Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uamuzi wa CAF wazua utata mwingi

CAF Pict

Muktasari:

  • Alhamisi ya Oktoba 29, Kamati ya Utendaji ya CAF ilipitisha kwa kauli moja uamuzi wa kuachana na mpango wa kuandaa AFCON kila baada ya miaka minne, uliotangazwa Desemba 2025.

CAIRO, MISRI: Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limerejesha rasmi mfumo wa kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kila baada ya miaka miwili, lakini ratiba mpya ya mashindano hayo imeibua maswali kuhusu namna mfumo huo utakavyotekelezwa.

Alhamisi ya Oktoba 29, Kamati ya Utendaji ya CAF ilipitisha kwa kauli moja uamuzi wa kuachana na mpango wa kuandaa AFCON kila baada ya miaka minne, uliotangazwa Desemba 2025.

Hata hivyo, ratiba iliyotangazwa inaonyesha matoleo manne yajayo ya mashindano hayo yatafanyika mwaka 2027, 2028, 2031 na 2033. Hali hiyo imeibua swali la msingi: ikiwa AFCON imerejea kwenye mfumo wa miaka miwili, kwa nini kutakuwa na pengo la miaka mitatu kati ya mashindano ya 2028 na 2031?

Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, uamuzi huo umetokana na tathmini upya ya mkakati wa mashindano ya shirikisho hilo. Mpango wa awali wa kuandaa AFCON kila baada ya miaka minne ulitangazwa Desemba 2025, ukiwa sehemu ya mabadiliko ya kalenda ya soka Afrika na kuanzishwa kwa Ligi ya Mataifa ya Afrika.

Hata hivyo, mpango huo ulikosolewa kutokana na hofu ya kuathiri timu za taifa, fursa za kibiashara na nafasi ya AFCON katika maendeleo ya soka la Afrika.

CA 04

Rais wa CAF, Patrice Motsepe, alifungua tena mjadala kuhusu muda wa kuandaa mashindano hayo wakati wa mkutano wa mkakati wa shirikisho hilo nchini Cape Verde mapema mwezi uliopita. Uamuzi wa Oktoba 29 sasa umefuta rasmi mpango wa miaka minne.

Ratiba mpya inaonyesha AFCON 2027 itafanyika Kenya, Tanzania na Uganda, ikifuatiwa na toleo la 2028, kisha 2031 na 2033. Pengo la mwaka mmoja kati ya 2027 na 2028, na miaka mitatu kati ya 2028 na 2031, linafanya mpangilio huo usiwe wa kawaida.

Kwa mfumo wa miaka miwili unaoanzia 2027, ratiba inayotarajiwa ingekuwa 2027, 2029, 2031 na 2033. Vilevile, kama mfumo huo ungeanzia 2028, matoleo yaliyofuata yangekuwa 2030, 2032 na 2034.

CAF imeeleza kuwa AFCON haitafanyika mwaka 2030 kwa sababu mwaka huo kutakuwa na Fainali za Kombe la Dunia, lakini haijaweka wazi kwa nini mwaka 2029 haupo kwenye ratiba iliyotangazwa wala namna itakavyohamishia mashindano hayo kwenye mfumo wa kawaida wa miaka miwili.

Hata hivyo, pengo la miaka mitatu kati ya 2028 na 2031 halimaanishi kuwa CAF imeamua kuandaa AFCON kila baada ya miaka mitatu. Badala yake, linaonyesha kuwa ratiba ya mpito kuelekea mfumo mpya bado haijawekwa wazi kikamilifu.

Sababu kubwa iliyochangia CAF kubadili msimamo wake ni masuala ya kifedha. Awali, shirikisho hilo lilipendekeza kuanzisha Ligi ya Mataifa ya Afrika ili kutoa fursa za mara kwa mara kwa timu za taifa kushindana na kuongeza mapato kwa vyama wanachama.

CA 01

Hata hivyo, CAF imekubali kuwa mashindano hayo mapya yangehitaji miaka kadhaa kabla ya kuanza kuzalisha fedha za kutosha kusaidia maendeleo ya soka la Afrika.

Motsepe ameeleza kuwa kuendelea kuandaa AFCON katika mfumo wake wa kawaida kutasaidia kulinda maslahi ya vyama 54 wanachama wa CAF pamoja na wachezaji wa Afrika wanaocheza katika klabu za nje ya bara hili.

AFCON si mashindano ya kuwania ubingwa wa bara pekee, bali pia ni chanzo muhimu cha mapato, matangazo ya televisheni na fursa za kibiashara kwa vyama vya soka. Kupunguza idadi ya matoleo yake kunaweza kuathiri manufaa hayo.

Hata hivyo, CAF bado haijaeleza kwa kina hatma ya Ligi ya Mataifa ya Afrika, iwapo itaendelea kama ilivyopangwa, itafanyiwa mabadiliko au kuachwa kabisa.

CA 03

Mabadiliko hayo pia yameibua maswali kuhusu maandalizi ya nchi zitakazoandaa matoleo yajayo ya AFCON. Julai 2026, CAF ilialika vyama wanachama kuwasilisha maombi ya kuandaa mashindano ya mwaka 2028, 2032 na 2036.

Lakini ratiba mpya iliyotangazwa Oktoba inaonyesha matoleo ya 2028, 2031 na 2033, jambo linaloibua sintofahamu kuhusu namna mchakato wa awali wa kuwania uenyeji utakavyorekebishwa.

Kwa nchi zinazotaka kuandaa AFCON, ratiba thabiti ni muhimu katika kupanga uwekezaji wa viwanja, miundombinu ya usafiri, malazi na usalama. Mabadiliko ya mara kwa mara yanaweza kufanya maandalizi ya muda mrefu kuwa magumu, hasa kwa nchi ambazo tayari zimeanza mchakato wa kuwania uenyeji.

CA 02

Kwa sasa, AFCON 2027 haijaathiriwa na mabadiliko hayo. Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, yakiongozwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda. Hiyo itakuwa mara ya kwanza mashindano hayo kuandaliwa na nchi tatu.

Mchakato wa kufuzu unaendelea, huku mechi za mwisho za kuwania nafasi ya kushiriki fainali hizo zikipangwa kufanyika Machi 2027.

Hata hivyo, kuandaliwa kwa AFCON 2028 mwaka mmoja tu baada ya mashindano ya 2027 kunaweza kuibua changamoto nyingine kuhusu ratiba ya kufuzu, mzigo wa mechi kwa wachezaji na maandalizi ya timu za taifa.

Kwa sasa, maswali makubwa yanayoikabili CAF ni kwa nini AFCON haitafanyika mwaka 2029, namna itakavyoshughulikia maombi ya awali ya uenyeji na hatma ya Ligi ya Mataifa ya Afrika.

Changamoto inayofuata kwa CAF ni kuweka wazi mpango wa mpito utakaoifanya ratiba hiyo iwe na mfumo endelevu na unaoeleweka kwa vyama wanachama, timu za taifa na nchi zinazotaka kuandaa mashindano hayo.