Klabu Bingwa Dunia… Nani anafuata?
Muktasari:
- Mwaka huu pia inaweza ikaongeza idadi ya mataji iliyochukua kupitia michuano itakayoanza Juni 15 nchini Marekani.
NEW YORK, MAREKANI: HISTORIA na rekodi zinaonyesha Real Madrid inaongoza katika msimamo wa timu ambazo zimefanikiwa kushinda taji la Klabu Bingwa Dunia mara nyingi zaidi kuliko timu yoyote.
Mwaka huu pia inaweza ikaongeza idadi ya mataji iliyochukua kupitia michuano itakayoanza Juni 15 nchini Marekani.
Hata hivyo, sio Real Madrid pekee ambayo imewahi kushinda taji hilo lakini kuna orodha ya timu kibao ambazo zimewahi kulipata na hapa ni baadhi ya zilizoshinda kombe hilo tangu lilipoanzishwa 2000.
9. AC Milan - Taji 1
Ni timu nyingine ya Italia iliyowahi kushinda taji hilo ililofanikiwa kufanya hivyo 2007.
AC Milan ilipata kombe mbele ya Boca Juniors ambayo ilikuwa ni kana kwamba inajaribu kulipiza kisasi.
Kabla ya mechi hiyo, AC Milan na Boca ziliwahi kukutana 2003 na AC Milan ikapoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare.
8. Inter Milan-Taji 1
Walishinda mwaka 2010, wakati huo walikuwa wakitawala soka la Ulaya na dunia kwa ujumla. Mbali ya taji hilo pia ilishinda Ligi Kuu Italia na Ligi ya Mabingwa kwa mwaka huo.
7. Liverpool -Taji 1
Liverpool walifanikiwa kushinda Kombe la Dunia kwa klabu 2019, ikirejea kileleni katika soka la kimataifa baada ya mafanikio makubwa kwenye ligi za ndani na Ulaya. Timu hiyo ilifanikiwa kupata taji baada ya kuichapa Flamengo ya Brazil, bao 1-0 katika mchezo ambao ulienda dakika 30 za ziada baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
6. Manchester United-Taji 1
Huu ulikuwa ni miongoni mwa miaka ya mafanikio kwa Mashetani Wekundu kwani mbali ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na baadaye Klabu Bingwa Dunia pia walifanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu England. Katika mchezo wa fainali ilicheza dhidi ya LDU Quito ya Ecuador na ikashinda kwa bao 1-0. Michuano ya mwaka huo ilifanyika Yokohana nchini Japan.
5. Chelsea - taji 1
Chelsea walifanikisha kushinda taji hili mwaka 2021 baada ya kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huohuo ikiongozwa na kocha Thomas Tuchel ambaye kwa sasa anaifundisha England.
4. Bayern Munich- Mataji 2
Bayern Munich inashika nafasi ya tatu kwa timu za Ulaya zilizoshinda mara nyingi zaidi taji hili ikifanya hivyo mwaka 2013 na mwaka 2020.
Klabu hii ambayo imekuwa ikitawala Bundesliga kwa miaka mingi, ilishinda taji la mwaka 2013 dhidi ya Raja Casablanca ambao ndio walikuwa wenyeji wa michuano hiyo.
Mechi hiyo ilimalizika kwa Bayern kushinda mabao 2-0.Fainali ya 2020 ilicheza dhidi ya mabongwa kutoka Mexico, Tigres UANL na ikashinda kwa bao 1-0.
3. Corinthians- Mataji 2
Corinthians ni miongoni mwa timu kubwa za Brazil iliyoshinda Kombe la Dunia la Klabu mara nyingi zaidi kuliko timu yoyote ndani ya Bara la Amerika Kusini.
Mataji mawili iliyoshinda ilikuwa ni 2000 na 2012. Mwaka 2000 ilikuwa ni mara ya kwanza kabisa mashindano haya kuanzishwa, na Corinthians walishinda kabla ya kutwaa tena 2012.
2. Barcelona - Mataji 3
Barcelona imefanikiwa kushinda Kombe la Dunia la klabu mara tatu, ikiwa inashika nafasi yapili katika orodha ya timu zilizoshinda mataji mengi. Wamefanikiwa kutwaa mataji haya 2009, 2011 na 2015. Mataji hayo matatu Barcelona imeshinda dhidi ya Kashima Antlers ya Japan 2016, Gremio ya Brazil mwaka 2017 na mbele ya Al Ain ya Falme za Kiarabu mwaka 2018 ambapo iliichapa bao 4-1.
1. Real Madrid - Mataji 5
Real Madrid ndiyo klabu yenye mafanikio makubwa zaidi katika Kombe la Dunia la klabu, wakiwa wameshinda mataji matano. Mafanikio haya yalianza 2014, wakati wa mzunguko wa kwanza wa mashindano yaliyokuwa na mfumo wa kisasa ambapo mabingwa wa UEFA Champions League huingia moja kwa moja. Kuanzia hapo, Real Madrid wamekuwa wakirejea kwa mara kwa mara na kuonyesha ubabe mkubwa dhidi ya vilabu vya mabara mengine. Mataji haya ilishinda mwaka 2014 dhidi ya San Lorenzo, pia 2016, 2017, 2018 na 2022.
TIMU NYINGINE
Mbali ya timu tajwa hapo juu mabingwa wengine waliowahi kutwaa taji hili ni pamoja na Manchester City na Internacional ambayo ilishangaza watu zaidi 2006 ilipoicha Barcelona iliyokamilika bao 1-0 katika michuano iliyofanyika kule Japan.