Mmesikia? Mainoo katua kwenye rada za Chelsea
Muktasari:
- Mainoo mwenye umri wa miaka 19, mkataba wake wa sasa na mashetani wekundu unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
CHELSEA inadaiwa kuwa katika harakati za kutaka kumsajili kiungo wa Manchester United, Kobbie Mainoo ambaye mazungumzo yake na mabosi wa Man United juu ya mkataba mpya yanadaiwa kukwama.
Mainoo mwenye umri wa miaka 19, mkataba wake wa sasa na mashetani wekundu unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Staa huyu wa kimataifa wa England anadaiwa kuhitaji mshahara wa Pauni 200,000 kwa wiki pamoja na bonasi mbalimbali kutokana na mchango wake katika timu.
Hata hivyo, Man United imempa ofa ndogo ambayo haikaribii kiasi hicho hali iliyosababisha mazungumzo kusimama na hiyo imeziweka tayari baadhi ya timu ikiwemo Chelsea juu ya kumsajili mchezaji huyo.
Kwa sasa Mainoo ni miongoni mwa mastaa wanaokunja pesa kiduchu katika kikosi hicho ambapo kwa mujibu wa tovuti ya Spotrac.com anakunja Pauni 20,000 kwa wiki.
BORUSSIA Dortmund pia imeungana na timu Juventus na AC Milan kwenye mchakato wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na England, Marcus Rashford, 27, katika dirisha hili.
Rashford ni miongoni mwa wachezaji ambao wameomba kuondoka Man United katika dirisha hili akihitaji kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine baada ya kuwekwa nje ya kikosi.
MABOSI wa Eintracht Frankfurt wamesisitiza kwamba hadi sasa hawajapokea ofa yoyote kutoka kwa timu yoyote kuhusu mshambuliaji wao raia wa Misri, Omar Marmoush, 25, anayehusishwa na timu mbalimbali kubwa barani Ulaya ikiwa ni pamoja na Manchester City.
Marmoush ambaye ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Frankfurt, msimu huu amecheza mechi 24 za michuano yote na kufunga mabao 18.
RIPOTI zinaeleza mabosi wa Manchester United wapo tayari kusikiliza ofa kutoka timu mbalimbali zinazohitaji saini ya winga wao raia wa Argentina, Alejandro Garnacho, 20, pamoja na mshambuliaji wao kutoka Denmark, Rasmus Hojlund, 21, ambao kocha Ruben Amorim anadaiwa kutoridhishwa na utendaji kazi wao. Garnacho na Hojlund bado wameendelea kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.
NOTTINGHAM Forest ipo katika mazungumzo na wawakilishi wa beki wao raia wa Brazil, Murillo, 22, kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Murillo mwenye umri wa miaka 22, ameonyesha kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu hali inayosababisha timu nyingi kubwa barani Ulaya kutaka kumsajili.
ARSENAL imeonyesha nia ya kumsajili winga wa Athletic Bilbao na Hispania, Nico Williams, 22, katika dirisha hili lakini inashindwa kutimiza mchakato huo kutokana na masuala ya kiuchumi.
Nico alikuwa katika rada za Barcelona kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana lakini ilishindwa kutimiza mchakato huo. Mkataba wa Nico unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
PALMEIRAS inataka kumsajili kiungo wa Fulham na Brazil, Andreas Pereira, 29, lakini hadi sasa bado wanakumbana na wakati mgumu katika mazungumzo yao na Fulham juu ya masuala ya ada ya uhamisho. Pereira, 29, msimu huu amecheza mechi 18 za michuano yote na kufunga mabao 12.
BORUSSIA Dortmund imeingia katika mchakato wa kuiwania saini ya kiungo wa Chelsea na England, Carney Chukwuemeka, 21, ambaye amepewa ruhusa ya kuondoka katika dirisha hili au mwisho wa msimu ikiwa atapata timu itakayokuwa tayari kumsajili. Msimu huu amecheza mechi tano za michuano yote na mkataba unamalizika mwaka 2028.