Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Orlando, Stellenbosch zatinga robo fainali CAF

Orlando Pict

Muktasari:

  • Orlando ikiwa uwanja wa nyumbani wa Orlando, jijini Johannesburg iliishindilia CR Belouizdad ya Algeria kwa mabao 2-1 katika mechi ya Kundi C na kufikisha pointi 11 baada ya kushuka uwanjani mara tano ikiungana na watetezi Al Ahly ambayo ilitangulia robo tangu jana usiku ilipoifumua Stade d'Abidjan ya Ivory Coast kwa mabao 3-1 ikiwa ugenini na kufikisha pointi 10.

TIMU mbili za Afrika Kusini, Orlando Pirates inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Stellenbosch iliyopo Kombe la Shirikisho zimefuzu hatua ya robo fainali jioni hii baada ya kila moja kushinda nyumbani na kuungana na vigogo vingine vilivyotangulia hatua hiyo kwa michuano hiyo ya CAF.

Orlando ikiwa uwanja wa nyumbani wa Orlando, jijini Johannesburg iliishindilia CR Belouizdad ya Algeria kwa mabao 2-1 katika mechi ya Kundi C na kufikisha pointi 11 baada ya kushuka uwanjani mara tano ikiungana na watetezi Al Ahly ambayo ilitangulia robo tangu jana usiku ilipoifumua Stade d'Abidjan ya Ivory Coast kwa mabao 3-1 ikiwa ugenini na kufikisha pointi 10.

Orlando iliandika bao moja kila kipindi na kuwazima wababe hao wa Algeria ambayo itamaliza mechi ya mwisho kukamilisha ratiba dhidi ya Waivory Coast wikiendi ijayo.

Bao la kwanza la Orlando liliwekwa kimiani dakika ya 20 kupitia kwa Relebohile Mofokeng lililodumu hadi mapumziko kabla ya Thalente Mbatha dakika ya 61 akimalizia pasi ya Patrick Maswanganyi na wageni walipata la kufutia machozi dakika za lala salama kupitia kwa Abdelraouf Benguit.

Orlando inakuwa timu ya tano kutinga robo fainali katika Ligi ya Mabingwa msimu huu, sambamba na watetezi Al Ahly na Pyramids za Misri, Far Rabat ya Morocco na Al Hilal ya Sudan ambayo usiku wa leo itakuwa wenyeji wa Yanga katika mechi ya Kundi A itakayopigwa huko Mauritania.

Orlando na Al Ahly zitavaana wikiendi ijayo katika mechi ya kukamilisha ratiba ya kundi hilo, lakini kuamua ipi imalize kama kinara wa kundi hilo na nyingine kukamata nafasi ya pili.

Katika mechi za Kombe la Shirikisho, Stellenbosch ikiwa Uwanja wa Danie Craven, mjini Stellenbosch, iliinyuka Stade Malien ya Mali kwa mabao 2-0 na kuwa timu ya tatu kutinga robo fainali hadi sasa ikiungana na vinara wana fainali wa msimu uliopita, RS Berkane ya Morocco waliopo kundi moja na timu hiyo ya Sauzi. Timu nyingine iliyofuzu hatua hiyo ni USM Alger ya Algeria iliyoifumua Orapa United ya Botswana ikiwa kwao kwa mabao 2-1.

Stellenboch inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza ikiwa imeanzishwa mwaka 2016 ilipata mabao hayo katika kipindi kwa kwanza kupitia kwa Fawaaz Basadien aliyefunga kwa penalti dakika ya 30 kabla ya mfungaji huyo kumsetia mpira Jayden Adams aliyekwamisha wavuni bao la pili dakika ya 39.

Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kufikisha pointi tisa ambazo haziwezi kufikiwa na Stade Malien au CD Luanda Sul ya Angola iliyolazimishwa suluhu jioni hii na vinara wa kundi B, Berkane yenye pointi 10 ikiwa ni timu ya kwanza kutinga mapema robo fainali tangu wiki iliyopita.

Kuanzia saa 1:00 usiku huu na Saa 4:00 usiku zitapigwa mechi nyingine zitakazotoa picha halisi ya timu nyingine za kutinga hatua hiyo ikiwamo kundi A lenye timu za CS Constantine, Simba na Bravos do Maquis, mbali na makundi mengine.