Kounde wa Barcelona aingia anga za Chelsea
Muktasari:
- Licha ya ofa hiyo inayoonekana kuwa nono, Barca haina mpango wa kumuuza na tayari imeshaanza mazungumzo na wawakilishi wake kwa ajii ya kumsainisha mkataba mpya.
CHELSEA ipo tayari kulipa Pauni 83 milioni kwenda Barcelona ili kuipata saini ya beki kisiki wa timu hiyo na timu ya taifa ya Ufaransa, Jules Kounde, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Licha ya ofa hiyo inayoonekana kuwa nono, Barca haina mpango wa kumuuza na tayari imeshaanza mazungumzo na wawakilishi wake kwa ajii ya kumsainisha mkataba mpya.
Barca haitaki kumuuza Kounde kutokana na mchango wake mkubwa katika kikosi cha kwanza akisaidia ubora katika eneo lao la ulinzi.
Mkataba wa Mfaransa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 36 za michuano yote na kutoa asisti saba.
Charles de Ketelaere
BENCHI la ufundi la Manchester City linamfuatilia kwa karibu kiungo wa Atalanta, Charles de Ketelaere mwenye umri wa miaka 23, ambaye linamwangalia kama mbadala wa Kevin de Bruyne ambaye haonekani kuwa na muda mrefu wa kuendelea kusalia katika kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England. Tangu kuanza kwa msimu huu, Charles de Katelaere amecheza mechi 37 za michuano yote na kufunga mabao 11 na ameonyesha kiwango kizuri kilichoivutia Man City.
Tariq Lamptey
MABOSI wa Ajax wana matumaini makubwa ya kumsajili beki wa Brighton na Ghana, Tariq Lamptey, 24, na Joel Veltman ambaye anaichezea Brighton. Ajax ina matumaini ya kuwapata mastaa hawa kwa sababu mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote ya kuwaongeza, na kunauwezekano wawili hao wakaenda kutafuta changamoto mpya kwengineko.
Mateo Retegui
ARSENAL imewasiliana na Atalanta kuhusu mpango wa kuipata huduma ya mshambuliaji wao, Mateo Retegui, lakini mchakato unaonekana kuwa na ugumu kwa asilimia kadgaa kutokana na uwepo wa vigogo wengine ambao wanahitaji saini yake. Mateo mwenye umri wa miaka 25, huduma yake pia inahitajika sana na Manchester United iliyojaribu kutaka kumsajili tangu Januari mwaka huu na kuna wezekano akaondoka.
Micky van de Ven
LIVERPOOL imeanza mazungumzo na Tottenham kwa ajili ya kumsajili beki wa timu hiyo raia wa Uholanzi, Micky van de Ven, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Micky ni miongoni mwa mastaa ambao kocha Arne Slot amependekeza wasajiliwe ili kuboresha eneo lao la ulinzi ambalo huenda likavurugika msimu ujao kwa Trent Alexander Arnold na Virgil van Dijk ambao wanamaliza mikataba yao kuondoka.
Luis Diaz
AL-Nassr na Al-Hilal zinapambana kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Colombia, Luis Diaz mwenye umri wa miaka 28 ambaye tangu mwaka jana amekuwa akihusishwa kuondoka. Diaz ambaye pia anawindwa na Barcelona, mkataba wake wa sasa untarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu huu amecheza mechi 34 za michuano yote na kufunga mabao 12.
Dusan Vlahovic
ARSENAL imeripotiwa kuwa katika mazungumzo na Juventus ili kuipata saini ya straika wao, Dusan Vlahovic, 24,ambaye Mikel Arteta alihitaji asajiliwe tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini ilishindikana. Vlahovic alikuwa katika orodha ya mastaa waliopendekezwa na kocha Mikel Arteta ili kusajiliwa dirisha hili ili kuboresha safu yake ya ushambuliaji.
Tyler Dibling
TOTTENHAM inadaiwa kuweka nguvu zaidi kwenye mchakato wa kutaka kumsajili kiungo wa Southampton, Tyler Dibling dirisha lijalo baada ya kushindwa kumsajili lililopita. Tyler amezivutia timu nyingi kutokana na kiwango bora msimu huu. Timu zote zilikuwa tayari kutoa zaidi ya Pauni 20 milioni kufanikisha mchakato wa kumsajili.