Neto akichafua, Chelsea ikiichapa Burnley kwao
Muktasari:
- Chelsea kwa muda ilikuwa ikifahamika kama timu isiyokuwa na maajabu endapo kama Palmer anapokosekana kwenye mechi yao, hasa kwenye eneo la kushambulia, lakini sasa winga wa Kireno, Neto ameamsha dude kwa kuwaonyesha kiwango matata akimweka benchi Estevao.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imezika rasmi jina la utani la ‘Cole Palmer FC’ shukrani kwa kiwango matata kabisa cha mshambuliaji Pedro Neto.
Chelsea kwa muda ilikuwa ikifahamika kama timu isiyokuwa na maajabu endapo kama Palmer anapokosekana kwenye mechi yao, hasa kwenye eneo la kushambulia, lakini sasa winga wa Kireno, Neto ameamsha dude kwa kuwaonyesha kiwango matata akimweka benchi Estevao.
Bao lake la kwanza alilofunga dakika 37 ilikuwa mara ya kwanza kwa Neto kufunga kwenye mechi mfululizo za Ligi Kuu England katika kipindi cha miaka mitano, hivyo kufikisha mabao matatu na asisti mbili katika mechi tano alizocheza.
Chelsea iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burnley uwanjani Turf Moor, huku bao jingine likifungwa na Enzo Fernandez kwenye kipindi cha pili. Kocha, Enzo Maresca uamuzi wake wa kuanzishia benchini Alejandro Garnacho na Estevao kuliamsha maswali mengi, lakini bao la Neto, alilofunga baada ya asisti ya Jamie Gittens lilishusha presha.
Chelsea imefanya uwekezaji mkubwa kwenye usajili wa mawinga, ikitumia Pauni 168 milioni, ambapo Neto alinaswa kwa Pauni 51.4 milioni, Agosti 2024 huku Garnacho na Estevao walinaswa kwa ada ya Pauni 69 milioni. Ushindi huo uliifanya Chelsea kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa kukusanya pointi 23 katika mechi 12.
Hata hivyo, hiyo ilikuwa kabla ya mechi nyingine za Jumamosi.
TAKWIMU ZA MCHEZO BURNLEY VS CHELSEA
-Mashuti golini: Burnley 2, Chelsea 5
-Mashuti yote: Burnley 8, Chelsea 15
-Mashuti yaliyozuiwa: Burnley 3, Chelsea 5
-Umiliki mpira: Burnley 44%, Chelsea 56%
-Pasi zote: Burnley 415, Chelsea 525
-Pasi sahihi: Burnley 325, Chelsea 439
-Kupiga takolin: Burnley 16, Chelsea 15
-Kucheza rafu: Burnley 13, Chelsea 9
-Kona: Burnley 1, Chelsea 9