Manchester United yapanga mikakati kwa Osimhen

Muktasari:
- Ripoti zinaeleza mabosi wa Man United wanataka kumtumia staa wao raia wa Uholanzi, Joshua Zirkzee, 24, kama sehemu ya dili hilo ili kutoa pesa kiduchu.
MANCHESTER United inafanya majadiliano ya ndani kuhusu ofa ambayo inaweza kuiandaa kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Napoli na timu ya taifa ya Nigeria, Victor Osimhen, mwenye umri wa miaka 26.
Ripoti zinaeleza mabosi wa Man United wanataka kumtumia staa wao raia wa Uholanzi, Joshua Zirkzee, 24, kama sehemu ya dili hilo ili kutoa pesa kiduchu.
Hivi karibuni Osimhen alikataa ofa ya kujiunga na Al-Hilal katika dirisha dogo lililopita lililofunguliwa maalum kuzipa nafasi timu zinashiriki Kombe la Dunia la klabu.
Fundi huyu bado anahitaji kuendelea kucheza soka la kiushindani. Timu nyingi zinataka kumsajili lakini zinarudi nyuma kutokana na ada ya uhamisho.
Mkataba wake unaisha 2026. Galatasaray ambayo aliichezea kwa mkopo msimu uliopita inamhitaji jumla pia.
Martin Zubimendi
ARSENAL imekubali kutoa ada ya takriban Pauni 59 milioni kwa ajili kumsajili kiungo wa Real Sociedad na Hispania, Martin Zubimendi, mwenye umri wa miaka 26, katika dili ambalo linatarajiwa kukamilika Julai 01 mwaka huu.
Katika msimu uliomalizika Zubimendi ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, alicheza mechi 48 za michuano yote.
Benjamin Sesko
MSHAMBULIAJI wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Slovenia, Benjamin Sesko, mwenye umri wa miaka 22 – anayehusishwa na Arsenal alikataa kujiunga na Al-Hilal ya Saudi Arabia, siku moja kabla ya dirisha la muda la usajili kufungwa juzi, Jumanne.
Sesko ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, msimu uliomalizika alicheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao 21.
Milos Kerkez
BEKI wa kushoto wa Bournemouth na timu ya taifa ya Hungary, Milos Kerkez, mwenye umri wa miaka 21, yuko karibu kujiunga na Liverpool kwa ada ya Pauni 45 milioni katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Liverpool imepata matumaini ya kumsajili Kerkez katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya Bournemouth kukubali kumsajili beki wa kushoto wa Rennes na Ufaransa Adrien Truffert, 23.
James Trafford
NEWCASTLE United imefungua mazungumzo na Burnley kuhusu kumsajili kipa wake raia wa England James Trafford, mwenye umri wa miaka 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Awali, Trafford alikuwa akihusishwa na Manchester United, lakini imeshaachana na mpango wa kumsajili. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Joao Pedro
BRIGHTON iko tayari kukubali ofa ya kati ya Pauni 50 hadi 60 milioni kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wake wa kimataifa wa Brazil, Joao Pedro, 23, ambaye anahitajika na Newcastle United.
Pedro ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Brighton, msimu uliopita alicheza mechi 52 za michuano yote na kufunga mabao matano.
Benoit Badiashile
CHELSEA iko tayari kupokea ofa kwa ajili ya kuwauza mabeki wake Benoit Badiashile, 24, na Axel Disasi, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mabeki hawa wanadaiwa kuwa hawapo katika mipango ya kocha Enzo Maresca ambaye ametoa ruhusa ya kuuzwa kwao.
Julio Enciso
INTER Milan inataka kumsajili kiungo wa Brighton na Paraguay, Julio Enciso, mwenye umri wa miaka 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kuvutiwa na kiwango alichoonyesha katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Katika msimu uliopita, Enciso alicheza mechi 29 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani.