Mastaa hawa fainali ni kawaida

Muktasari:
- Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 15 nchini Marekani ikihusisha timu 32 hadi sasa kuna wachezaji wanaongoza zaidi kwa kufika fainali. Baadhi ya mastaa hao wamefika fainali nyingi na kushinda zote, lakini wapo wengine waliotinga nyingi na kupoteza baadhi.
NEW YORK, MAREKANI: UTAMU wa michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia inayokuja kwa mfumo mpya unakaribia kuanza huku, zianikwa baadhi ya rekodi zilizowahi kuwekwa na zinazoweza kuwekwa katika mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi ya klabu duniani.
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 15 nchini Marekani ikihusisha timu 32 hadi sasa kuna wachezaji wanaongoza zaidi kwa kufika fainali. Baadhi ya mastaa hao wamefika fainali nyingi na kushinda zote, lakini wapo wengine waliotinga nyingi na kupoteza baadhi.
Hawa hapa mastaa ambao wamecheza fainali nyingi zaidi za michuano hiyo na mabao waliyofunga na mataji waliyoshinda.
11. Lionel Messi (3)
Hadi sasa nyota wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi ana mataji tatu katika fainali tatu alizocheza za michuano hiyo ingawa bado ana nafasi ya kuongeza ikiwa atafanya vizuri na timu yake ya Inter Miami ambayo itashiriki mwaka huu.
Messi alifika fainali tatu akiwa na Barcelona ambapo ya kwanza ilikuwa 2009 zilizopigwa katika Falme za Kiarabu pamoja na 2011, 2015 zilipofanyika nchini Japan.
Katika fainali tatu zile mbili alifanikiwa kufunga ambapo alianza dhidi ya Estudiantes 2009 kisha Santos 2011.
10. Andres Iniesta (3)
Mmoja kati ya viungo bora kuwahi kutokea katika kikosi cha Barcelona, Andres Iniesta akiwa katika kikosi cha Barcelona iliyoshiba wakati huo alifanikiwa kushinda mataji matatu baada ya kucheza fainali tatu za michuano hiyo. Fainali alizocheza ni ile ya 2009, 2011 na 2015 ambapo alifunga bao moja katika fainali ya 2011 dhidi ya Santos ya Brazil kwenye michuano iliyofanyika nchini Japan. Mechi hiyo ilimalizika kwa Barcelona kushinda mabao 4-0.
9. Dani Alves (3)
Dani Alves pia ana medali tatu za michuano hiyo katika kabati lake kwani fainali alizocheza ni pamoja na ile ya 2009, 2011 na 2015. Alves ambaye alicheza kama beki wa kulia katika fainali zote licha ya kutofunga bao, alihusika katika kupandisha mashambulizi jambo lililosababisha kutengenezwa kwa mabao mengi.
8. Xavi Hernandez (3)
Kiungo mwingine hatari kuwahi kutokea katika historia ya Barcelona, Xavi Hernandez ambaye baadaye alikwenda kuiongoza timu hiyo kama kocha. Xavi ambaye anasifika kuwa ndiye alitengeneza Barcelona ya sasa inayoonekana kuwa na mafanikio kupitia vijana aliowakuza amecheza fainali tatu na timu hiyo na kushinda zote. Fainali alizocheza ni zile za 2009, 2011 na 2015. Hata hivyo, hakuna hata moja kati ya hizo alizofanikiwa kufunga bao.
7. Cristiano Ronaldo (3)
Kimahesabu Cristiano Ronaldo anaonekana kuchukua mataji manne ya michuano hiyo, lakini fainali alizocheza ni tatu kwani ile ya 2008 aliyochukua akiwa na Manchester United hakuwepo katika mchezo wa fainali. Fainali nne alizocheza ni pamoja na ile iliyopigwa Morocco 2014, Japan 2016 na Falme za Kiarabu 2017 na 2018. Pia alifunga katika fainali mbili - ile ya 2014 dhidi ya San Lorenzo kutoka Argentina na pia bao moja 2016 dhidi ya Kashima Antlers ya Japan. Katika fainali hizo nne, Ronaldo amefanikiwa kushinda tatu.
6. Sergio Ramos (4)
Sergio Ramos ni staa mwingine kutoka Real Madrid ambaye amecheza fainali hizo mara nyingi akiwa amecheza nne ambazo ni zile za 2014, 2016, 2017 na 2018. Katika fainali hizo alifanikiwa kuvaa medali za ubingwa mara zote na 2016 alifunga bao dhidi ya Kashima Antlers ya Japan.
5. Luka Modric (4)
Kama ilivyokuwa kwa Marcelo, Luka Modric licha ya kucheza mara nne katika fainali za michuano hiyo hakuwahi kufunga hata bao moja. Katika fainali hizo pia staa huyo ambaye ameachana na Real Madrid mwisho wa msimu uliopita zote aliisaidia timu yake kupata ushindi. Fainali alizocheza ni pamoja na ile ya 2014 iliyopigwa Morocco, 2016 ya Japan na 2017, 2018 zilizopigwa Falme za Kiarabu.
4. Karim Benzema (5)
Benzema pia akiwa na Real Madrid ni miongoni mwa mastaa walioinjoi michuano hiyo kwa kushinda mataji matano. Nyota huyo amecheza fainali tano kama ilivyo kwa wenzake wengi, lakini pia akifunga bao moja alilotia kambani 2016 katika fainali dhidi ya Kashima Antlers ya Japan.
3. Marcelo (5)
Marcelo alicheza fainali tano, lakini hakuna hata moja aliyofanikiwa kufunga bao na zote hizo alicheza akiwa na Realn Madrid kuanzia ile ya 2014, 2016, 2017, 2018 na 2013. Beki huyo ambaye kwa sasa amerudi zake Brazil kumalizia soka ni miongoni mwa mabeki wa kushoto waliocheza kwa kiwango bora katika fainali hizo ambazo zote zilimalizika kwa Real Madrid kuibuka na ushindi.
2. Thomas Muller (5)
Hadi sasa Thomas Muller ndiye anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza fainali nyingi zaidi za michuano hiyo akicheza tano za 2013 nchini Morocco, Falme za Kiarabu 2014, Japan 2015, Qatar 2020 na Falme za Kiarabu 2021. Katika fainali hizo Muller akiwa na Bayern Munich tatu alimaliza kwa kuchukua ubingwa huku mbili akipoteza. Vilevile ni miongoni mwa mastaa wanaoongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika mechi za fainali akifanya hivyo mara nne.
Mara ya kwanza ilikuwa 2013 alipofunga bao moja dhidi ya Raja Casablanca, akafunga bao mbele ya Al Ahly 2020 katika fainali zilizopigwa huko Qatar. Fainali ya mwisho kufunga bao ilikuwa 2021 dhidi ya Palmeiras katika michuano iliyopigwa katika Falme za Kiarabu.
1. Toni Kroos (6)
Hadi sasa Toni Kroos ndiye mchezaji anayeongoza zaidi kwa kucheza fainali nyingi za michuano hiyo akikipiga mara sita na zote timu zake ziliibuka na ushindi. Fainali moja kati ya sita alicheza akiwa na Bayern Munich 2023 ambapo walishinda dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco. Pia aliwahi kucheza fainali tano akiwa na Real Madrid 2014, 2016, 2017, 2018 na 2023 ambazo zote zilimalizika kwa Real Madrid kutwaa ubingwa.