Pochettino na kibarua kigumu UEFA dhidi ya Sporting
Muktasari:
- Chini ya Hans Flick, Barcelona imeshinda mechi 10 kati ya 11 za Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu zinazotoka nje ya ligi tano kubwa za Ulaya, huku ikitoka sare mara moja. Katika mechi hizo imefunga mabao 45, ikiwamo mabao matatu au zaidi katika mechi 10 kati ya hizo 11. Kwa kuzingatia takwimu hizo, Barcelona ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo kwa asilimia 81.2.
MASAZIR, AZERBAIJAN: BAADA ya jana kupigwa mechi 10, Ligi ya Mabingwa Ulaya inaendelea leo kwa mechi nyingine kama hizo kuchezwa katika miji mbalimbali ambapo wababe wataonyeshana kazi viwanjani.
BARCA vs SABAH
Barcelona itakuwa Azerbaijan kuvaana na Sabah, ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambako timu hiyo iliyorejea vizuri baada ya kupoteza kwa mabao 4-2 dhidi ya PSG katika mchezo wa tatu, kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Aston Villa katika mchezo wa nne itakuwa mzigoni.
Chini ya Hans Flick, Barcelona imeshinda mechi 10 kati ya 11 za Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu zinazotoka nje ya ligi tano kubwa za Ulaya, huku ikitoka sare mara moja. Katika mechi hizo imefunga mabao 45, ikiwamo mabao matatu au zaidi katika mechi 10 kati ya hizo 11. Kwa kuzingatia takwimu hizo, Barcelona ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo kwa asilimia 81.2.
SLAVIA PRAGUE vs VILLARREAL
Mchezo mwingine ni kati ya Slavia Prague na Villarreal, utakaochezwa nchini Jamhuri ya Czech. Itakumbukwa kwamba Villarreal haijawahi kupoteza dhidi ya timu inayotoka Czech. Mchezo huo utakuwa wa 10 kwa timu hiyo kukutana na wapinzani kutoka nchini humo, ikiwa imeshinda mara sita na kutoka sare mara tatu. Ingawa Villarreal imeruhusu mabao 10 katika mechi mbili zilizopita za Ligi ya Mabingwa, inapewa nafasi ya kuondoka na pointi zote tatu kwa asilimia 43.
ATLETICO vs VIKING
Atletico Madrid itakuwa mwenyeji wa Viking katika mchezo ambao unatenganishwa na nafasi moja tu kwenye msimamo wa ligi, baada ya Viking ya Norway kuandika historia kwa ushindi wake wa kwanza kabisa katika Ligi ya Mabingwa kwenye mchezo wa nne.
Kwa upande wa Atletico Madrid imepoteza mechi tatu kati ya tano zilizopita za makundi ya mashindano hayo. Idadi hiyo ni mchezo mmoja tu pungufu ya mechi ilizopoteza katika michezo 21 iliyotangulia, ambayo ilishinda 14 na kutoka sare tatu. Licha ya kuyumba huko katika michezo ya hivi karibuni, Atletico Madrid inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda mchezo hu kwa asilimia 81.3.
CLUB BRUGGE vs LIVERPOOL
Liverpool imekutana na Club Brugge mara tatu katika historia, huku kukutana huko kukitokea katika fainali za mashindano ya Ulaya. Hata hivyo, safari hii hakutakuwa na uzito wa fainali wakati Liverpool itakapokuwa Ubelgiji. Liverpool itakuwa na hamu ya kurekebisha makosa baada ya kupoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Fenerbahce katika mchezo wa nne wa hatua ya ligi. Club Brugge imekuwa katika kiwango bora, ikiwa imeshinda mechi tatu zilizopita za Ligi ya Mabingwa. Hata hivyo, haijawahi kushinda mechi nne mfululizo katika historia ya Kombe la Ulaya.
Hata hivyo, mfululizo huo wa ushindi wa Club Brugge unaweza kukatika katika mchezo huu, kwani Liverpool inapewa nafasi ya ushindi ya asilimia 54.6.
INTER MILAN vs STUTTGART
Inter Milan imerejea katika kiwango bora baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo katika hatua ya ligi, kwa kushinda michezo miwili iliyofuata.
Sasa itakuwa mwenyeji wa Stuttgart katika mchezo wa tano wa hatua hiyo, ambapo haijapoteza katika mechi zake tatu zilizopita dhidi ya timu za Ujerumani katika Ligi ya Mabingwa, ikiwa imeshinda mara mbili na sare moja. Inter inaingia katika mchezo huo ikiwa na nafasi kubwa ya ushindi kwa asilimia 63.9, huku Stuttgart ikiwa na 17.9.
LILLE vs BAYERN MUNICH
Bayern Munich haijapoteza katika mechi nne za mwanzo za Ligi ya Mabingwa msimu huu. Hata hivyo, sare mbili dhidi ya Viking (3-3) na Arsenal (2-2) zimeifanya kujikuta katika nafasi ya 13 kwenye msimamo. Kwa upande wa Lille imepoteza mechi nne zilizopita za mashindano ya Ulaya ikiwa nyumbani. Kutokana na hali hiyo, kikosi cha Vincent Kompany kinaonekana kuwa na nafasi nzuri ya kupata ushindi mwingine katika mchezo huo kwa asilimia 56.8.
PSG vs Roma
Mabingwa watetezi PSG wameendelea kuonyesha ubora katika mashindano makubwa ya klabu Ulaya na Jumatano watakuwa wenyeji wa Roma katika mchezo utakaochezwa Parc des Princes. Kama ilivyoelezwa, PSG imekuwa ikifunga mabao mengi ikiwa imefunga angalau mabao manne katika kila mchezo wa Ligi ya Mabingwa msimu huu. PSG imekuwa timu ya kwanza kufunga mabao manne au zaidi katika mechi nne mfululizo za mashindano hayo. Ni katika misimu ya 2017-18 ilipofunga mabao 25 katika mechi sita, na 2025-26 mabao 21 katika mechi nane, ndipo ilipowahi kufunga mabao mengi zaidi katika hatua moja ya makundi. Roma inafanya vizuri katika Ligi Kuu Italia, lakini kucheza ugenini dhidi ya PSG ni moja ya changamoto kubwa katika soka la Ulaya. PSG ina nafasi ya ushindi ya asilimia 65.2, huku Roma ikipewa asilimia 16.6.
SHAKHTAR vs FENERBAHCE
Shakhtar Donetsk na Fenerbahce zinatarajiwa kukutana katika mashindano ya Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya muongo mmoja, ambapo Fenerbahce inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali baada ya kufunga mabao mawili ya dakika za mwisho na kuishinda Liverpool katika mchezo uliopita. Timu hiyo ya Uturuki inalenga kushinda mechi mbili mfululizo katika mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu Februari 2008. Hata hivyo Fenerbahce inapewa nafasi ya ushindi ya asilimia 36.7, ambayo ni ndogo kidogo ikilinganishwa na Shakhtar Donetsk, inayopewa asilimia 37.4.
SPORTING CP vs MAN UNITED
Paulo Fonseca ndiye kocha mpya wa Sporting; hakuna hata mmoja kati ya makocha watano wa mwisho wa kudumu kuinoa Sporting aliyeshinda mchezo wa kwanza katika mashindano hayo tangu Paulo Bento aliposhinda Septemba 2006. Na bila shaka, Mauricio Pochettino atakuwa kocha wa Man United katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na timu hiyo, ambapo alikabidhiwa kikosi kinashika nafasi ya 17, lakini hali ingekuwa mbaya zaidi kama kisingefanya mabadiliko makubwa katika mchezo wake dhidi ya Roma, siku ya nne ya mechi za hatua ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo kilitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.
Manchester United imefungwa mabao mawili au zaidi katika kila mmoja wa michezo yake mitatu iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (mabao manane kwa jumla). Awali, haikuwahi kufungwa mabao mawili au zaidi katika michezo minne mfululizo ya mashindano hayo.
Udhaifu huo wa safu ya ulinzi unaifanya Sporting kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda mchezo huo, ikiwa na asilimia 38.4. Kwa upande wake, Pochettino ana nafasi ya asilimia 36.4 ya kupata ushindi wake wa kwanza wa Ulaya akiwa na Mashetani Wekundu.