MAZIKO! ‘Sikia mabao Barca hata baada ya kifo’
Muktasari:
- Mpango huo unakusudia kuwafanya mashabiki hao kuendelea kuwa karibu na timu yao hata baada ya kufariki dunia, ingawa kama ilivyo kwa mambo mengine yanayohusu Barcelona, kujitoa kwao kwa klabu hiyo kutakuwa na gharama.
BARCELONA, HISPANIA: MASHABIKI wa Barcelona watengewa eneo la kuhifadhi majivu yao katika uwanja mpya wa klabu hiyo wa Spotify Camp Nou ambayo itakuwa na sehemu 26,000 za kuhifadhi majivu ya mashabiki wa muda mrefu watakaofariki dunia.
Mpango huo unakusudia kuwafanya mashabiki hao kuendelea kuwa karibu na timu yao hata baada ya kufariki dunia, ingawa kama ilivyo kwa mambo mengine yanayohusu Barcelona, kujitoa kwao kwa klabu hiyo kutakuwa na gharama.
Katika sehemu ya maboresho ya Uwanja wa Camp Nou, klabu hiyo imeanzisha mradi wa Memorial FC Barcelona unaohusishwa na kumbukumbu za baada ya mashabiki kindakindaki kufariki dunia, na iwapo wao au jamaa zao wataridhia kwamba miili yao ichomwe moto kisha majivu yakahifadhiwe eneo hilo.
Inaelezwa kwamba kwa mashabiki watakaokuwa tayari ‘kuendelea kuishangilia’ timu hiyo hata baada ya kifo kutagharimu Euro 2,490 (takribani Sh7.3 milioni) kwa kipindi cha miaka 10 au Euro 6,000 (takriban Sh17,8 milioni) kwa miaka 50, pamoja na ada ya maboresho ya Euro 70 (zaidi ya Sh 207,691) kwa mwaka.
Hata hivyo, kwa wale wanaotaka kuhifadhi nafasi zao kwa kipindi chote cha maisha, gharama itakuwa Euro 10,000 (takriban Sh29.4 milioni), huku wakitakiwa kulipa Euro 490 (zaidi ya Sh1.4 milioni) zaidi kwa ajili ya bamba la kumbukumbu.
Akiutambulisha mradi huo wa Memorial FC Barcelona, Makamu wa Rais wa Masuala ya Taasisi wa klabu hiyo, Maria Elena Fort, anasema: “Babu yangu alipofariki (dunia) miaka mingi iliyopita, alisema kitu pekee alichokuwa anakitaka ni kuzikwa karibu na uwanja wa Barca ili aweze kusikia mabao yakifungwa hata baada ya kifo. Mashabiki wengi wana ndoto kama hiyo.”
Sehemu hiyo ya kumbukumbu itakuwa na ukubwa wa mita 1,500, iliyobuniwa na mbunifu wa majengo Quique Montoya, itakuwa na maeneo manne makubwa yenye mwanga, huku mabamba ya kumbukumbu yakiwekwa kwenye ukuta wa kioo wenye taa za LED.
Vyombo vitakavyohifadhi majivu vitawekwa nyuma ya michoro mikubwa itakayoonyesha matukio muhimu katika historia ya miaka 125 ya klabu hiyo. Pia kutakuwa na vipengele vya picha, video na sauti.
Mradi huo wa Memorial FC Barcelona unaofanyika umbali wa mita chache kutoka katikati ya uwanjani, utawapa mashabiki njia mbalimbali za kuhifadhi uhusiano wao na klabu pamoja na kutoa heshima kwa wapendwa wao.
Eneo hilo litakuwa wazi wakati wote, huku lilipo likiwezesha wanachama na mashabiki kufika kwa urahisi kutokana na kuwa katika mazingira ya mjini yenye huduma nzuri za usafiri.
Inaelezwa kwamba kutakuwa na njia mbili za kutoa heshima na kuhifadhi kumbukumbu za wapendwa waliotangulia mbele ya haki. Njia ya kwanza ni kuweka majivu yao katika sehemu maalumu ya kuhifadhi vyombo vyenye majivu, huku nyingine ikiwa ni kuandika jina na ujumbe kwenye bamba la kumbukumbu ndani ya uwanja huo.
Machaguo yote mawili yatapatikana kwa mashabiki wa Barcelona kutoka sehemu mbalimbali duniani, bila kulazimika kuwa wanachama wa klabu hiyo.
Mabamba hayo yatawawezesha mashabiki kuonyesha uhusiano wao na Barcelona katika uwanja huo mpya kwa kuandika majina yao au kutoa heshima kwa wapendwa wao waliofariki. Kila bamba litaweza kuwekwa jina na ujumbe maalumu wa kumbukumbu.
Kazi za ujenzi wa sehemu hiyo ya Barcelona zinatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka ujao, huku klabu hiyo ikisema zaidi ya mashabiki 1,000 wa Barca tayari wamewekewa nafasi zao, ambapo fedha zitakazopatikana kupitia mradi huo zitasaidia kugharamia gharama kubwa za ukarabati wa uwanja huo uliojengwa mwaka 1957. Mradi kama huo unaendeshwa pia na klabu za Hispania kama Atletico Madrid, Real Betis na Espanyol, ambazo tayari zina sehemu ndogo za kuhifadhi majivu ya marehemu ndani ya viwanja vyao.
MRADI WENYEWE
Tangu kuzinduliwa kwa mradi huo, mashabiki wengi, wanachama na watu waliowahi kuwa na uhusiano na klabu wameonyesha nia ya kushiriki katika Memorial FC Barcelona. Miongoni mwao wapo baadhi ya wachezaji wa zamani pamoja na ndugu wa watu mashuhuri waliowahi kuwa sehemu ya historia ya Barcelona.
Sehemu za kuhifadhi majivu na mabamba ya kumbukumbu zitapatikana kwa mikataba ya matumizi ya miaka 10, 25 au 50, huku watumiaji wakipewa nafasi ya kuchagua eneo wanalotaka ndani ya sehemu hiyo.
Sehemu ya kuhifadhi majivu itakuwa na nafasi za vyombo vya mtu mmoja mmoja, huku majina ya marehemu yakionyeshwa katika sehemu ya mbele ya kila nafasi.
Pia kutakuwa na chaguo la baadaye kuhamishia majivu katika chombo cha pamoja cha kuhifadhi majivu kwa kila aina ya mpango wa matumizi ya eneo hilo.
Hata hivyo, kwa wale watakaolipia mpango wa miaka 50, huduma hiyo tayari itakuwa imejumuishwa. Kumbukumbu binafsi na za kifamilia zikipata nafasi katika kumbukumbu za pamoja za mashabiki wa Barcelona.
UJENZI UWANJA
Mwaka 2023, Barcelona ilianza mpango wa kuongeza uwezo wa Uwanja wa Camp Nou kutoka watazamaji 99,354 hadi 105,000. Idadi hiyo ni kubwa kwa watazamaji 15,000 zaidi ya Uwanja wa Wembley uliopo England, jambo litakaloufanya kuwa uwanja wa pili kwa ukubwa duniani kwa michezo ya soka, nyuma ya Uwanja wa Rungrado 1st of May uliopo Pyongyang uliopo Korea Kaskazini.
Gharama za maboresho hayo, ambazo awali zilikadiriwa kuwa Euro 900 milioni (zaidi ya Sh2.65 trilioni), sasa zinakaribia Euro 2 bilioni (takriban Sh5.93 trilioni). Gharama hizo kwa sasa zinabebwa pia na mashabiki ambao hawana tiketi za msimu mzima, ambao wamekuwa wakikabiliwa na ongezeko la bei za tiketi mara mbili katika miaka ya hivi karibuni.
Kazi za ukarabati huo zinafanywa na kampuni ya Limak Construction kutoka Uturuki, lakini zimekuwa zikikwamishwa na ucheleweshaji pamoja na migogoro ya wafanyakazi. Mwaka 2024, Barcelona ilikiri kuwapo kwa ukiukwaji mbalimbali wa haki za wafanyakazi, ikiwamo zaidi ya wakandarasi wadogo 1,000 kutolipwa malipo ya saa za ziada walizofanya kazi.
Kazi hizo zinatarajiwa kukamilika baadaye mwaka huu, lakini klabu italazimika kucheza sehemu ya msimu ujao katika Uwanja wa Olimpiki wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 55,926 wakati paa jipya likiendelea kufungwa katika Uwanja wa Camp Nou.