Mpeni hawa wanne Amorim atakuwa moto
Muktasari:
- Amorim ameshinda mechi nne tu kati ya 11 za kwanza kwenye kikosi cha Man United, huku timu yake ikishindwa kufunga bao kwenye mechi tatu za mwisho na ushindi wake wa mwisho ulikuwa dhidi ya Manchester City kwenye Manchester derby.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imeingia kwenye Mwaka Mpya wa 2025 ikitokea kwenye vichapo vinne mfululizo na kumfanya kocha Ruben Amorim afahamu ni aina gani ya timu aliyoamua kujiunga nayo na mtihani mzito uliopo mbele yake.
Amorim ameshinda mechi nne tu kati ya 11 za kwanza kwenye kikosi cha Man United, huku timu yake ikishindwa kufunga bao kwenye mechi tatu za mwisho na ushindi wake wa mwisho ulikuwa dhidi ya Manchester City kwenye Manchester derby.
Kocha, Amorim, 39, alikiri kwamba alitamani kuchukua kibarua cha kuinoa timu hiyo kwenye kipindi cha majira ya kiangazi, kwamba afanye usajili wa mastaa anaowataka na kwenda nao kwenye pre-season kuwatengeneza vile anavyotaka wawe. Lakini, sasa ameingia katikati ya msimu na kilichopo mbele yake kwa sasa ni dirisha la usajili la Januari, ambalo atahitaji kuwafungulia mlango wachezaji asiowahitaji kama Marcus Rashford ili kuleta sura mpya.
Kunaweza kuwa na ugumu kwenye dirisha hili, lakini mashabiki wa Man United wana ndoto kubwa kwamba timu yao itasajili kurekebisha hali ya mambo.
Eneo mojawapo linalomsumbua Amorim ni beki ya upande wa kushoto, ambako Luke Shaw na Tyrell Malacia wote hawapo fiti kuingia kwenye mfumo wake wa 3-4-3. Jambo hilo linamfanya amtumie beki wa kulia, Diogo Dalot kucheza upande wa kushoto, ambalo limekuwa mtihani mzito kwake.
Hivyo kusajili beki anayetumia mguu wa kushoto anayesaidia ushambuliaji ni jambo muhimu kwa Amorim na hapo mpango ni kunasa saini ya Alphonso Davies wa Bayern Munich, ambaye pia yupo kwenye rada za klabu kibao ikiwamo Real Madrid. Wakala wake Davies, Nick Huoseh, amefichua wazi kusaka timu na hakika mchezaji huyo anaweza kwenda kufiti kwenye mfumo wa Man United.
Kutokana na viungo Christian Eriksen na Casemiro umri kuwatupa mkono, kocha Amorim atahitaji pacha wa kuja kucheza na Kobbie Mainoo sambamba na Manuel Ugarte na kwenye hilo mpango ni kumsajili Bruno Guimaraes wa Newcastle United. Staa mwingine wa tatu, ambaye Man United inahitaji saini yake ni Dani Olmo, ambaye alijiunga na Barcelona akitokea RB Leipzig mwaka jana kwa Pauni 51 milioni, lakini sasa ukata unamfanya ashindwe kuandikishwa kwenye La Liga kwa ajili ya kuitumikia miamba hiyo ya Nou Camp. Olmo atakuja kucheza pacha na Bruno Fernandes kwenye Namba 10 kuboresha ushambuliaji.
Mchezaji wa nne ambaye Man United inahitaji sana huduma yake ni mshambuliaji na kwenye hilo mpango ni kumsajili Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon, huku mpango wa timu hiyo ukiwa ni kuwaondoa kwenye kikosi Rashford na Joshua Zirkzee, lakini Rasmus Hojlund atabaki kusaidiana na straika mpya atakayeletwa.
Gyokeres ni mtambo wa mabao na Amorim anamfahamu vyema walipokuwa pamoja Sporting Lisbon, mahali ambapo alifunga mabao 70 katika mechi 77 alizocheza chini yake. Msimu huu straika huyo wa kimataifa wa Sweden amefunga mabao 27 katika mechi 27.
Kikosi kinachotarajiwa (3-4-3): Onana; Yoro, De Ligt, Martinez; Davies, Mainoo, Guimaraes, Amad; Fernandes, Olmo, Gyokeres.