Tajiri Leon Cooperman anunua hisa Man United
Muktasari:
- Mzee huyo mwenye umri wa miaka 82 alinunua hisa 900,000 mwaka 2023, muda mfupi kabla ya mmiliki wa sasa Sir Jim Ratcliffe kukamilisha ununuzi wake na kupewa haki ya kuongoza masuala ya michezo.
MANCHESTER, ENGLAND: MFANYABIASHARA wa Marekani Leon Cooperman amenunua hisa zaidi za Manchester United, lakini hana mpango wa kuchukua umiliki kamili wa klabu hiyo.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 82 alinunua hisa 900,000 mwaka 2023, muda mfupi kabla ya mmiliki wa sasa Sir Jim Ratcliffe kukamilisha ununuzi wake na kupewa haki ya kuongoza masuala ya michezo.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Independent,Cooperman kwa sasa anamiliki asilimia 5.2 ya hisa za Manchester United baada ya kununua hisa nyingine milioni mbili.
Thamani ya hisa za Cooperman sasa inakadiriwa kuwa zaidi ya Dola 50 milioni (sawa na Pauni 36.9 milioni 36.9), baada ya kununua hisa hizo kutoka kampuni ya uwekezaji ya England Lindsell Train.
Cooperman ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Omega Advisors, haonekani kuwa na mpango wa kuchukua rasmi umiliki wa Man United.
Inaripotiwa hisa zake ziko kwenye kundi la Class A, ambazo zinatoa kura moja ya maamuzi kwa kila hisa.
Hisa za Class B zina nguvu kubwa zaidi za kura na kila hisa ina kura 10. Hisa za Class A zinamilikiwa kwa wingi na familia ya Glazer pamoja na Ratcliffe.
Mmiliki wa INEOS, Jim Ratcliffe, alikamilisha makubaliano ya kununua asilimia 25 ya hisa za Man United Februari 2024, lakini umiliki huo uliongezeka hadi asilimia 27.7 baada ya kuwekeza zaidi ya Pauni 300 milioni, ambazo zimetumika kuboresha miundombinu ya klabu.
Hivi karibuni Man United ilitangaza mipango ya kujenga uwanja mpya wa kisasa katika eneo la Old Trafford, huku kituo cha mazoezi cha Carrington pia kikikarabatiwa. Hata hivyo, Ratcliffe amekumbana na ukosoaji mkali kutokana na kupunguza wafanyakazi na kubana matumizi katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa sasa, Man United ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, huku Michael Carrick akifanya kazi nzuri sana Old Trafford tangu achukue nafasi ya Ruben Amorim kama kocha wa muda.