Liverpool yaingia vitani kuisaka saini ya Osimhen

Muktasari:
- Osimhen ambaye anahusisha na timu mbalimbali za England ikiwemo Manchester United, hivi karibuni alikataa ofa nono kutoka kwa Al-Hilal ya Saudi Arabia akisisitiza kuwa bado anahitaji kuendelea kucheza soka la kiushindani.
LIVERPOOL wamejitosa katika vita ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Napoli na timu ya taifa ya Nigeria Victor Osimhen, mwenye umri wa miaka 26, ambaye msimu uliopita alikuwa kwa mkopo Galatasaray.
Osimhen ambaye anahusisha na timu mbalimbali za England ikiwemo Manchester United, hivi karibuni alikataa ofa nono kutoka kwa Al-Hilal ya Saudi Arabia akisisitiza kuwa bado anahitaji kuendelea kucheza soka la kiushindani.
Mabosi wa Liverpool wanataka kumsajili Osimhen kwa sababu hawana uhakika ikiwa wataendelea kuwa na Darwin Nunez ambaye timu za Saudi Arabia zimeendelea kumfatilia.
Napoli ipo tayari kumuuza mshambuliaji huyu ambaye mkataba wake unamalizika mwakani lakini wanahitaji karibia Euro 70 milioni kama ada ya uhamisho kiasi ambacho kinaonekana sio kikubwa sana kwa Liverpool ambayo inafungu la kutosha la kufanyia usajili katika dirisha hili.
Jarell Quansah
BAYER Leverkusen inataka kumsajili beki wa kati wa Liverpool, Jarell Quansah, mwenye umri wa miaka 22, katika dirisha hili la usajili majira ya kiangazi. Inaelezwa Liverpool ipo tayari kumuuza staa huyu lakini inahitaji Pauni 40 milioni. Awali Liverpool ilihitaji kufanya mabadilishano ya wachezaji kwa kumjumuisha fundi huyu katika dili la kumpata Florian Wirtz pamoja na kutoa pesa kidogo, lakini sasa inamuuza kivyake.
Bradley Barcola
MABOSI wa Paris Saint-Germain wanadaiwa kutaka kukataa ofa yoyote itakayokuja mezani kwao kwa ajili ya mshambuliaji wao wa kimataifa wa Ufaransa, Bradley Barcola, mwenye umri wa miaka 22, ambaye anawindwa na Liverpool na Bayern Munich katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Ripoti za awali zilidai PSG ilikuwa tayari kumuuza fundi huyu lakini kwa zaidi ya Pauni 60 milioni, lakini sasa inaonekana haitaki kumwachia na kuendelea kumtumia.
Hugo Ekitike
MANCHESTER United inataka kumsajili mshambuliaji wa Kimataifa wa Ufaransa, Hugo Ekitike, mwenye umri wa miaka 22, kutoka Eintracht Frankfurt kwa ada inayoweza kufikia Pauni 85 milioni. Vigogo wa Man United wanataka kumsajili staa huyu kama mbadala ikiwa watashindwa kuzipata saini za washambuliaii ambao zimewaweka kama kipaumbele. Ekitie anawindwa pia na Newcastle na Liverpool.
Nico Williams
ARSENAL inajaribu kufanya kila linalowezekana ili kuipiku Bayern Munich kwenye dili la winga wa Athletic Bilbao na timu ya taifa ya Hispania, Nico Williams, mwenye umri wa miaka 22. Williams inadaiwa kuwa karibu kujiunga na Bayern Munich baada ya timu hiyo kufikia makubaliano na Bilbao juu ya ada ya uhamisho na sasa imebakia kwa upande wa mchezaji tu kukubali na dili kumalizika.
Jorrel Hato
ARSENAL wametuma wawakilishi wake kwenda Uholanzi kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Ajax juu ya beki wao wa kati wa kimataifa wa Uholanzi, Jorrel Hato, mwenye umri wa miaka 19. Benchi la ufundi la Arsenal linapambana kuboresha kikosi chao kuhakikisha wanafanya vizuri kwa msimu ujao. Hato ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Ajax.
Oleksandr Zinchenko
AC Milan wanataka kumsajili beki wa Arsenal, Oleksandr Zinchenko, 28, ambaye hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Arsenal hali inayosababisha atamani kuondoka katika dirisha lijalo kwa ajili ya kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza. Mbali ya Milan, timu kadhaa za ndani ya England zimetuma maomba ya kumsajili kwa mkopo.
Junior Fripo
REAL Betis wamewasilisha ofa ya mkataba wa miaka mitatu kwa beki wa zamani wa Leeds United, Junior Firpo, mwenye umri wa miaka 28, ambaye ameachana na timu yake mwisho wa msimu uliopita. Licha ya kupokea ofa hiyo, staa huyu wa kimataifa wa Jamhuri ya Dominika hadi sasa bado hajafanya uamuzi ikiwa atajiunga nao au laa.