Mastaa wa NBA wanavyotesa na rekodi zao
Muktasari:
- Lakini, wakati ligi hiyo ikishika kasi, LeBron James na Chris Paul walikuwa mastaa wawili wa kwanza wenye umri wa miaka 39 au zaidi kutengeneza kila mmoja pasi katika mchezo mmoja.
SAN FRANCISCO, MAREKANI : DRAYMOND Green alifunga pointi 13, rebaundi nane na asisti saba kabla ya kutolewa uwanjani mwishoni mwa mchezo kwa makosa mawili ya kiufundi ndani ya sekunde 33, Golden State Warriors wakishinda dhidi ya Memphis Grizzlies kwa pointi 123-118 kwenye mchezo wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA).
Lakini, wakati ligi hiyo ikishika kasi, LeBron James na Chris Paul walikuwa mastaa wawili wa kwanza wenye umri wa miaka 39 au zaidi kutengeneza kila mmoja pasi katika mchezo mmoja.
Chris anayeichezea San Antonio Spurs na Lebron anayekipiga Los Angeles Lakers walifanya hivyo katika mchezo uliozikutanisha timu hizo ambapo Sans walifungwa kwa pointi 115-120.
Mara nyingine pekee ambapo wachezaji wawili wenye umri wa miaka 37 au zaidi walifanya hivyo ilikuwa Februari 17, 2011 wakati Jason Kidd (Dallas Mavericks) na Steve Nash (Phoenix Suns) walitoa asisti kwa wachezaji wenzao katika mchezo uliozikutanisha timu hizo.
Kwa upande mwingine imekuwa ni wiki tamu kwa staa wa New York Knicks, Karl-Anthony Towns ambaye katika mechi 11 akiichezea amevunja rekodi ya ufungaji wa mitupo mitatu akiwa na ‘threes 30’ na rebaundi 125.
Kwa mujibu wa rekodi za NBA hakuna mchezaji mwingine katika historia ya mashindano hayo aliyeifikia alama hizo katika mechi chache zaidi ya 13.
Utamu wa ligi hiyo pia haujamuacha nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry ambaye ameandika rekodi yake kwani katika miaka 15 iliyopita, ni mara mbili tu mchezaji wa NBA kawa na mfululizo wa dakika nne za mwisho kubadili matokeo akifunga alama mbili za ushindi bila mchezaji mwingine kufunga kipindi hicho.
Wiki hii pia imekuwa bora kwa mastaa Giannis Antetokounmpo (Milwaukee Bucks) aliyefunga pointi 59 katika ushindi dhidi ya Detroit Pistons 127-120, lakini jana Pistons nayo ikaifunga Toronto Raptors kwa pointi 99-95 ugenini.
Pia Victor Wembanyama (San Antonio Spurs) alichangia 50 dhidi ya Lakers, huku Towns akiwa nazo 46 na Jordan Poole (Washington Wizards 42) katika kichapo walichopata cha 129-117 kutoka kwa Atlanta Hawks.
Kimsingi hakujawahi kutokea katika historia ya NBA kuwa na mchezaji mmoja mwenye alama zaidi ya 55, mwingine zaidi ya 50, mwingine zaidi ya 45 na mwenye alama zaidi ya 40 katika siku moja ya mechi.