Ukiwataka hawa hata Pauni 70M haifiki
Muktasari:
- Liverpool inaweza kuingia dirisha lijalo la usajili ikiwa bingwa wa Ligi Kuu England, wakati Arsenal yenyewe itaingia kwenye kipindi hicho ikisaka straika wa kwenda kuboresha kikosi chao, sawa na Man United, ambayo kwa sasa inapambana kwanza kubaki kwenye Ligi Kuu England kabla ya kufikiria nani wa kumsajili.
LONDON, ENGLAND: LIVERPOOL, Manchester United na Arsenal zinasubiri dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa mitazamo tofauti, lakini ukweli hakuna timu itafumbia macho dili la kunasa mchezaji wa maana kwa bei ndogo.
Liverpool inaweza kuingia dirisha lijalo la usajili ikiwa bingwa wa Ligi Kuu England, wakati Arsenal yenyewe itaingia kwenye kipindi hicho ikisaka straika wa kwenda kuboresha kikosi chao, sawa na Man United, ambayo kwa sasa inapambana kwanza kubaki kwenye Ligi Kuu England kabla ya kufikiria nani wa kumsajili.
Kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, kuna mastaa sita matata kabisa ambao wanaweza kupatikana kwa bei hata isiyofika Pauni 70 milioni kutokana na vipengele vilivyomo kwenye mikataba yao.
1.Harry Kane - Pauni 67 milioni; Kurudi kwenye Ligi Kuu England kwenda kuvunja rekodi ya mabao ya Alan Shearer ni kitu ambacho kipo kwenye mpango wa Kane. Na kitu kizuri kuhusu straika huyo ni kwamba anafikika kutokana na kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake huko Bayern Munich, kwamba kwenye dirisha lijalo, timu inaweza kumsajili kwa Pauni 67 milioni tu. Na bei hiyo inaweza kushuka hadi Pauni 54 milioni.
2.Matheus Cunha - Pauni 62 milioni; Staa huyo wa Wolves amesaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Molineux hivi karibuni, lakini hilo halina maana kwamba hawezi kuhama mwisho wa msimu. Kinachoelezwa ni kwamba kwa timu ambayo itahitaji huduma yake kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, Cunha, anaweza kunaswa kwa Pauni 62 milioni tu kutokana na kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake na kutaja bei.
3.Eberechi Eze - Pauni 68 milioni; Fowadi huyo wa Crystal Palace, kipengele kilichopo kwenye mkataba wake kinataja kwamba bei atakayouzwa mkali huyo kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi ni Pauni 68 milioni. Palace ilimpiga bei Michael Olise kwenda Bayern Munich dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, kitu ambacho kinaweza kuwashuhudia wakiachana na staa wao mwingine wa Selhurst Park mwaka huu.
4.Dean Huijsen - Pauni 50 milioni; Staa huyo wa Bournemouth amezivutia timu nyingi sana kutokana na kiwango chake cha uwanjani na kinachofurahisha ni kwamba kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachotaja bei atakayouzwa kuwa ni Pauni 50 milioni. Timu kibao zinahitaji huduma yake kama Malaga, Juventus na AS Roma na kwa kiwango cha mchezaji huyo, kuuzwa kwa bei hiyo anayouzwa ni ya kutupa.
5.Victor Osimhen - Pauni 65 milioni; Nyakati za Mnigeria huyo kwenye kikosi cha Napoli zimefika mwisho baada ya ujio wa kocha Antonio Conte, ambaye ameamua kufanya kazi na straika Romelu Lukaku. Osimhen kwa sasa yupo kwa mkopo huko Galatasaray, lakini itakapofika mwisho wa msimu straika huyo anaweza kupatikana kwa ada ya Pauni 65 milioni tu kutokana na kipengele kilichopo kwenye mkataba wake kinavyoeleza.
6.Nico Williams - Pauni 48 milioni; Alikuwa mmoja wa mastaa wa maana kwenye Euro 2024 alipoisaidia Hispania kunyakua ubingwa na timu nyingi zilimtaka, lakini aliamua kubaki Athletic Bilbao. Hata hivyo, habari itakuwa tofauti kwenye dirisha lijalo, ambapo kuna timu kibao zinapambana kumng'oa San Mames na kinachorahisisha hilo ni bei yake anayouzwa, Pauni 48 milioni kwa mujibu wa kipengele cha kwenye mkataba.