Real Madrid yajisogeza kwa Wirtz

Muktasari:
- Awali, ilionekana kwamba Wirtz angetua England ambako alianza kuwindwa na Manchester City ambayo ilijitoa kabla ya Liverpool kuingia katika vita ya kumuwania staa huyo hivi karibuni.
REAL Madrid inapambana kutaka kumsajili winga wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Ujerumani, Florian Wirtz, 22, kwa kumtumia kocha wake wa zamani Xabi Alonso ambaye ametangazwa kuwa kocha mpya wa miamba hiyo ya Hispania baada ya kuondoka kwa Carlo Ancelotti.
Awali, ilionekana kwamba Wirtz angetua England ambako alianza kuwindwa na Manchester City ambayo ilijitoa kabla ya Liverpool kuingia katika vita ya kumuwania staa huyo hivi karibuni.
Mkataba wa sasa wa Wirtz unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliomalizika alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 16.
Alonso na Wirtz waliiwezesha Leverkusen kutwaa ubingwa wao wa kwanza kabisa wa Bundesliga msimu uliopita, na kuna hisia kwamba ujio wa Alonso huko Madrid bado unaweza kuwa na ushawishi katika uamuzi wa Wirtz kuhusu uhamisho wake.
Kwa mujibu wa gazeti la AS, ingawa Bayern Munich wamejiondoa katika mbio za kumsajili Wirtz huku Liverpool wakisonga mbele, Real Madrid bado haijakata tamaa ya kumnasa kiungo huyo.
Inaaminika kuwa Wirtz tayari amefikia makubaliano ya kujiunga na Liverpool msimu ujao na ameiambia Leverkusen kuwa Merseyside ndiyo anayoitaka kama kituo chake kipya cha soka.
Kwa sasa pendekezo la kwanza la bei la Leverkusen ili kumuuza ni zaidi ya Euro 100 milioni.
Caoimhin Kelleher
BRENTFORD imewasiliana na wawakilishi wa Liverpool kuulizia uwezekano wa kuipata saini ya kipa wa majogoo hao na Jamhuri ya Ireland, Caoimhin Kelleher katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo ripoti zinaeleza anaweza kuuzwa kwa Pauni 20 milioni.
Kelleher anataka kuondoka Liverpool katika dirisha lijalo ili kujiunga na timu itakayompa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Cody Gakpo
BAYERN Munich imeonyesha shauku ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uholanzi, Cody Gakpo, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Inaelezwa Bayern ni miongoni mwa timu ambazo Gakpo yupo tayari kujiunga nazo lakini dili hili linaonekana kuwa na ugumu kwani Liverpool haiko tayari kumwachia.
Milos Kerkez
BEKI wa Bournemouth, Milos Kerkez amekubali kujiunga na Liverpool katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na kinachosubiriwa ni Majogoo hao na Bournemouth kufikia makubaliano katika masuala ya ada ya uhamisho.
Milos ambaye mkataba wake na Bournemouth unamalizika mwaka 2028, msimu uliomalizika alicheza mechi 41 za michuano yote.
Marcus Rashford
MAZUNGUMZO baina ya wakala wa mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford na Mkurugenzi wa Michezo Barcelona, Deco, yanadaiwa kwenda vizuri na kuna asilimia kadhaa za staa hiyo wa kimataifa wa England kutua Nou Camp katika dirisha lijalo.
Vyombo vya habari mbalimbali vya Hispania, juzi viliripoti kuwa wakala huyo ametua Hispania kwa ajili ya mazungumzo.
Leroy Sane
ARSENAL imeingia katika orodha ya timu zinazohitaji saini ya winga wa Bayern Munich, Ujerumani Leroy Sane mwenye umri wa miaka 29, ambaye mkataba wake na Bayern Munich unamalizika mwisho wa msimu huu.
Sane ambaye pia amepewa ofa ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Bayern, pia anawindwa na vigogo kama Barcelona na Tottenham.
Liam Delap
NEWCASTLE ni miongoni mwa timu zinazofanya harakati za kutaka kumsajili mshambuliaji wa Ipswich Town, Liam Delap, 22, ambaye pia amepata ofa kutoka Chelsea, Manchester United na Everton zinazomhitaji katika dirisha hili.
Delap anawindwa na timu nyingi kutokana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita akiwa na Luton ambapo amefunga mabao 12.
Benjamin Sesko
ARSENAL imeambiwa na RB Leipzig kuwa lazima ilipe Pauni 92.5 milioni ili kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Slovenia mwenye umri wa miaka 21, Benjamin Sesko, ambaye pia anawindwa Manchester United kuelekea dirisha lijalo.
Kwa msimu uliopita Sesko alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 21.