Tuchel amchana Rashford, mwenyewe afichua kilichomuangamiza
Muktasari:
- Rashford kwa sasa yuko kwa mkopo Barcelona, akijaribu kufufua uwezo wake baada ya kupoteza nafasi kwenye kikosi cha Manchester United chini ya kocha Ruben Amorim, ambaye hakuridhishwa na kiwango chake kwenye uwanja wa mazoezi.
Kocha wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel amemuonya Marcus Rashford kwa kumwambia ni lazima aonyeshe uwezo wake au akubali hatari ya kumaliza uwezo wake kisoka katika kipindi hiki ambacho kila mtu anamtazama kwa jicho la tatu.
Rashford kwa sasa yuko kwa mkopo Barcelona, akijaribu kufufua uwezo wake baada ya kupoteza nafasi kwenye kikosi cha Manchester United chini ya kocha Ruben Amorim, ambaye hakuridhishwa na kiwango chake kwenye uwanja wa mazoezi.
Ingawa hajachezea timu ya taifa ya England tangu Machi 2024, Rashford alijumuishwa katika kikosi cha kwanza cha Tuchel kilichotangazwa hivi karibuni, na alicheza dakika chache katika mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Wales wiki iliyopita.
Tuchel raia wa Ujerumani, sasa amemtaka Rashford kupambana na kuonyesha uwezo kama zamani, na endapo atashindwa kufanya hivyo kuna kila dalili akajipoteza katika ramani ya soka la ushindani.
“Sio swala la kipaji, ni kama anaweza kuthibitisha uwezo wake katika klabu na timu ya taifa,” Tuchel amesema akiwa mjini Riga kabla ya mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Latvia.
“Vinginevyo, ataishia kujuta miaka 10 ijayo kwa kile ambacho kingeweza kuwa kwa uwezo wake wa kupambana uwanjani.
“Nadhani kila mmoja wetu ana ufahamu uwezo wa Rashford, ana kiwango cha juu sana kisoka. Mimi ninaamini ana uwezo mkubwa sana, na changamoto anazozipitia ni za kawaida kwenye mchezo wa soka.
Tuchel ameendelea kwa kusisitiza kuwa Rashford hana mipaka ya kile anachoweza kukifanikisha, lakini takwimu zake hazilingani na kiwango chake kwa sasa.
“Anaweza kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani kwa sababu ubora alionao mazoezini, uwezo wa kumalizia kwa miguu yote miwili na kwa kichwa, ana kasi ya ajabu, ni mwepesi, ni mzuri hewani, kwa hiyo anatakiwa kupewa moyo na kuongoza ili arudi kwenye kiwango chake."
Akizungumza na kituo cha ITV Football kabla ya mchezo dhidi ya Latvia, Rashford ametaja mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha Manchester United kama chanzo cha changamoto anazozipitia kwa sasa.
“Watu wanapozungumzia juu ya uwezo wangu, wanatakiwa kutambua nilikuwa wapi na kwa sasa nipo wapi, nimepitia vipindi tofauti sana.
“Pale Manchester United tulikuwa na mabadiliko mengi sana ya makocha, na hadi sasa suala hilo linaendelea, ninaamini hili limechangia sana kwenye changamoto inazozipitia kwa sasa, lakini ninapaswa kupambana zaidi, ninaamini hakuna kinachoshindikana, nitaweza kufikia pale ambapo kila shabiki wangu anataka nifike,” amesema Rashford.