Isak aitamani nafasi ya Salah Liverpool
Muktasari:
- Isak mwenye mkataba na Newcastle United hadi 2028, ameripotiwa kupendezwa na mpangokazi wa Liverpool inayomtaka akawe mbadala wa Mohamed Salah ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
STRAIKA wa Newcastle United na Sweden, Alexander Isak, 25, anadaiwa kutamani zaidi kujiunga na Liverpool badala ya timu nyingine ikiwa ataondoka Newcastle United.
Isak mwenye mkataba na Newcastle United hadi 2028, ameripotiwa kupendezwa na mpangokazi wa Liverpool inayomtaka akawe mbadala wa Mohamed Salah ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Licha ya kutamani zaidi kutua Liverpool, inaonekana usajili huo utakuwa na asilimia chache za kukamilika kwani Majogoo hao watatakiwa kuweka kiasi kikubwa cha pesa mezani ili kushinda vita dhidi ya timu nyingine zinazomtaka.
Mkataba wa staa huyo unatarajiwa kumalizika 2028 na kumekuwa na timu nyingi kubwa zinazohitaji huduma yake tangu mwaka jana kutokana na kiwango bora anachoendelea kukionyesha akiwa na Newcastle United tangu ajiunge nayo.
Vinicius Jr
INAELEZWA kwamba wakala wa winga wa Real Madrid, Vinicius Jr, amewatajia mabosi wa timu hiyo kiasi kikubwa cha pesa ambacho mchezaji wake anahitaji ili kusaini mkataba mpya utakaomfanya kusalia katika kikosi chao kwa mrefu. Vinicius anayewindwa na timu za Saudi Arabia katika mkataba wake wa sasa kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa Real Madrid italipa zaidi ya Pauni 500 milioni.
Igor Paixao
TOTTENHAM Hotspur, Newcastle na Bournemouth zinapambana kutaka kumsajili winga wa Feyenoord, Igor Paixao katika dirisha lijalo la majira kiangazi. Staa huyo wa kimataifa wa Brazil alikuwa akihitajika na timu hiyo tangu dirisha la majira ya baridi mwaka huu, lakini alikataa na kuamua kusalia Feyenoord hadi mwisho wa msimu. Mkataba wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 unatarajiwa kumalizika 2029.
Marcus Thuram
INTER Milan inataka kumpa ofa ya mkataba mpya straika raia wa Ufaransa, Marcus Thuram, 27, ambao hautakuwa na kipengele cha sasa kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu inayomtaka italipa Pauni 75 milioni. Nyota huyo anawindwa na PSG ambayo ilitaka kumsajili dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Inter inataka kuondoa kipengele cha kumruhusu kuondoka au kuweka bei kubwa.
Dario Essugo
CHELSEA imevutiwa na kiungo wa Sporting Lisbon na Ureno, Dario Essugo ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo katika timu ya Las Palmas inayoshiriki Ligi Kuu Hispania (La Liga). Kwa mujibu wa ripoti ya awali kutoka kwa maskauti iliowatuma kumtazama, staa huyu mwenye umri wa miaka 19 anafaa kusajiliwa. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027.
Jean-Philippe Mateta
Crystal Palace inataka kiasi kisichopungua Pauni 40 milioni ili kumuuza mshambuliaji Jean-Philippe Mateta, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo timu nyingi zimeonyesha nia ya kumsajili ikiwa ni pamoja na Barcelona. Mateta ambaye ni mshambuliaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Palace, mkataba wake unamalizika mwakani.
Antonio Cordero
NEWCASTLE United inapambana kuhakikisha inaipata saini ya winga wa Malaga, Mhispania Antonio Cordero anayewindwa pia na Barcelona na Real Madrid. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Malaga imekuwa ikijaribu kumshawishi asaini mkataba mpya ili asiondoke bure, lakini Cordero, 18 amekataa.
Johan Bakayoko
NEWCASTLE United imeripotiwa kufanya makubaliano binafsi na mshambuliaji wa PSV Eindhoven na Ubelgiji, Johan Bakayoko ili kuipata huduma yake katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Bakayoko mwenye umri wa miaka 21, alikuwa akihusishwa na timu nyingi kubwa Ulaya tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.