Man United kuipiku Arsenal kwa Viktor Gyokeres

Muktasari:
- Gyokeres ni mmoja kati ya washambuliaji bora na Man United inataka kumchukua ili kutibu tatizo la ukosefu wa mabao ya kutosha kutoka kwa washambuliaji wao.
MANCHESTER United ina matumaini kwamba inaweza kumshawishi mshambuliaji wa Sporting na timu ya taifa ya Sweden, Viktor Gyokeres, 26, kujiunga nayo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo Lisbon imemruhusu kuondoka ikiwa itapatikana timu itakayokuwa tayari kulipa kiasi cha pesa kinachohitajika.
Gyokeres ni mmoja kati ya washambuliaji bora na Man United inataka kumchukua ili kutibu tatizo la ukosefu wa mabao ya kutosha kutoka kwa washambuliaji wao.
Licha ya matumaini ambayo Man United inaonekana kuwa nayo, ripoti zinaeleza Arsenal inapambana kufanya kila linalowezekana ili kumsajili fundi huyu.
Mkataba wa sasa wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, msimu huu amecheza mechi 51 za michuano yote na kufunga mabao 53.
Mkali huyo mashine ya mabao amehusika katika mabao 121 katika mechi 99 za misimu miwili akifunga mabao 96 na kutoa asisti 25.
Anasemekana kuuzwa kwa Euro 65 milioni.
LIAM DELAP
NEWCASTLE United ni kati ya timu zilizoingia katika vita ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Ipswich Town na England mwenye umri wa miaka 22, Liam Delap kwa ajili ya kumsajili katika dirisha hili.
Vigogo wengi wanataka kumsajili staa huyu kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu ambapo hadi sasa amefunga mabao 12, katika mechi 39 za michuano yote.
Mbali ya Newcastle, saini ya staa huyu pia inahitajika na Chelsea na Manchester United.
MILOS KERKEZ
MANCHESTER City inatarajia kuingia katika vita dhidi ya Liverpool kwa ajili ya kumsajili beki wa kushoto wa Bournemouth na timu ya taifa ya Hungary, Milos Kerkez, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kerkez ambaye pia mara kadhaa amehusishwa na Real Madrid, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, msimu huu amecheza mechi 40 za michuano yote.
DARWIN NUNEZ
LIVERPOOL imepokea maombi ya kutoka timu kadhaa za Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambazo zinahitaji huduma ya mshambuliaji wake wa kimataifa wa Uruguay mwenye umri wa miaka 25, Darwin Nunez, na mawinga wake kutoka Ureno, Diogo Jota na Colombia, Luis Diaz, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Kwa mujibu wa taarifa ofa hizo zinadaiwa kufikia Pauni 70 milioni kwa kila mmoja.
EMILIANO MARTINEZ
ASTON Villa haina mpango wa kumzuia kipa wake raia wa Argentina, Emiliano Martinez, 32, kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Hivi karibuni Emiliano alionekana akiwaaga mashabiki wa Villa jambo lililoibua tetesi kwamba huenda akaondoka mwisho wa msimu ambapo tayari kuna timu kibao zilizoonyesha nia ya kumsajili.
RAPHINHA
BARCELONA imefikia makubaliano na mshambuliaji wa Brazil, Raphinha kuhusu mkataba mpya ambao utamwezesha kusalia katika kikosi hicho hadi Juni, 2028.
Raphinha ambaye ni mmoja kati ya wachezaji walioonyesha kiwango bora kwa msimu huu kiasi cha kuisaidia Barca kuchukua ubingwa, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
JORREL HATO
CHELSEA imeanza mazungumzo na Ajax kuhusu uwezekano wa kumsajili beki kisiki wa timu hiyo, Uholanzi, Jorrel Hato, mwenye umri wa miaka 19, ambaye pia anawindwa na Liverpool na Arsenal. Hato ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Ajax, msimu huu amecheza mechi 50 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
HARVEY ELLIOTT
WOLVES wanapambana sana kuhakikisha wanaipata huduma ya kiungo wa Liverpool na timu ya taifa ya England, Harvey Elliott, mwenye umri wa miaka 22.
Elliot anataka kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Liverpool. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.