyeiongoza Auckland City kuwa klabu yenye mafanikio.
7. Javier Zanetti (Argentina)
Umri: Miaka 37 na siku 127
Timu: Inter Milan
Mwaka: 2010
Zanetti aliweka historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga bao katika michuano hii. Alikuwa beki wa pembeni mwenye uwezo wa kushambulia na kurudi haraka, pia alihudumu kama nahodha wa Inter kwa zaidi ya muongo mmoja.
Aliweka rekodi ya kucheza michuano akiwa na umri mkubwa mwaka 2010 ambapo aliiwezesha Inter kufika hadi fainali ikiichapa TP Mazembe mabao 3-0 na kuchukua taji lao la tatu la msimu.
6. Paolo Maldini (Italia)
Umri: Miaka 39
Timu: AC Milan
Mwaka: 2007
Maldini, anakumbukwa kama mmoja kati ya mabeki bora wa muda wote. Aliiongoza AC Milan kutwaa taji la michuano hii mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 39 ambapo walifika na fainali na kuichapa Boca Juniors.
Alikuwa mfano wa uongozi, nidhamu na uaminifu, akicheza kwa maisha yake yote ya soka katika kikosi cha AC Milan. Ushiriki wake katika michuano hii ilikuwa sehemu ya kutoa heshima kwa safari yake ya soka akiwa na Milan.
5. Ante Covic (Australia)
Umri: Miaka 39
Timu: Western Sydney Wanderers
Mwaka: 2014
Alishiriki michuano hii baada ya kuiwezesha Western Sydney Wanderers kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Asia mwaka 2014 kwa kuichapa Al-Hilal ya Saudi Arabia.
Katika michuano ya mwaka huo, Covic ambaye aliwahi kuwa kipa katika timu mbalimbali za Ulaya, aliiwezesha timu hiyo kufika robo fainali ambapo ilipoteza dhidi ya Cruz Azul ya Mexico kwa kichapo cha mabao 3-1 baada ya dakika 120.
4. Miguel Calero (Colombia)
Umri: Miaka 39
Timu: Pachuca
Mwaka: 2008
Calero alikuwa kipa maarufu kwa wakati wake, uwezo wa kuruka na kuokoa mipira iliyoonekana kwenda kuzaa mabao ulizidisha umaarufu wake.
Alikuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya Pachuca katika mashindano ya kimataifa. Pia aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Colombia kwa mafanikio, ikiwa ni pamoja na kushinda Copa America mwaka 2001. Alistaafu muda mfupi baada ya michuano hii kabla ya kufariki dunia mwaka 2012.
3. Mitsuo Ogasawara (Japan)
Umri: Miaka 39
Timu: Kashima Antlers
Mwaka: 2016
Ogasawara alikuwa kiungo wa kiufundi aliyeshiriki Kombe la Dunia akiwa na Japan mara mbili (2002, 2006), na alikuwa mhimili wa eneo lao la kiungo kwa klabu na timu ya taifa kwa karibia miongo miwili.
Katika michuano ya Kombe la Dunia ya Klabu mwaka 2016, aliiongoza Kashima Antler kufika fainali kwa mara ya kwanza na kuweka historia kuwa timu ya kwanza ya Japan kufanya hivyo.
Katika fainali waliyocheza dhidi ya Real Madrid walifanya vizuri na mechi ikaenda kuamuliwa katika muda wa dakika 30 za ziada ambapo walipoteza kwa mabao 4-3.
2. Ivan Vicelich (New Zealand)
Umri: Miaka 40
Timu: Auckland City
Mwaka: 2016
Vicelich alikuwa nguzo ya ulinzi ya timu ya Auckland City kwa zaidi ya muongo mmoja, na pia ni mmoja wa wachezaji waliochezea mechi nyingi zaidi timu ya taifa ya New Zealand.
Katika michuano ya Club World Cup ya mwaka 2016, uzoefu wake ulisaidia timu kuhimili presha dhidi ya wapinzani kutoka mabara mengine. Aliwahi pia kushiriki Kombe la Dunia 2010, na alisifika kwa nidhamu yake ya hali ya juu uwanjani.
1. Oscar Perez (Mexico)
Umri: Miaka 44 na miezi 10
Timu: Pachuca
Mwaka: 2017
Aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kucheza michuano ya Kombe la Dunia la Klabu mwaka 2017 akiwa na Pachuca ya Mexico na hadi sasa ndio anashikilia rekodi hiyo.
Perez, jina lake la utani ni El Conejo, aliishangaza dunia kwa wakati huo baada ya kushiriki mashindano haya akiwa na karibu miaka 45.
Uzoefu wake mkubwa na uongozi ndani ya uwanja viliisaidia Pachuca kuwapa wachezaji wachanga ujasiri mkubwa. Aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Mexico kwenye Kombe la Dunia mara tatu (1998, 2002, 2010), na michuano hii ilikuwa hitimisho la heshima kwa kazi yake ndefu ya zaidi ya miaka 25 katika soka la ushindani.