Ipswich yarejea EPL kibabe, nne za play-offs zafahamika
Muktasari:
- Baada ya kushuka daraja miezi 12 iliyopita kufuatia kushinda mechi nne pekee katika msimu wao wa kwanza wa ligi ya juu baada ya miaka 22, kikosi hicho cha Kocha Kieran McKenna kimerejea Premier kibabe.
LONDON, ENGLAND: IKICHEZA nyumbani, Ipswich Town imefanikiwa kurejea Ligi Kuu ya England baada ya kuifunga Queens Park Rangers na kujihakikishia nafasi ya pili ya kupanda daraja moja kwa moja kutoka Championship ambapo imeungana na Coventry City, huku zingine nne zikienda kucheza mtoano.
Baada ya kushuka daraja miezi 12 iliyopita kufuatia kushinda mechi nne pekee katika msimu wao wa kwanza wa ligi ya juu baada ya miaka 22, kikosi hicho cha Kocha Kieran McKenna kimerejea Premier kibabe.
Wakiwa na hatma yao mikononi mwao kuelekea siku ya mwisho kuhitimisha msimu wa Championship leo Mei 2, 2026, Ipswich walijua kuwa ushindi katika uwanja wa Portman Road ungefuta kabisa matokeo yoyote ambayo wapinzani wao wa kupanda daraja, Millwall au Middlesbrough, wangeweza kupata.
Mabao ndani ya dakika tisa za mwanzo kutoka kwa George Hirst na Jaden Philogene, yaliwaweka kwenye njia sahihi kabla ya mchezaji wa akiba, Kasey McAteer kufunga bao la tatu mwishoni mwa mchezo na kuthibitisha ushindi huo.
Hii imeifanya Ipswich kusherehekea kupanda daraja kwa mara ya tatu ndani ya misimu minne chini ya McKenna, huku kocha huyo akiweka rekodi ya kuwa meneja wa kwanza wa klabu hiyo kuiongoza kupanda madaraja mara tatu, ikiwa ni pamoja na mara mbili kufika Ligi Kuu.
Kwa upande wa QPR, mechi hii ilikamilisha mwisho mbaya wa msimu wao, wakimaliza wakiwa na vipigo vinne mfululizo na mechi sita bila ushindi, na hatimaye kumaliza nafasi ya 15 huku wakitimiza msimu wao wa 11 mfululizo katika ligi hiyo.
Katika mafanikio mawili ya awali ya kupanda daraja chini ya McKenna, Ipswich waliingia mechi yao ya mwisho ya nyumbani wakijua kuwa ushindi ungewawezesha kufanikisha lengo hilo kama ilivyokuwa pia safari hii.
Wakiwa katika mazingira yenye shamrashamra kubwa Portman Road, walianza mchezo kwa kasi na kuonyesha soka bora.
Ipswich walikuwa na wachezaji watatu waliobaki kutoka kikosi kilichoifunga Huddersfield Town kupanda daraja hapo awali ambao ni George Hirst, Leif Davis na Wes Burns, wawili kati yao walihusika moja kwa moja kwenye bao la kwanza, ambapo Davis alipiga krosi iliyomkuta Hirst aliyefunga kwa karibu kabisa.
Mshambuliaji wa Scotland, Hirst, ambaye pia aliwahi kufunga wakati walipopanda kutoka League One miaka mitatu iliyopita, aligeuka mtoa pasi ya bao la pili kwa kumpasia Philogene aliyefunga kwa ustadi dhidi ya kipa wa QPR, Joe Walsh.
Baada ya hapo, Ipswich walitawala mchezo kama walivyotaka, na licha ya majaribio machache kutoka kwa mchezaji wa akiba wa wageni Paul Smyth, hawakuonyesha dalili ya kupoteza udhibiti.
Katika kipindi cha pili, McKenna aliingiza wachezaji wa akiba kama McAteer, mfungaji bora Jack Clarke, pamoja na wachezaji waliosajiliwa Januari Dan Neil na Anis Mehmeti, ambao wangeanza kikosi cha kwanza katika karibu timu yoyote ya Championship kuonyesha ubora wa kikosi chao.
Ipswich wamekuwa wakinufaika sana na wachezaji wa akiba msimu huu, na katika bao la tatu, Mehmeti pamoja na mshambuliaji Mhispania Ivan Azon walileta mkanganyiko mkubwa, mpira ukadondoka na McAteer kuupiga nyavuni, na kuanzisha rasmi sherehe za kupanda daraja.
Habari hizo zilisambaa haraka kwa mashabiki wa Millwall na wale wa Middlesbrough waliokuwa Wrexham, na matumaini yao ya kushika nafasi ya pili yakazimika mapema kwani timu hizo zimebaki nafasi ya kucheza mechi za mchujo (play-offs), zikijiunga na Southampton na Hull City.
PLAY_OFFS KITAWAKA
Timu nne zilizomaliza nafasi ya tatu hadi sita ambazo ni Millwall, Southampton, Middlesbrough na Hull, zinakwenda kucheza mtoano 'play-offs' kuwania nafasi moja ya kupanda daraja ambapo zitaanzia nusu fainali, kisha fainali ambapo bingwa ndiye anapanda.
Femi Azeez alifunga mabao mawili wakati Millwall wakishinda 2-0 dhidi ya Oxford United waliokwisha shuka daraja, lakini wakalazimika kuridhika na nafasi ya play-offs.
Kufuzu kwa play-offs kwa mara ya kwanza tangu 2002 ni mafanikio makubwa kwa Millwall, ambao watacheza nusu fainali dhidi ya Hull, waliopata nafasi ya sita siku ya mwisho.
Mapambano ya nafasi ya play-offs yaliendelea kati ya Hull, Wrexham na Derby County ili kuona nani ataungana na Southampton na wengine.
Ndoto za Wrexham za kupanda daraja kwa mara ya nne mfululizo zilizimwa baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Middlesbrough kwenye uwanja wa SToK Cae Ras.
Hull walitumia vizuri matokeo hayo kwa kushinda 2-1 dhidi ya Norwich City na kujihakikishia nafasi ya sita. Mabao mawili ya Oli McBurnie yaliwasaidia kurejea na kushinda baada ya kuwa nyuma.
Wakati huo huo, Sheffield United walifanya comeback ya kipindi cha pili na kushinda 2-1 dhidi ya Derby, na kuzima matumaini yao ya kuingia play-offs.
Derby walikuwa mbele kipindi cha kwanza kupitia bao la mapema la Sam Szmodics, lakini wageni walirudi kwa nguvu na kuharibu ndoto ya wenyeji kumaliza ndani ya sita bora.
ZILIZOSHUKA
Timu tatu zilizomaliza nafasi ya 22, 23 na 24 ambazo ni Oxford United, Leicester City na Sheffield Wednesday zimeshuka daraja ambapo msimu ujao zitashiriki League One.
Wakati ligi hiyo ikihitimishwa leo, imeshuhudiwa msimu huu timu tatu zikikatwa pointi kutokana na sababu mbalimbali.
West Bromwich Albion iliyomaliza nafasi ya 21, moja juu ya mstari wa kushuka daraja ikiwa na pointi 51, wakati wa chini yake Oxford United anazo 47, Aprili 24, 2026 ilipokwa pointi mbili kutokana na kukiuka sheria za PSR ambazo ni Kanuni za Uendelevu wa Kifedha za UEFA ilizowekwa ili kuzuia klabu za soka za kulipwa kutumia fedha zaidi ya wanazopata katika jitihada za kupata mafanikio. Lengo lake ni kuhakikisha kuwa klabu hazijiingizi kwenye matatizo ya kifedha ambayo yanaweza kuhatarisha uhai wao wa muda mrefu.
Adhabu kama hiyo iliikuta Leicester City ambayo Februari 5, 2026 ilipokwa pointi sita. Rufaa ya Leicester City kupinga adhabu hiyo ilikataliwa Aprili 8, 2026. Hatua hiyo imefanya Leicester kumaliza na pointi 46 ambazo kama zisingekatwa, basi isingeshuka daraja.
Sheffield Wednesday nayo Oktoba 24, 2025, ilipokwa pointi 12 kutokana na ishu za usimamizi wa kiungozi, kisha ikakatwa pointi sita zaidi, Desemba 1, 2025 kwa kushindwa kutimiza majukumu ya malipo. Jumla imekatwa pointi 18 ambazo ndizo imezikusanya msimu huu iliposhinda mechi mbili na sare 12, huku ikipoteza 32, hivyo imemaliza haina pointi.