Pierluigi Collina: Mstaafu anayezidi kupiga pesa
Muktasari:
- Baada ya kazi yake ya kiwango cha juu kama mwamuzi wa Ligi Kuu na kwenye michuano mikubwa (ikiwemo Fainali ya Kombe la Dunia 2002), Collina ambaye ni raia wa Italia, ameendelea kuwa na nafasi za uongozi na ushauri katika mamlaka za soka duniani.
TUSCANY, ITALIA: PIERLUIGI Collina ni mojawapo ya nyuso zinazotambulika sana katika soka la kimataifa.
Baada ya kazi yake ya kiwango cha juu kama mwamuzi wa Ligi Kuu na kwenye michuano mikubwa (ikiwemo Fainali ya Kombe la Dunia 2002), Collina ambaye ni raia wa Italia, ameendelea kuwa na nafasi za uongozi na ushauri katika mamlaka za soka duniani.
Nafasi hizo za uongozi zinamfanya apate pesa na kuendelea kutajirika licha ya kustaafu. Hapa chini tumekuwekea utajiri wake wote na jinsi anavyopiga pesa kupitia nyadhifa hizo pamoja na biashara nyingine.
ANAPIGAJE PESA?
Kiujumla anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 5 milioni. Utajiri huu unatokana na mshahara aliokuwa analipwa wakati anafanya kazi ya uamuzi.
Mbali ya mshahara ambao anadaiwa kuwa alikuwa akipata wa Dola 50,000 kwa mwezi, Collina pia anapata mkwanja wa kutosha kutokana na kusaini kwake mikataba ya ubalozi na kampuni mbalimbali kama Opel/Vauxhall, MasterCard, Adidas na kampuni nyingine ambazo nyingi zilisaini naye mikataba wakati yupo katika kilele cha umaarufu wake.
Kwa sasa chanzo chake kikubwa cha mapato ni ajira na teuzi alizopata katika Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA,) pamoja na Shirikisho la Soka la Kimatifa (FIFA).
Anafanya kazi kama mshauri wa masuala ya kifedha wa Uefa, Mkuu wa Waamuzi wa Uefa na Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya FIFA.
Kupitia kazi hizi, Collina anakunja takribani Dola 4 milioni kwa mwaka kama mshahara na marupurupu. Mtaalamu huyu pia ana biashara zake binafsi ambazo pia zinaongeza kipato chake.
NYUMBA
Anamiliki mjengo wa kifahari huko Forte dei Marmi eneo maarufu la pwani la Italia ambalo ni eneo linalokaliwa na watu wengi maarufu na matajiri nchini humo.
Kijumla mjengo anaoishi unakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 2 milioni.
NDINGA
Hakuwa mtu wa magari sana lakini mara kadhaa alionekana akiendesha gari kutoka kampuni ya Opel kutoka Ujerumani ambayo ilichangia kufanya uamuzi wa kustaafu.
Collina alisaini dili la ubalozi na kampuni ya Opel lakini wakati huo, kampuni hiyo pia ilikuwa ikiidhamini AC Milan.
Timu nyingine za Serie A zililalamikia suala hilo na kueleza kwamba Collina anaweza kuipendelea Milan kutokana na mgongano wa maslahi. Chama cha soka cha Italia kikamtaka Collina aachane na dili hilo la Opel lakini yeye badala yake akaamua kustaafu jumla.
Dili lake la Opel linadaiwa kuwa lilikuwa likienda kumpa takribani Dola 10 milioni.
MSAADA KWA JAMII
Alihudumu kama mwamuzi wa matukio ya hisani kama Soccer Aid (matukio ya kuchangisha fedha kwa ajili ya shirika la misaada la UNICEF).
Pia ameshiriki kama mjumbe na mshirika wa miradi inayohusiana na mashirika kama SOS Children’s Villages kupitia FIFA.
Collina pia amekuwa akijitolea kuchezesha mechi mbalimbali za hisani ambazo zina lengo la kukusanya pesa ili kusaidia watu wenye uhitaji.
MAISHA BINAFSI
Collina alikutana na mkewe Gianna mwaka 1988 katika eneo la Versilia na tangu wakati huo wameishi pamoja na kufunga ndoa.
Wamebahatika kupata watoto wawili ambao wote ni wa kike. Licha ya sura yake kali uwanjani na heshima kubwa aliyoijenga kama mwamuzi, Collina katika maisha ya kawaida ni mtu anayejua kupumzika na kufurahia matunda ya kazi yake. Baada ya kustaafu uamuzi alibadilisha mwelekeo kidogo katika maisha na kutumia muda mwingi akiwa na familia yake katika jumba lake la kifahari huko Forte dei Marmi.