Super League yarudi kwa sura mpya Ulaya
Muktasari:
- Zaidi ya miaka mitatu baada ya wazo la awali la michuano hiyo kupigwa na kufutwa ndani ya saa 48 kutokana na maandamano ya mashabiki wa klabu mbalimbali za soka huko Ulaya, kampuni ya A22 imekuja na mtindo mpya wa kuanzisha michuano hiyo ya soka huku ikijibu matatizo mengi ya ule mpango wa awali.
MADRID, HISPANIA: ILE michuano ya soka ya Super League iliyopigwa vita kali huko Ulaya na kufa kabla ya kuanza kufanyika imerudi upya na katika mtindo mpya, imefichuka.
Zaidi ya miaka mitatu baada ya wazo la awali la michuano hiyo kupigwa na kufutwa ndani ya saa 48 kutokana na maandamano ya mashabiki wa klabu mbalimbali za soka huko Ulaya, kampuni ya A22 imekuja na mtindo mpya wa kuanzisha michuano hiyo ya soka huku ikijibu matatizo mengi ya ule mpango wa awali.
Katika mtindo huo mpya, michuano hiyo sasa itaitwa ‘The Unify League’, na jumla ya timu 96 za Ulaya zitashiriki kila mwaka. Nafasi zote za ushiriki zinatokana na viwango vya ligi za ndani vya msimu uliopita kama ilivyo kwa sasa zinavyopatikana tiketi za kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League na Conference League.
Muundo wake utafanyika kwa mtindo wa ligi nne: Star League, Gold League, Blue League na Union League. Ligi mbili za juu, Star na Gold, kila moja itakuwa na timu 16, zinazogawanywa kwenye makundi mawili ya timu nane. Makundi hayo ya timu nane zitachuana zenyewe kwa zenyewe nyumbani na ugenini, ikiwa ni jumla ya mechi 14 kwa kila klabu kwa msimu. Ligi mbili za chini, Blue na Union, zitakuwa na timu 32 kila moja, zikigawanywa kwenye makundi manne ya timu nane. Nazo zitacheza zenyewe kwa zenyewe kwenye makundi kwa mechi za nyumbani na ugenini.
Kwenye Star na Gold, timu nne za juu kwenye kila kundi zitacheza mechi mbili za nyumbani na ugenini kuwania kuingia robo fainali. Kwenye ligi ya Blue na Union, timu mbili za juu zitachuana zenyewe kwenye makundi yao ili kutinga robo fainali. Kwenye hatua za juu za michuano hiyo, mechi zitapigwa kwenye viwanja huru. Ligi Kuu England ina uhakika wa nafasi tatu kwenye Star League, timu mbili kwenye Gold League. Timu nyingine tano kwenye ligi mbili za chini.
Tofauti na ilivyokuwa kwenye mpango wa Super League, kuhusisha timu 12 vigogo na jambo hilo liliibua maandamano makubwa, safari hii uwanja umeachwa wazi na timu itakayofanya vizuri kwenye ligi ya ndani itapata tiketi ya kucheza michuano hiyo tofauti na mwanzoni ilivyokuwa inalenga timu fulani.
Kwa mpango huo wa A22 ni timu zitacheza mechi 14 kwa mtindo wa ligi kati ya Septemba na Aprili. Kinachoelezwa ni mpango uliopo juu ya ligi michuano hiyo itaanza, imedaiwa ni Septemba 2026.
Wakati promota wa ligi hiyo, A22 bado haijaweka wazi zawadi ya pesa, rais wa Real Madrid, Florentino Perez - ambaye anadaiwa kuwa mstari wa mbele kwenye mchakato huo, ametoa ahadi ya mkwanja wa Pauni 330 milioni ikiwa ni mgawo kwa timu ndogo na nchi zao, huku zawadi ya jumla ikitarajia kuvuka Pauni 2 bilioni inayotolewa kwa sasa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Pauni 700 milioni kwenye Europa na Conference Leagues.
Pendekezo hilo la A22 limewasilishwa kwenye mamlaka ikiwamo Shirikisho la soka la Ulaya (Uefa) na Shirikisho la kimataifa la vyama vya soka (Fifa) kwa ajili ya kutoa kibali na kuingizwa kwenye kalenda ya mwaka ya michuano.