Sheria ya pigo la penalti yaboreshwa

Muktasari:
- Kwa mujibu wa muongozo wa FIFA, IFAB ndio chombo chenye mamlaka ya kufanya marekebisho ya sheria 17 za mpira wa miguu ambazo zinatumika duniani kote.
Bodi ya Vyama vya Mpira wa Miguu Duniani (IFAB) imefanya maboresho ya sheria mbili za soka ambazo ni sheria namba 10 inayohusu kuamua matokeo ya mchezo na sheria namba 14 inayohusu pigo la penalti.

Mabadiliko hayo yanahusu namna ya upigaji penalti na matokeo yake pale inapotokea mpigaji wa penalti akaugusa mipira kwa miguu yake miwili jambo ambalo kwa msimu uliopita na mingine ya nyuma lilikuwa ni kosa linalopelekea uamuzi wa adhabu ya pigo lisilo la moja kwa moja kwa timu iliyopigiwa penalti na ile iliyopiga kuhesabiwa imekosa.
Hata hivyo katika mabadiliko ambayo IFAB imeyafanya na yamepitishwa na Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa sasa uamuzi wa timu inayopiga penalti kuhesabiwa imekosa utategemeana na utafsiri wa refa kama mchezaji anayepiga penalti amefanya kwa makusudi au bahati mbaya.
"Mpigaji penalti akipiga mpira kwa makusudi kwa miguu yote miwili au kwa makusudi akaugusu mpira kabla haujagusa mchezaji mwingine, pigo lisilo la moja kwa moja litazawadiwa (isipokuwa mwamuzi atachezesha kwa faida pale inaponufaisha timu inayojilinda) au kwenye tukio la penalti, pigo litahesabika kuwa limekoswa," inafafanua sehemu ya barua ya IFAB iliyoandikwa kwenda kwa vyama na mashirikisho ya soka kufafanua mabadiliko hayo.
Lakini mabadiliko hayo yamekuwa na unafuu kwa mpigaji iwapo ataugusa mpira kwa bahati mbaya kwa miguu yake yote miwili.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, iwapo refa atajiridhisha kuwa mpigaji ameugusa mpira kwa bahati mbaya, refa ataamuru pigo hilo lirudiwe iwapo amefunga mkwaju huo.
Iwapo mpigaji atakuwa amekosa refa ataamuru pigo lisilo la moja kwa mija kwa timu ambayo inakuwa inazuia.
Hakuna shaka mabadiliko hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na tukio lililotokea Machi 12, 2025 katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Real Madrid na Atletico Madrid.
Katika mchezo huo Real Madrid ilipata ushindi wa mikwaju ya penalti 4-2, mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez licha ya kukwamisha wavuni mkwaju wake wa penalti, haukuhesabika kuwa ni bao kwa vile ilionekana ameugusa mpira na miguu miwili wakati alipokuwa akipiga penalti hiyo.
Tukio hilo ambalo liliamriwa na refa Syzmon Marciniak kutoka Poland, lilioneka kuzua mjadala huku Atletico Madrid ikiandika barua kwenda kwa Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) ikihitaji ufafanuzi kwa vile ilionekana Alvarez hakufanya kwa kukusudia.

Siku moja baadaye, UEFA ilitoa taarifa ya kukutana na IFAB kujadili kuhusu tukio hilo na kuona uwezekano wa kufanyia mabadiliko sheria ya pigo la penalti
"Atlético de Madrid imeiuliza UEFA juu ya tukio hilo, ambalo lilisababisha kukataliwa kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Julian Alvarez mwishoni mwa mechi ya jana ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
"Ingawa ni kwa udogo, mchezaji aligusa mpira kwa mguu wake uliosimama kabla ya kuupiga, kama inavyoonyeshwa kwenye kipande cha video kilichoambatanishwa. Chini ya sheria ya sasa (Sheria za Mchezo, Sheria 14.1), VAR ililazimika kumwita mwamuzi kuashiria kwamba bao hilo limekataliwa..
"UEFA itaingia kwenye majadiliano na FIFA na IFAB ili kubaini iwapo sheria hiyo inafaa kuangaliwa katika hali ambapo kuguswa mara mbili ni dhahiri bila kukusudia," ilifafanua taarifa ya UEFA.