Mbappe aomba msamaha China
Muktasari:
- Mzozo huo ulianza baada ya kipande cha mahojiano ya Mbappe katika kipindi cha mazungumzo cha Ufaransa, The Bridge, kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
PARIS, UFARANSA: NYOTA wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe amepoteza udhamini wa kibiashara kutoka kwa kampuni tatu za China baada ya kauli yake kuhusu aliyekuwa kiongozi wa zamani wa China, Mao Zedong, kuzua mjadala na hasira kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press (AP), kampuni za Dongpeng, Mengniu na Milkground zilitangaza Jumanne kusitisha mikataba yao na Mbappe. Ingawa kampuni hizo hazikueleza moja kwa moja sababu za kuvunja ushirikiano huo, taarifa zao zilirejelea kupinga “maneno na vitendo vinavyoumiza hisia za kitaifa.”
Mzozo huo ulianza baada ya kipande cha mahojiano ya Mbappe katika kipindi cha mazungumzo cha Ufaransa, The Bridge, kusambaa kwenye mitandao ya kijamii. Katika mazungumzo hayo, nyota huyo alizungumzia picha ya mzaha (meme) iliyohaririwa kwa kuweka uso wake kwenye picha ya Mao Zedong, akimtaja kiongozi huyo kuwa “dikteta wa China.”
Kauli hiyo ilizua malalamiko kutoka kwa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini China na kusababisha mjadala mpana kuhusu namna Mbappe alivyomrejelea kiongozi huyo wa kihistoria.
Kutokana na mwitikio huo, Mbappe alitoa taarifa ya kuomba radhi Jumanne, akikiri kuwa kauli yake haikuwa ya busara na kwamba sasa ameelewa jinsi ilivyowaumiza watu wengi nchini China na jamii za Wachina katika maeneo mengine duniani.
“Kauli yangu haikuwa ya busara, na sasa ninaelewa kuwa iliwaumiza watu wengi nchini China na katika jamii za Wachina duniani kote,” amesema Mbappe.
Aliendelea kusema: “Nawaomba radhi wote waliochukizwa na maneno yangu. Hilo halikuwa kabisa kusudio langu. Nina heshima kubwa kwa watu wa China na historia yao, na ninaomba radhi kwa dhati.”
Kabla ya Mbappe kutoa msamaha huo, La Liga ilitoa taarifa ya kujitenga na kauli zake. Hatua hiyo ilikuja wakati kukiwa na taarifa zilizodai kuwa matangazo ya mechi za ligi hiyo nchini China yalisimamishwa kufuatia mzozo huo.
Rais wa La Liga, Javier Tebas Medrano, naye aliomba radhi Jumanne kutokana na kauli ya Mbappe na kueleza kuwa ligi hiyo ilikuwa ikifanya kazi moja kwa moja na washirika wake nchini China kutafuta namna ya kutatua hali hiyo.
Tukio hilo limeweka doa katika uhusiano wa Mbappe na baadhi ya wadhamini wake nchini China, huku msamaha wake ukiwa hatua ya kujaribu kupunguza mvutano uliojitokeza kutokana na kauli hiyo.