Madrid v Man City kuna mtu atapata aibu
Muktasari:
- Kwa miaka ya karibuni, miamba hiyo imekutana mara kadhaa, huku usiku wa leo kipute kitakuwa huko Bernabeu, katika mechi ya marudiano ya raundi ya mchujo ili kukatia tiketi ya 16 Bora ya michuano hiyo.
MADRID, HISPANIA: MWISHO wa ubishi wote ni usiku wa leo, juu ya swali la timu gani itapenya kwenda mtoano wa hatua ya 16 Bora katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Real Madrid na Manchester City.
Kwa miaka ya karibuni, miamba hiyo imekutana mara kadhaa, huku usiku wa leo kipute kitakuwa huko Bernabeu, katika mechi ya marudiano ya raundi ya mchujo ili kukatia tiketi ya 16 Bora ya michuano hiyo.
Mchezo wa kwanza uliofanyika Etihad, Jumanne iliyopita, Real Madrid ilishinda ugenini 3-2. Je, Man City itapindua meza na kushinda ugenini? Au Madrid itaendelea na ubabe wake katika Ligi ya Mabingwa Ulaya?
Mechi hiyo inakutanisha makocha wawili wenye mafanikio makubwa kwenye soka, Carlo Ancelotti na Pep Guardiola. Lakini, uwanjani pia kutakuwa na vita kali, ambapo upande wa Los Blancos kutakuwa na Kylian Mbappe, Vinicius Jr na Jude Bellingham, ule wa Cityzen utakuwa na Erling Haaland, Kevin de Bruyne na Phil Foden. Moto utawaka.
Vita ya kujuana na kasheshe la Ballon d'Or
Timu hizo zimekutana mara 13 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu msimu wa 2012-13, huku kila timu ikishinda mara nne na mechi tano zilimalizika kwa sare. Lakini, kama hizi zenye hadhi ya mtoano, ndizo zilizovutia zaidi wakati miamba hiyo ilipokutana. Kazi ipo.
"Nahisi kama vile ni vita ya kizazi hiki kwa sababu tumekutana mara nyingi kwenye michuano hii kwa miaka ya karibuni," amesema Ancelotti na kudai ni mechi ambayo inaweza kuamuliwa na uwezo binafsi.
Baada ya kupoteza kwa jumla ya mabao 6-5 mbele ya Madrid katika nusu fainali 2021-22, Man City iliichapa miamba hiyo ya Hispania 5-1 kwenye mechi mbili za hatua kama hiyo mwaka uliofuatia ilipokwenda kushinda taji. Timu hizo zilikutana tena mwaka jana, ambapo Real Madrid ilipindua meza katika mechi ya marudiano ya robo fainali uwanjani Etihad baada ya mechi hiyo kucheza kwa dakika 120 kabla ya kupigiana penalti.
Msimu huu timu hizo zitachuana katika mchujo wa kuwania tiketi ya kucheza mtoano wa 16 Bora.
Kuongeza utamu wa mechi hiyo unaongezwa na vita ya Ballon d'Or ya mwaka jana, ambapo Madrid iligoma kupeleka mtu kwenye sherehe ambazo zilimshuhudia kiungo wa Man City, Rodri akiibuka mshindi mbele ya mkali wa Los Blancos, Vini Jr.
'Don Carlo' v Pep 'the innovator'
Carlo Ancelotti na Pep Guardiola wote wameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwanza wakiwa wachezaji na baadaye wakiwa makocha. Ancelotti, ambaye amepachikwa jina la 'Don Carlo' huko Hispania, ni kocha mwenye mafanikio makubwa zaidi katika michuano hiyo ya Ulaya, akishinda ubingwa mara tano. Amecheza fainali sita za michuano hiyo kama ilivyo kwa Guardiola. Ancelotti pia alishinda ubingwa wa Lgi kati ya Ligi zote tano kubwa za Ulaya - England, Hispania, Ujerumani, Italia na Ufaransa.
Guardiola, ambaye anatajwa kama mbunifu (The innovator) naye ameshinda ubingwa wa Ligi kati ya Ligi kubwa tatu za Ulaya ambazo amewahi kufanya kazi kama kocha, La Liga, Bundesliga na Ligi Kuu England.
Guardiola ni kocha mwenye ufundi mwingi na mbunifu wa mambo mengi ndani ya uwanja jambo ambalo limekuwa silaha kubwa kwake katika kuwatesa wapinzani wake. Atafanya nini usiku wa leo?
Katika vita ya wenyewe kwa wenyewe Don Carlo na The innovator, Guardiola ameshinda sita dhidi ya nne za Ancelotti, huku timu ya fundi wa Kihispaniola ikifunga maba 28 na kuruhusu 21 katika mechi 13.