Mastraika watakavyogonganisha klabu za Ulaya dirisha hili

Muktasari:
- Na kinachoelezwa ni kwamba kama kuna wachezaji watakaokwenda kutikisa dirisha la usajili la majira ya kiangazi huko kwenye Ligi Kuu England basi ni washambuliaji wa kati maarufu kama mastraika.
LONDON, ENGLAND: MSIMU wa Ligi Kuu England wa 2024-25 umeshafika tamati na sasa macho na masikio ya mashabiki wa timu zinazoshiriki ligi hiyo yameelezwa kwenye dirisha la usajili kuona ni wachezaji gani watakaoondoka na kuongezeka kwenye timu wanazozishangilia.
Na kinachoelezwa ni kwamba kama kuna wachezaji watakaokwenda kutikisa dirisha la usajili la majira ya kiangazi huko kwenye Ligi Kuu England basi ni washambuliaji wa kati maarufu kama mastraika.
Mabingwa wa Ligi Kuu England, Liverpool wataingia sokoni kutafuta mshambuliaji wa kati, wakati Arsenal ikifahamu wazi hilo ni pengo wanalohitaji kuliziba ili kuwa na kikosi chenye nguvu ya kushindania mataji msimu ujao baada ya kuona mshimu huu kuangushwa na kukosekana kwa mastraika kwenye kikosi.
Chelsea pia itaendelea na msako wa Namba 9, kama ambavyo imekuwa ikifanya muda wote madirisha ya usajili wa majira ya kiangazi yanapofunguliwa.
Na Manchester United - iliyomaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ikiwa ya chini zaidi kuwahi kushika kwenye historia katika michuano hiyo, inajiandaa kupanga mabadiliko kwenye kikosi ikiwamo kuingiza wachezaji wa maana wakiwamo mastraika wa kiwango cha dunia.
Jambo hilo linafanya kuwapo na uhitaji mkubwa wa mastraika, huku vita ikitarajiwa kuwa kali kwenye msako wa washambuliaji wa kati.

Viktor Gyokeres
Straika huyo mwenye umri wa miaka 26 anayeichezea Sweden kimataifa ndiye mshambuliaji wa kati anayesakwa zaidi na hilo linatokana na ubora wake wa uwanjani. Gyokeres amefunga mabao 54 katika mechi 52, huku 39 akifunga mechi 33 za ligi. Arsenal ipo namba moja kwenye mbio za kuwania saini ya straika huyo mwenye kimo cha futi 6 na inchi 2, ambaye klabu yake ya Sporting Lisbon inamthaminisha kuwa na thamani ya Pauni 60 milioni. Man United nayo inamtaka, lakini Arsenal na Chelsea ndizo zenye nafasi kubwa baada ya kumpa nafasi ya kwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya akichagua kujiunga na moja ya timu hizo mbili.

Liam Delap
Mtoto wa gwiji wa Stoke City, Rory anaonekana kuwa na uhakika wa kuachana na Ipswich Town dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya Tractor Boys’ kushuka daraja. Na kwa mujibu wa kipengele kilichopo kwenye mkataba wake, Delap anaweza kupatikana kwa Pauni 30 milioni jambo linaloziingiza vitani Chelsea na Man United. Akiwa na umri wa miaka 22, straika huyo amemaliza msimu wa Ligi Kuu England akifunga mabao 12, huku soka lake la kutumia nguvu na mwili wake ulivyojengeka linazipa timu hizo hamu ya kuwa naye. Chelsea na Man United zinamtaka, lakini ripoti zinafichua, The Blues ndio wenye nafasi kubwa kutokana na kocha Enzo Maresca kuwahi kufanya kazi na Delap akademia Man City.

Victor Osimhen
Straika huyo Mnigeria kuna kipindi alikuwa gumzo la Ulaya na kusakwa na timu nyingi baada ya kuonyesha makali yake alipokuwa na kikosi cha Napoli, alipokisaidia kushinda ubingwa wa Serie A. Lakini, kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2024, kocha mpya wa Napoli, Antonio Conte aliamua kumpiga chini Osimhen na kumpa nafasi Romelu Lukaku. Chelsea ilikaribia kumsajili Osimhen, lakini mahitaji yake ya kutaka alipwe mshahara mkubwa ulizuia dili hilo kukamilika. Hivyo, mkali huyo alikwenda kujiunga na Galatasaray kwa mkopo na kwenda kuwasaidia kubeba ubingwa wa ligi baada ya kufunga mabao 25 katika mechi 29 huku akimaliza msimu kwa kufunga mabao 36 katika mechi 40 za michuano yote.

Benjamin Sesko
Straika huyo mwenye kimo cha futi 6 na inchi 5 yupo kwenye rada za klabu ya Arsenal kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, wakimhitaji Sesko endapo kama watakwama kwa Gyokeres. Sesko amefunga mabao 21 katika mechi 45 alizocheza msimu huu, huku mabao 13 akifunga kwenye mechi 33 alizocheza kwenye ligi.
Kimo chake na uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya vichwa hicho ndizo kitu kinachomfanya timu nyingi za Ligi Kuu England kuhitaji saini yake. Ripoti zinafichua kwamba klabu yake inamchukulia kuwa na thamani ya Pauni 86 milioni, lakini mabosi hao wa RB Leipzig watakuwa tayari kupokea ofa ya Pauni 60 milioni.
Chelsea imekuwa na mpango wa kumfukuzia mshambuliaji huyo, lakini baada ya kuona Timo Werner na Christian Nkunku waliotokea Leipzig wakishindwa kung’ara baada ya kutua Stamford Bridge hilo limewatia wasiwasi. Man United nayo inamtaka Sesko, lakini kama itakwama kwenye dili zake nyingine.

Hugo Ekitike
Straika Mfaransa mwenye umri wa miaka 22, alijiunga na Frankfurt kwa dili la jumla akitokea PSG kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana baada ya kutumia msimu mmoja kabla ya hapo kwa mkopo. Ekitike alifunga mabao 22 katika mechi 48 alizocheza msimu huu, akitumbukiza nyavuni mara 15 katika mechi 33 za ligi. Akiwa na kimo cha futi 6 na inchi 3 amezifutia timu nyingi ikiwamo Chelsea, huku Arsenal na Man United zikidaiwa kwa muda mrefu kumweka kwenye orodha ya wachezaji inaowataka.
Lakini, Frankfurt imeshikilia ikitaka ilipwe Pauni 83.9 milioni, jambo ambalo linaifanya Chelsea pekee kuwa na uwezo wa kumsajili mchezaji huyo licha ya washambuliaji Gyokeres, Delap na Sesko kudaiwa kuwa ndiyo wanaopewa nafasi kubwa zaidi na Chelsea.

Julian Alvarez
Straika huyo wa Kiargentina alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati alipokuwa kwenye kikosi cha Man City kabla ya kutimkia zake Atletico Madrid wakati wa dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Alvarez amefunga mabao 29 katika mechi 54 alizocheza msimu huu, huku mabao 17 akifunga katika mechi 37 alizocheza kwenye ligi. Straika huyo mwenye umri wa miaka 25 anaonekana kutuliza daruga zake kwenye soka la Hispania, lakini Arsenal na Liverpool zinamtaka ili arudi kukipiga kwenye Ligi Kuu England. Lakini, ripoti za kutoka Hispania zinadai kwamba Alvarez hayupo tayari kurudi England kwa sababu mambo yake yapo vizuri Atletico Madrid.

Moise Kean
Fowadi huyo Mtaliano ana uzoefu wa Ligi Kuu England baada ya kuwahi kuitumikia Everton katikati ya vipindi vyake vya mkopo PSG na Juventus. Alijiunga na Juventus mwaka 2023 na kisha alihamia Fiorentina mwaka mmoja baadaye, amefunga mabao 25 katika mechi 44 - huku mabao 19 alifunga kwenye mechi 32 alizocheza kwenye ligi msimu huu. Man United imeripotiwa kumweka kwenye orodha washambuliaji inaowasaka kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Na fowadi huyo mwenye umri wa miaka 25 anaweza kuibukia na kuwa mbadala muhimu kwenye kikosi cha Man United ambacho kinahitaji mchezaji wa kuwafungia mabao kwa msimu ujao hasa ikizingatiwa kwamba hawatakuwa kwenye michuano ya Ulaya, ambayo itawaweka kwenye wakati mgumu wa kupata wachezaji bora zaidi.