Tchouameni aingia anga za Man United
Muktasari:
- Staa huyu ambaye pia anawindwa na Liverpool anahisishwa sana kuondoka Madrid kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Madrid.
MANCHESTER United inataka kufanya kila linalowezekana kuhakikisha inamsajili kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Aurelien Tchouameni, 26.
Staa huyu ambaye pia anawindwa na Liverpool anahisishwa sana kuondoka Madrid kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Madrid.
Man United inataka kusajili viungo wawili msimu huu na Tchouameni anaonekana kuwa kipaumbele chao wakiamini anaweza kuziba pengo la Casemiro ambaye atondoka mwisho wa msimu.
Mkataba wa sasa wa kiungo huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 44 za michuano yote, amefunga mabao mawili na kutoa asisti mbili.
Timu nyingi zinavutiwa na fundi huyu kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya mbili kwa ufanisi.
Anthony Gordon
NEWCASTLE imeweka wazi kuwa ipo tayari kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa England, Anthony Gordon, 25, kwenda Bayern Munich katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa klabu hiyo itawasilisha ofa itakayoanzia Pauni 75 milioni.
Gordon ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Newcastle na timu nyingi zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili lakini changamoto kubwa inaonekana ni bei yake.
Yan Diomande
WINGA wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yan Diomande, 19, kwa sasa yupo katika rada za Liverpool inayohitaji kumsajili akawe mbadala wa winga wao wa kimataifa wa Misri, Mohamed Salah mwenye umri wa miaka 33.
Diomande ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 yeye mwenyewe ameonyesha kuwa na uhitaji wa kuondoka na kutua Anfield.
Cristian Romero
BEKI wa Tottenham na timu ya taifa ya Argentina, Cristian Romero mwenye umri wa miaka 27, anataka kusubiri hadi mwisho kabla ya kufanya uamuzi ikiwa ataendelea kusalia katika kikosi hicho au ataondoka kwenda Atletico Madrid inayohitaji sana huduma yake.
Inaelezwa Romero anataka kusubiri kuona ikiwa Spurs itaendelea kusalia katika Ligi Kuu England au laa.
Alessandro Bastoni
MANCHESTER City na Liverpool huenda zikaangukia pua katika harakati zao za kuiwania saini ya beki wa Inter Milan, Alessandro Bastoni, dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Boston, 27, anadaiwa kuichagua Barcelona kama ndiyo timu pekee ambayo anataka ajiunge nayo ikiwa ataondoka Inter mwisho wa msimu huu.
Kwa sasa Barca inafanya majadiliano na wakala wake ili kuweza kufikia makubaliano bonafsi yanayohusisha mshahara pamoja na bonasi.
Enzo le Fee
LIVERPOOL ni miongoni mwa timu zilizoonyesha nia ya kumsajili kiungo wa Sunderland, Enzo le Fee mwenye umri wa miaka 26.
Le Fee ameonyesha kiwango bora sana msimu huu akiwa na Sunderland ambayo licha yakupanda daraja imeonekana kusumbua sana katika Ligi Kuu England.
Inaelezwa Sunderland haina mpango wa kumuuza staa huyu lakini suala hilo linaweza kutoka ikiwa timu inayomhitaji itaweka kiasi kikubwa cha pesa mezani.
Karim Adeyemi
WAWAKILISHI wa Chelsea wamekutana na wakala wa winga wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Karim Adeyemi mwenye umri wa miaka 24.
Vigogo hao wa Chelsea wamekutana na wakala huyo ili kufikia makubaliano binafsi kabla hawajawasilisha ofa kwenda Dortmund kwa ajili ya kuvunja mkataba wake. Tangu kuanza kwa msimu huu, Adeyemi amecheza mechi 37 za michuano yote.
John Stones
BEKI wa kati wa Manchester City na timu ya taifa ya England, John Stones, 31, anatarajiwa kuondoka katika viunga vya Etihad katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi akiwa mchezaji huru.
Stones ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hakuna mazungumzo ya kuurefusha yanayoendelea kati ya wawakilishi wake na mabosi wa Man City.