Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa Arsenal hii, kazi ipo 2025/26

ARSENAL Pict

Muktasari:

  • Baada ya kukaribia kubeba taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo na kukwama kwenye hatua za mwishoni, Arteta na mabosi wake huko Emirates wameshafahamu tatizo na sasa wamepanga kulitatua.

LONDON, ENGLAND: MISIMU mitatu mfululizo kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England, hilo limewachosha Arsenal.

Na sasa miamba hiyo ya Emirates inayonolewa na Mhispaniola Mikel Arteta, imepanga kufanya kweli kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kwa maana ya kunasa mastaa wa maana kwa lengo la kumaliza ukame wa mataji kwa kubeba taji la Ligi Kuu England msimu ujao.

Baada ya kukaribia kubeba taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo na kukwama kwenye hatua za mwishoni, Arteta na mabosi wake huko Emirates wameshafahamu tatizo na sasa wamepanga kulitatua.

Itafanyaje kumaliza tatizo hilo? Ni kusajili wachezaji wa maana. Na kwa kipindi hiki dirisha la usajili likiwa limefunguliwa, Arteta atakuwa tayari kufungulia pochi kunasa majembe yatakayoleta mataji Emirates.

Mastaa kibao wa maana wamekuwa wakihusishwa na timu hiyo akiwamo kiungo Martin Zubimendi na straika Benjamin Sesko. Sambamba na hilo kutakuwa na mastaa wengine ambao watafunguliwa mlango wa kutokea ili kutoa nafasi kwa wapya kuingia kwenye kikosi hicho.

Kwa jinsi mambo yalivyo, Arsenal itakuwa kwenye mwonekano tofauti kabisa msimu ujao, hasa kwenye kikosi chao kitakachokuwa kinaanza chini ya kocha Arteta.

Kipa David Raya bila shaka ataendelea kuwa chaguo la kwanza kwenye goli la miamba hiyo, hasa baada ya kufanikiwa kushinda tuzo ya Golden Glove kwa misimu miwili mfululizo. Lakini, Arsenal imepanga kuongeza kipa mwingine wa kuja kuleta ushindani wa namba kwenye kikosi kwa kuwa Neto atarudi kwenye timu yake ya Bournemouth baada ya mkopo kumalizika na Karl Hein ataondoka jumla.

Kwenye ukuta pia kutakuwa na sura zilizoeleka licha ya mabeki Myles Lewis-Skelly na William Saliba kuhusishwa na Real Madrid. Kocha Arteta hawezi kuruhusu mastaa wake hao kuondoka.

Gabriel Magalhaes na Jurrien Timber ni mabeki wengine muhimu kwenye kikosi hicho cha Arsenal na hivyo kuunda ukuta wa wakali wanne ambao umekuwa mgumu kupitika. Kwenye eneo hilo la ukuta, kuna baadhi ya mabeki watafunguliwa mlango wa kutokea akiwamo Kieran Tierney, Oleksandr Zinchenko, Takehiro Tomiyasu na Nuno Tavares - wataruhusiwa kuondoka.

Mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Arsenal kwa msimu ujao yatakuwa kwenye sehemu ya kiungo. Staa wa Real Sociedad, Martin Zubimendi - ambaye amekuwa akiwindwa na timu hiyo kwa muda mrefu, anaweza kuingia kwenye eneo hilo. Real Madrid inamtaka pia Zubimendi, lakini Arsenal ina nafasi kubwa ya kunasa saini yake ili akakamatie sehemu ya kiungo huko Emirates. Kwenye eneo hilo, Zubimendi atacheza sambamba na Declan Rice na nahodha Martin Odegaard. Jorginho ataondoka kwenda Brazil, huku Thomas Partey mkataba wake umekwisha na bado hakijaeleweka juu ya dili jipya. Kuna uwezekano mkubwa, Partey akabaki ili kumpa Arteta machaguo mapana katika eneo hilo la katikati ya uwanja. Viungo wengine wanaotarajia kuondoka ni Reiss Nelson, Marquinhos na Raheem Sterling.

Ndoto za kocha Arteta ni kumnasa pia winga wa Athletic Bilbao, Nico Williams. Arsenal ikifanikiwa kumnasa Mhispaniola huyo atakwenda kucheza kwenye wingi ya kushoto. Upande wa kulia kutakuwa na Bukayo Saka, kuifanya Arsenal kuwa na uwezo wa kukimbiza kote, kushoto na kulia. Eneo ambalo litakuwa na sura mpya ni nafasi ya mshambuliaji wa kati, ambapo kwa sasa dalili zote atanaswa Benjamin Sesko.

Hiki hapa kikosi cha ndoto Arsenal: Raya; Lewis-Skelly, Gabriel, Saliba, Timber; Rice, Zubimendi, Odegaard; Williams, Sesko, Saka.