SIO POA... Hadithi, vifo, rekodi vyatawala PSG ikibeba ndoo

Muktasari:
- PSG ambayo ilikuwa ni fainali yao ya pili kucheza katika michuano hiyo katika historia yao, imejiwekea rekodi kibao baada ya kushinda.
MUNICH, UJERUMANI: WIKIENDI iliyopita lilifungwa rasmi pazia la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo PSG ilitwaa taji hilo baada ya kuichapa Inter Milan kipigo kitakatifu cha mabao 5-0.
PSG ambayo ilikuwa ni fainali yao ya pili kucheza katika michuano hiyo katika historia yao, imejiwekea rekodi kibao baada ya kushinda.
Mbali ya rekodi ilizojiwekea, pia ushindi wao umezua hadithi, rekodi na vifo vilivyosababishwa na vurugu za mashabiki baada ya wao kubeba taji hilo, hapa tumekusogezea mzigo wote.

HADITHI
Hadithi ya kwanza ni ile ya kocha wa PSG. Ubingwa huu ameuelekeza kama heshima kwa bintiye mdogo, Xana ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka tisa, Agosti 29, 2019, baada ya kupambana kwa miezi mitano na saratani ya mifupa (osteosarcoma).
Luis Enrique alijitoa kumpambania binti yake kipindi hicho kiasi alifikia kujiuzulu nafasi yake ya kocha wa timu ya taifa ya Hispania Juni 2019 ili kuwa karibu na familia yake katika kipindi hicho kigumu.
Baada ya kifo cha Xana, Luis Enrique alijitahidi na kurejea katika soka. Wikiendi iliyopita katika mchezo wa fainali alionekana kuwa na picha ya binti yake kwenye fulana ikiwa ni ishara ya kumkumbuka.
Pia mashabiki walikuwa wameingia uwanjani na vitambaa vikubwa vilivyomwonyesha mtoto huyo akiwa na jezi ya PSG ambayo nyuma yake iliandikwa jina lake ‘Xana’.
Mbali ya stori ya kocha. Katika safu ya ulinzi ya PSG kwenye mchezo huo wa fainali, kulikuwa na beki mdogo Willian Pacho ambaye alikuwa akicheza sambamba na mkongwe Marquinhos.
Baada ya mechi, alionekana kuwa katika huzuni na sio furaha sana na moja kati ya vitu alivyosema ilikuwa ni kumkumbuka mama yake.
Pacho ambaye amezaliwa katika famili ya kimaskini huko Ecuador, anaeleza kwamba mama yake ambaye ndio alikuwa msaada mkubwa kwake alimlea kwa tabu na bahati mbaya hajaonja ladha ya mafanikio yake kwani alifariki muda siku chache tu baada yeye kucheza mechi yake ya kwanza kama mchezaji wa kulipwa mwaka 2019.
“Mama yangu alikuwa msaada wangu mkubwa. Alinifundisha kuwa na subira, heshima, na kujitolea. Alikuwa nguzo ya maisha yangu, na ninamshukuru kwa kila kitu.”
Mbali ya Pacho, mmoja kati ya wachezaji walioonekana kumwaga machozi baada ya fainali hiyo kumalizika alikuwa ni beki Marquinhos ambaye amekuwapo katika kikosi hicho kwa zaidi ya miaka 14 sasa.
Beki huyu wa kati ambaye pia ni kapteni wa timu amepitia katika panda shuka nyingi na taji hili ilikuwa ni ndoto yao ya muda mrefu hivyo kuchukua ilimfanya kuwa na hisia ya tofauti.
Marquinhos alikuwapo wakati PSG ikiwa na mastaa kama Neymar, Mbappe na Lionel Messi lakini ikashindwa kubeba taji hili kwa wakati huo.

VURUGU NA VIFO
Mashabiki wa PSG waliokuwa wakisherehekea kwa furaha baada ya ushindi wao, walijikuta wakipigwa mabomu ya machozi baada ya mapigano ya vurugu kuzuka jijini Paris na kusababisha karibu watu 200 kujeruhiwa huku wawili wakipoteza maisha.
Mbali ya majeruhi pia idadi kubwa ya watu karibia 559 wamekamatwa baada ya polisi wa kupambana na ghasia kujaribu kuwatawanya mashabiki waliokuwa na furaha wakisherehekea ushindi wao wa kwanza wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Maelfu ya mashabiki walikusanyika kote jijini Paris usiku wa Jumamosi kutazama mechi hiyo, huku wengi wakijazana kwenye Uwanja wa Parc des Princes na wengine wengi wakifuatilia mechi hiyo kote Ufaransa.
Hata hivyo, sherehe hizo za kitaifa ziligeuka kuwa za majonzi baada ya kijana wa miaka 17 kuchomwa kisu kifuani hadi kufa huko Landes, karibu na Bordeaux, na mwanamke wa miaka 20 kufariki baada ya kugongwa na gari lililokuwa limebeba mashabiki jijini Paris.

Polisi wa eneo hilo walisema kijana huyo “alikuwa sehemu ya umati uliokuwa ukisherehekea ushindi wa PSG katika eneo rasmi la mashabiki, na alifariki dunia kutokana na majeraha yake baada ya kufikishwa hospitalini.”
Wakati huohuo, huko Grenoble, karibu na Lyon, watu wanne walijeruhiwa vibaya baada ya gari kuwagonga wakiwa katika sherehe za ushindi wa PSG.
Mwanamke mmoja aliwahishwa hospitalini baada ya gari lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kubwa kumgonga.
Video za kusikitisha mtandaoni zilionyesha jinsi Paris ilivyogeuka kuwa eneo la vurugu wakati wa fainali hiyo ilipomalizika na wakati inaendelea.
Moto pia ulizuka kote katika Jiji hilo hali iliyosababisha kuwepo kwa operesheni kubwa za usalama.
Video nyingine zilionyesha baiskeli na magodoro yakichomwa moto karibu na uwanja wa mpira huku moshi mzito mweusi ukifunika anga ya usiku.
Inaelezwa kuwa watu 559 wamekamatwa kutokana na vurugu hizo, huku 192 wakiripotiwa kujeruhiwa.

Wasiwasi kuhusu usalama katika mji mkuu wa Ufaransa uliongezeka zaidi kadri fainali ilivyokuwa ikikaribia na kwa sababu hiyo polisi walianza kujihami mapema.
Jiji la Paris lilituma maofisa wa polisi 5,400 kufanya doria maeneo mbalimbali ya jiji hilo kwa ajili ya mechi ya mechi hiyo.
Mkuu wa polisi jijini humo, Laurent Nunez alisema licha ya mechi hiyo kuchezwa mjini Munich, matokeo yake yalitarajiwa kusababisha sherehe ambazo zingezaa vurugu katika jiji la Paris.
Polisi waliamini kungekuwa na vurugu kama zile zilizozuka mitaani saa chache baada ya mechi ya nusu fainali kati ya PSG na Arsenal.
Kukabiliana na hilo, vikosi vya polisi vilitumwa kwenda kuongeza nguvu huko Paris ambako askari wengi walikuwa wakilinda maeneo mbalimbali ya mji, hasa katika barabara ya Champs-Elysees, ambako kawaida mashabiki wana tabia ya kujaa ikiwa PSG imepata matokeo mazuri.
Polisi pia walifunga barabara karibu na eneo hilo, na waliongeza wingi wa kamera na kufuatilia matukio yaliyoendelea eneo hilo kwa umakini wa hali ya juu.
Usalama pia uliimarishwa kwenye Uwanja wa Parc des Princes, ambao ni uwanja wa nyumbani wa PSG ulioko pembezoni mwa jiji upande wa kusini-magharibi.
Lakini hiyo haikusaidia kwani baadhi ya mashabiki walionekana wakiwa kiwanjani humo wakichana nyavu za uwanja vipande vipande na kugawana, ikiwa ni shemu yao ya kushangilia ushindi.

REKODI
1. Taji la kwanza
PSG ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia tangu ianzishwe mwaka 1970. Hii ilikuwa ndoto ya muda mrefu kwa klabu hiyo inayomilikiwa na Waarabu, ambao wamewekeza mamilioni ya euro katika miaka ya hivi karibuni.
2. Ushindi mkubwa zaidi fainali
Mabao 5-0, ambayo PSG imepata, ni ushindi mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika fainali ya michuano hii.
Kabla ya hapo, ushindi mkubwa zaidi ulikuwa ni mabao 4-0 iliyopata AC Milan mbele ya Barcelona mwaka 1994 katika fainali iliyopigwa Olympic Stadium, Athens, Ugiriki.
3. Doue aingia kwenye historia
Desire Doue, mwenye umri wa miaka 19 na siku 362, alifunga mabao mawili na kutoa pasi ya bao katika fainali hiyo. Amekuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufanya hivyo kwenye fainali ya michuano hiyo.
4. PSG mataji matatu (TREBLE)
Mbali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, msimu huu PSG imetwaa mataji mengine mawili ambayo ni Ligue 1 (Ufaransa) na Coupe de France. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa klabu yoyote ya Ufaransa kufanya hivyo.
5. Luis Enrique kwenye historia
Kocha Luis Enrique alifanikiwa kushinda mataji matatu makubwa akiwa na timu ya bara la Ulaya kwa mara ya pili katika maisha yake ya ukocha, mara ya kwanza alifanya hivyo akiwa na Barcelona mwaka 2015. Kocha mwingine pekee aliyewahi kufanya hivi ni Pep Guardiola tu.
6. PSG yavuka mabao 500 katika Ulaya
Mbali ya taji, PSG pia imefanikisha kuvuka mabao 500 ya jumla katika historia yake ya kushiriki mashindano ya UEFA.