Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha wa Kenya afichua kudai mishahara, FIFA, CAF zapewa ombi

Muktasari:

  • Hali hiyo imeibua tena wasiwasi kuhusu usimamizi wa timu ya taifa ya Kenya kuelekea mchezo wake wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 dhidi ya Afrika Kusini, kesho Ijumaa, Novemba 13, 2026.

Nairobi, Kenya. Kocha wa Harambee Stars, Benni McCarthy, amefichua kuwa yeye pamoja na baadhi ya wasaidizi wake wa benchi la ufundi hawajalipwa mishahara yao.

Hali hiyo imeibua tena wasiwasi kuhusu usimamizi wa timu ya taifa ya Kenya kuelekea mchezo wake wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 dhidi ya Afrika Kusini, kesho Ijumaa, Novemba 13, 2026.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema kuwa suala hilo bado halijapatiwa ufumbuzi, licha ya wachezaji kulipwa fedha zao za posho zilizokuwa zimechelewa kufuatia mgogoro wa malipo uliovuruga maandalizi ya Kenya kwa michezo yake miwili ya kwanza ya kuwania kufuzu AFCON dhidi ya Eritrea na Guinea.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Sporty TV, McCarthy amefichua kuwa hakuna hata mmoja kati ya maofisa wa benchi lake la ufundi aliyelipwa, huku akiziomba kuwa vyombo vinavyosimamia soka duniani, ikiwemo Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), vinaweza kulazimika kuingilia kati iwapo suala hilo halitapatiwa ufumbuzi.

"Benchi la ufundi halijapokea chochote," alisema McCarthy.

Amesisitiza kuwa mamlaka husika zinapaswa kutekeleza wajibu wao wa kifedha na kuwalipa makocha, ingawa amedai kuwa hali hiyo haitaathiri dhamira yake ya kuitumikia timu ya taifa.

Kocha huyo wa zamani wa washambuliaji wa Manchester United amesema kipaumbele chake kinaendelea kuwa kuendeleza soka la Kenya na kuhakikisha anaiacha timu ya taifa katika hali nzuri zaidi kuliko alivyokuta alipojiunga nayo.

Suala hilo limeibuka wiki chache baada ya maandalizi ya Harambee Stars kwa ajili ya mechi za kufuzu AFCON 2027 kuvurugwa na mgogoro kuhusu kutolipwa kwa posho za wachezaji.

Kabla ya mchezo wao wa kwanza wa Kundi D dhidi ya Eritrea katika Uwanja wa Nyayo mwezi Septemba, wachezaji waliripotiwa kugoma kufanya mazoezi kutokana na kuchelewa kulipwa fedha zao.

McCarthy alifichua kuwa aliingilia kati binafsi ili kuwashawishi wachezaji kurejea mazoezini huku Kenya ikiwa imebakiwa na kipindi kimoja tu cha mazoezi kabla ya mchezo huo kufuatia mgogoro huo.

Alisema aliwashawishi wachezaji kurejea katika maandalizi siku moja kabla ya mchezo na baadaye kuwataka kutimiza wajibu wao kwa kuitumikia timu ya taifa.

Tatizo la kutokuwa na uhakika kuhusu malipo liliendelea kuikabili timu hiyo hata iliposafiri kwenda Guinea kwa mchezo wake wa pili wa kufuzu.

Hata hivyo, wachezaji wengi hatimaye walilipwa posho zao zilizokuwa zimechelewa baada ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) na serikali kushinikizwa kuchukua hatua.

Kwa sasa, Kenya inapaswa kuelekeza nguvu zake katika mchezo mgumu wa ugenini dhidi ya Afrika Kusini utakaochezwa katika Uwanja wa Orlando, jijini Johannesburg.

Harambee Stars ina pointi moja pekee katika michezo yake miwili ya mwanzo, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Eritrea jijini Nairobi na kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Guinea ugenini.

Mbali na changamoto za kifedha, McCarthy pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu mustakabali wake wa muda mrefu katika soka la kimataifa.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini aliwahi kueleza kuwa angependa kurejea katika ukocha wa ngazi ya klabu. Alifafanua kuwa anakosa mwingiliano wa kila siku na wachezaji pamoja na fursa ya kufanya kazi nao kwa karibu katika kuboresha uwezo na maendeleo yao.

Anaamini kuwa ukocha wa timu za taifa unamuwekea mipaka katika uwezo wake wa kuleta mabadiliko ya kudumu, kutokana na muda mfupi anaopata kufanya kazi na wachezaji wakati wa mapumziko ya kalenda ya mechi za kimataifa.