Uefa Nations League… Kila kitu kipo hapa

Muktasari:
- Rekodi na mambo mengi vimetokea katika michuano hiyo na hapa tumekuwekea mchanganuo kamili kuanzia zawadi, mfumo ulivyokuwa, wafungaji na kila kitu kinachohusu michuano hii ambayo fainali yake ilipigwa pale Allianz Arena, jijini Munich, Ujerumani.
MUNICH, UJERUMANI: MICHUANO ya Uefa Nations League ilimalizika juzi kwa Ureno kushinda taji hilo mbele ya Hispania katika mchezo ambao mikwaju ya penalti ilitumika kuamua mshindi baada ya kutoshana nguvu kwa mabao 2-2.
Rekodi na mambo mengi vimetokea katika michuano hiyo na hapa tumekuwekea mchanganuo kamili kuanzia zawadi, mfumo ulivyokuwa, wafungaji na kila kitu kinachohusu michuano hii ambayo fainali yake ilipigwa pale Allianz Arena, jijini Munich, Ujerumani.

REKODI ZILIZOWEKWA
-Ureno imekuwa timu ya kwanza kuwahi kushinda UEFA Nations League mara mbili (2019 na sasa 2025).
-Cristiano Ronaldo, akiwa na umri wa miaka 40, alifunga goli kwenye fainali, akiweka rekodi kama mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga katika fainali ya michuano hiyo.
-Hispania imeweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa mashindano haya na imefunga mabao 25 katika mechi 10.
-Ronaldo alifikisha mabao 138 ya timu ya taifa, akizidi kuongeza idadi katika rekodi yake ya mfungaji bora wa muda wote.
-Rodrigo Mora ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi (miaka 18 na siku 34), kushinda taji la Nations League.

MFUMO ULIVYO
Jumla ya timu 55 zinashiriki michuano hii ambayo ina ligi nne tofauti ambazo ni A, B, C na D.
Ligi A, B na C zinakuwa na makundi manne ya timu nne, wakati League D ikiwa na makundi mawili ya timu tatu.
Kila timu inacheza michezo ya 'nyumbani na ugenini' dhidi ya timu nyingine kwenye kundi lake.
Katika ligi A, bingwa wa kila kundi (manne) na mshindi wa pili ziliingia hatua ya robo fainali na zilicheza mechi za nyumbani na ugenini na kuendelea hadi nusu fainali, mshindi wa tatu na fainali.
Timu tatu, mabingwa wa ligi B, C, D zinapanda kwenda ligi ya juu yake, wakati timu mbili zinazoishia nafasi ya mwisho katika ligi A, B na C hushuka ligi ya chini, huku zinazomaliza nafasi ya tatu zinacheza mtoano wa kubaki.
Zinazomaliza nafasi ya pili katika ligi ya Kundi B zinacheza mtoano wa kupanda Ligi A.
Timu za nafasi ya tatu katika Ligi B makundi, zinacheza mtoano wa kujinusuru kushuka Ligi C.
Ligi C, mshindi kila kundi inapanda Ligi B, wakati mshindi wa pili anacheza mtoano wa kupanda na wa tatu inabaki katika kundi huku ya nne ikiteremka hadi Ligi D.
Ligi D, mshindi inapanda Ligi C huku ya pili ikicheza mtoano wa kupanda na ya tatu inabaki katika kundi kusubiri zinazoshuka msimu ujao.

JE WASHINDI WAMEFUZU KOMBE LA DUNIA?
Kushinda taji la michuano hii au kufanya vizuri hakukuhakikishi nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia lakini kwa timu zilizofika nusu fainali katika ligi A zina faida kidogo.
Ipo hivi, kawaida timu zinazomaliza nafasi za kwanza katika kila kundi kwenye mashindano ya kuwania kufuzu Kombe la dunia huwa zinafuzu moja kwa moja huku zile zinazomaliza nafasi ya pili huitaji kucheza mechi ya mtoano ili kupata timu nyingine nne zitakazoungana na zile 12 kutimizia idadi ya timu 16 ambazo hushiriki Kombe la Dunia kutokea Ulaya.
Sasa ikiwa timu nne zilizofika nusu fainali kwenye Nations League hazitomaliza nafasi ya kwanza au ya pili kwenye mechi hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia, huwa zina nafasi ya kucheza mechi za mtoano na timu zilizoshika nafasi ya pili katika makundi ya mashindano hayo.
Hata hivyo, kama timu zilizofika nusu fainali kwenye Nations League zitafuzu moja kwa moja au baadhi zitafuzu na nyingine zitashindwa, ili kujazia nafasi zilizoachwa wazi, zitachukuliwa timu zilizofanya vizuri kuzifuatia hizo nne katika Nations League ikiwa nazo zimeshindwa kufuzu moja kwa moja kucheza Kombe la Dunia.

WAFUNGAJI
Mfungaji bora wa ligi zote kwa jumla ni staa wa Sweden, Viktor Gyokeres ambaye amefunga mabao tisa katika ligi C, akifuatiwa na Cristiano Ronaldo aliyefunga manane akiwa na Ureno kwenye ligi A na nafasi ya tatu inashikiliwa na Erling Haaland mwenye saba na taifa lake la Norway linaloshiriki ligi B.
Mbali ya mabao, katika asisti, kinara ni Joshua Kimmich wa Ujerumani aliyetoa asisti sita, akifuatiwa na staa wa Ureno, Nuno Mendes mwenye tano.
ZAWADI
Kwa timu 16 zinashoriki ligi A kila moja hupata Euro 2.5 milioni, kwa upande wa ligi B ambako pia kuna timu 16 kila moja hupata, Euro 1.50 milioni, ligi (timu 16) ni Euro 1.125 milioni na upande wa ligi D ambako kuna timu saba kila moja hukunja Euro 700,000.
Mbali ya pesa za ushiriki, pia kila mshindi wa kwanza wa kila kundi kwa ligi A hupata Euro 2.25 milioni, ligi B hupata Euro 1.50 milioni, ligi C ni Euro 1.125 milioni na ligi D ni Euro 700,000.
Vile vile huwa kuna zawadi kwa upande wa ligi A ambazo hutolewa kwa mshindi wa fainali na Ureno imepata Euro 6 milion, mshindi wa pili Hispania imekunja Euro 4 milioni, mshindi wa tatu Ufaransa (Euro 3 milioni) na Ujerumani ni ya nne imepata Euro 2 milioni.
Hivyo kijumla Ureno inakadiriwa kupata Euro 10.5 milioni, wakati Hispania ikipata Euro 9 milioni.

ZILIZOPANDA LIGI A
Jumla ya timu saba zilipanda daraja kwenda ligi A msimu ujao baada ya kumaliza zikiwa vinara wa makundi katika ligi B.
Timu hizo ni Jamhuri ya Czech, England, Norway na Wales.
Pia kuna timu zilizopanda daraja baada ya kushinda mechi za mtoano ambazo ni Ugiriki iliyoichapa Scotland kwa jumla ya mabao 3-1, Uturuki iliyoshinda 6‑1 dhidi ya Hungary na Serbia ambao waliowaondosha Austria kwa matokeo ya jumla ya mabao 3‑1.