Sababu hii itamuondoka Isak Newcastle United
Muktasari:
- Saini ya supastaa huyo inawindwa na timu mbalimbali kubwa barani humo ikiwa ni pamoja na Barcelona, Liverpool, Arsenal na Chelsea.
NEWCASTLE United huenda ikawa tayari kumuuza straika wake raia wa Sweden, Alexander Isak katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi Ulaya kwa Euro 100 milioni ikiwa itashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Saini ya supastaa huyo inawindwa na timu mbalimbali kubwa barani humo ikiwa ni pamoja na Barcelona, Liverpool, Arsenal na Chelsea.
Inaelezwa Isak ambaye tangu kuanza kwa msimu huu amefunga mabao 17 katika mechi 23 za Ligi Kuu England, anataka kupiga hatua zaidi katika maisha yake ya soka ikiwa ni pamoja na kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu ujao. Ikiwa Newcastle United itashindwa kufuzu mashindano hayo, Isak ataomba ama kuuzwa kwenda katika timu inayoshiriki michuano hiyo na ikishindikana hata kutolewa kwa mkopo katika timu inayokipiga Ulaya. Kwa sasa mchezaji huyo wa zamani wa Real Sociedad, Willem II, Borussia Dortmundna AIK yupo kwenye fomu huko England.
Wilfred Ndidi
ATLETICO Madrid imeonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo wa Leicester City na Nigeria, Wilfred Ndidi, 28, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mchezaji huyo ambaye aliwahi kucheza na Mbwana Samatta wakiwa KRC Genk ya Ubelgiji, awali aliripotiwa kuhitajika katika kikosi cha Atletico Madrid tangu mwaka jana.
Jarrad Branthwaite
EVERTON inataka kumsajili beki wa kati wa Burnley na Ufaransa, Maxime Esteve kama mbadala wa beki raia wa England, Jarrad Branthwaite, 22, ambaye kuna uwezekano mkubwa akaondoka mwisho wa msimu huu. Branthwaite amekuwa akihusishwa na vigogo wengi wa England, hususan Manchester United ambapo mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2027.
Nicolas Kuhn
NEWCASTLE United imeingia katika vita dhidi ya Brentford na Brighton kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji wa Celtic na Ujerumani, Nicolas Kuhn, 25. Kuhn ni miongoni mwa mastraika walioonyesha viwango bora tangu kuanza kwa msimu huu ambapo amecheza mechi 35 za michuano yote na kufunga mabao 17. Mkataba wake unamalizika 2029.
Rayan Cherki
MABOSI wa Everton wanataka kuanzisha tena mazungumzo na Olympique Lyon kwa ajili ya kuipata saini ya winga wa timu hiyo na Ufaransa, Rayan Cherki, 21, baada ya kufeli kumpata dirisha lililopita licha ya kuwasilisha ofa. Cherki ambaye msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote na kufunga mabao sita, mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2026.
Antonio Cordero
NEWCASTLE United imefanya mazungumzo na wawakilishi wa winga wa Malaga, Antonio Cordero, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Vigogo wa Newcastle United wanataka kumsajili staa huyo mwenye umri wa miaka 18, kwa usajili huru. Akiwa na Malaga, Cordero amecheza mechi 26 za michuano yote na kufunga mabao manne.
Marc Casado
CHELSEA imefikia pazuri katika mazungumzo na wawakilishi wa kiungo wa Barcelona, Marc Casado, 21, ambaye amekuwa mhimili kwenye safu ya kiungo ya Barcelona. Casado aliyepandishwa kutoka timu ya vijana ya Barca Julai mwaka jana, msimu huu amecheza mechi 30 za michuano yote. Mkataba wake unaisha 2028.
Jules Kounde
BARCELONA inataka kumsainisha mkataba mpya beki raia wa Ufaransa, Jules Kounde ambao utamwezesha kudumu hadi 2030 ikiwa ni baada ya kuona idadi kubwa ya timu zinahitaji saini yake. Katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Kounde, 26, alikuwa akihusishwa na Chelsea iliyokuwa tayari kutoa Pauni 83 milioni. Mkataba unaisha 2027.