Vigogo England wampigia hesabu Darwin Nunez
Muktasari:
- Nunez ambaye aliwahi kucheza Liverpool anaonekana kuwa mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa kutokana na kasi na kiwango bora alichoonyesha Saudia.
NEWCASTLE United na Chelsea zipo katika vita ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Al-Hilal ya Saudi Arabia na timu ya taifa ya Uruguay, Darwin Nunez, 26, ili kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Nunez ambaye aliwahi kucheza Liverpool anaonekana kuwa mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa kutokana na kasi na kiwango bora alichoonyesha Saudia.
Newcastle na Chelsea zinaamini kumsajili Nunez kutakuwa na faida nyingi ikiwemo ile ya kuwa na uzoefu wa Ligi Kuu England, hivyo haitamchukua muda mrefu kuingia katika mifumo. Staa huyo kwa sasa anadaiwa kuwa yupo tayari kurudi England, lakini hataki kulazimisha hivyo timu itakayofikia makubaliano na Al-Hilal ndio itakayomchukua.
Hata hivyo, ikiwa atahitaji kutua England atatakiwa kukubali kupunguziwa mshahara wake anaoupata wa Pauni 400,000 kwa wiki. Mkataba wa sasa wa Nunez na Al-Hilal unatarajiwa kumalizika 2028, msimu huu amecheza mechi 24 michuano yote na kufunga mabao tisa.
Joao Gomes
ATLETICO Madrid iko karibu kufikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa Wolves, Mbrazili Joao Gomes, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Inaripotiwa kuwa dili hilo linaweza kuigharimu Pauni 39 milioni na tayari makubaliano binafsi kati ya mchezaji na wawakilishi wa wababe hao wa Madrid yameshafanyika. Gomes anadaiwa kuwaambia mabosi wa Wolves kwamba hatasalia kikosini sababu hatakii kucheza Championship.
Guglielmo Vicario
INTER Milan inafikiria kuachana na mpango wa kumsajili kipa wa Tottenham Hotspur na Italia, Guglielmo Vicario, 29, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na badala yake kusajili maeneo mengine. Taarifa zinaeleza Inter ambayo ilitajwa kufikia makubaliano binafsi na wawakilishi wa Vicario, imebadilisha mpango kwa sababu bajeti haitoshi, hivyo inatazamia maeneo muhimu zaidi kwa sasa ambayo yanaonekana kuwa na upungufu zaidi tofauti na langoni.Mkataba wa sasa wa Vicario unatarajiwa kumalizika 2028.
Dusan Vlahovic
DUSAN Vlahovic, 26, anatarajiwa kuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Juventus kumalizika dirisha lijalo la kiangazi. Straika huyo wa kimataifa wa Serbia anaripotiwa kusubiri kama Barcelona au Bayern Munich zitapiga hodi ili kumsajili. Vlahovic ni miongoni mwa washambuliaji wanaowindwa na klabu nyingi Ulaya licha ya kutokuwa katika kiwango bora hivi karibuni kutokana na majeraha mara kwa mara.
Lois Openda
LEEDS United wanaonekana kuwa mbele katika mbio za kumsajili mshambuliaji wa Juventus na Ubelgiji, Lois Openda, 26. Hata hivyo, Coventry City pia imeonyesha nia ya kumsajili nyota huyo ambaye inaaminia atasaidia kikosi hicho katika Ligi Kuu England msimu ujao. Kwa upande wa Leeds, Openda ambaye msimu huu amecheza mechi 37 za michuano yote na kufunga mabao mawili ameahidiwa kuwa atakuwa kipaumbele safu ya ushambuliaji.
Jannik Schuster
BRIGHTON, Leeds United na West Ham United zinaweza kujaribu kuvuruga mpango wa Brentford wa kumsajili beki raia wa Austria, Jannik Schuster, 19, kutoka Red Bull Salzburg katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Brentford ilionekana kuwa mbele katika mbio hizo, lakini ushindani kutoka klabu nyingine za England unaonekana kufanya dili hilo kuwa gumu zaidi. Mkataba wa sasa wa Schuster, unatarajiwa kumalizika 2028.
Maxime Esteve
EVERTON italazimika kuongeza juhudi ikiwa inataka kumsajili beki wa Burnley, Mfaransa Maxime Estève, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Taarifa zinadai kuna asilimia nyingi za Spurs kushindwa kumsajili baada ya Leverkusen kudaiwa kuitamani saini yake na kuanza mazungumzo ili kumsajili. Esteve ameendelea kuvutia vigogo wengi Ulaya kutokana na uimara wake.
Josko Gvardiol
MANCHESTER City wako kwenye mazungumzo na beki wa kimataifa wa Croatia, Josko Gvardiol, 24, juu ya kumuongeza mkataba. Man City wanaonekana kupambana ili kuhakikisha huduma ya beki huyo inabakia muda mrefu kwani wameshaanza kuona baadhi ya timu zikianza kumnyemelea. Gvardiol ana uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi mbali ya majukumu yake ya kukaba.