Wakala ampeleka Silva Madrid
Muktasari:
- Mkataba wa nyota huyo unatarajiwa kumalizika Juni 30, na tayari imeshatangazwa kuwa ataondoka katika viunga vya Etihad ifikapo mwisho wa msimu huu, jambo lililosababisha kuhusishwa na timu nyingi ndani na nje ya Ulaya.
JORGE Mendes, wakala wa kiungo Bernardo Silva ameripotiwa kupiga simu Real Madrid na kuwaambia kuwa staa huyo wa Manchester City mwenye umri wa miaka 31, angependa kujiunga na timu hiyo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mkataba wa nyota huyo unatarajiwa kumalizika Juni 30, na tayari imeshatangazwa kuwa ataondoka katika viunga vya Etihad ifikapo mwisho wa msimu huu, jambo lililosababisha kuhusishwa na timu nyingi ndani na nje ya Ulaya.
Silva ambaye awali aliwahi pia kuhusishwa na Barcelona hadi sasa bado hajafanya uamuzi wa timu gani ataichezea kwa msimu ujao na anaendelea kuchambua ofa ambazo zimewasilishwa mezani.
Kuna wakati fulani matajiri kutoka Saudi Arabia waliripotiwa kuhitaji huduma yake, lakini staa huyo alionekana kuwa bado anahitaji kuendelea kucheza soka la ushindani barani Ulaya.
Ikiwa mpango wa kutua Hispania utafeli, kuna asilimia nyingi Silva akacheza Ligi Kuu Italia (Serie A) msimu ujao ambapo tayari Juventus na Napoli ni miongoni mwa timu zinazoonekana kumhitaji.
Inaelezwa kwamba Napoli imekuwa ikimtumia kiungo wake, Kevin de Bruyne, kumshawishi Silva akubali kujiunga na timu hiyo kutokana na ukaribu walionao.
Morgan Rogers
KIUNGO mshambuliaji wa Aston Villa na England, Morgan Rogers, 23, yupo tayari kucheza nje ya England msimu ujao na tayari PSG imeanza kuwania saini yake. Fundi huyo ambaye pia anawindwa Arsenal, Man United na Chelsea anaonekana kuvutiwa zaidi na mpango wa kujiunga na PSG akiamini itampa nafasi kubwa zaidi ya kuitwa katika timu ya taifa ya England. Licha ya vigogo hao kuonyesha nia ya kumsajili, Villa hawatarajiwi kirahisi.
Manuel Akanji
BEKI wa Manchester City na timu ya taifa ya Uswisi, Manuel Akanji, 30, anatarajiwa kujiunga moja kwa moja na Inter Milan katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kufikia makubaliano. Taarifa zinaeleza kuwa Inter wamekubaliana kulipa takriban Euro 15 milioni ili kumsainisha mkataba wa moja kwa moja baada ya kuhudumu kwa mkopo. Akanji amekuwa mchezaji muhimu kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi za safu ya ulinzi.
Teun Koopmeiners
MANCHESTER United inajindaa kuwasilisha ofa Juventus ili kuipata saini ya kiungo wa Uholanzi, Teun Koopmeiners, 28, katika dirisha lijalo. Koopmeiners anaweza kucheza kama namba sita na nane, na klabu yake inahitaji zaidi ya Pauni 40 milioni ili kumuuza. Kiasi hicho kinaonekana kuwa kikubwa kwa timu zinazomhitaji, hivyo kwa sasa zinafanya mazungumzo na wawakilishi wa pande mbili ili kupunguziwa bei.
Elliot Anderson
MANCHESTER City bado ina imani kubwa kumsajili kiungo wa England, Elliot Anderson, 23, kutoka Nottingham Forest dirisha lijalo. Taarifa zinaeleza dili hilo linaweza kuigharimu Man City hadi Pauni 100 milioni kutokana na ushindani kutoka klabu nyingine zinazomhitaji nyota huyo. Anderson ameendelea kuwa katika rada za timu nyingi England kutokana na ubora aliouonyesha tangu msimu uliopita. Mbali ya Man City, anawindwa na Man United.
James Trafford
BRIGHTON inaangalia uwezekano wa kumsajili kipa wa Manchester City na timu ya taifa ya England, James Trafford, 23, katika dirisha la majira ya kiangazi. Trafford anatafuta timu itakayompa nafasi zaidi ya kucheza mara kwa mara, jambo ambalo limekuwa changamoto Manchester City kutokana na ushindani uliopo. Brighton imemhakikishia kuwa atakuwa kipa namba moja ikiwa atakubali kujiunga nayo.
Joao Gomes
ATLETICO Madrid imefungua mazungumzo na Wolves kumsajili kiungo wa Kibrazili Joao Gomes, 25, dirisha lijalo. Taarifa zinaeleza Wolves itahitaji Pauni 40 milioni ili kumuza. Gomes anadaiwa kutotaka kusalia Wolves kwa sababu anataka kucheza Ligi Kuu msimu ujao na timu hiyo tayari imeshashuka. Hakuna makubaliano yaliyofikiwa ingawa Atletico ina nafasi kubwa ya kumchukua.
Lorenzo Lucca
MSHAMBULIAJI wa Napoli na timu ya taifa ya Italia, Lorenzo Lucca, 27, anayecheza kwa mkopo Nottingham Forest anatarajiwa kurejea baada ya mkataba wa mkopo kumalizika. Forest, ambayo ilikuwa na chaguo la kumnunua moja kwa moja imeamua kutofanya hivyo kwa sababu haijavutiwa na kiwango alichoonyesha. Lucca alitamani kuendelea kusalia Forest kwani anaamini bado ana nafasi ya kufanya vizuri.