Hii hapa ratiba ya gwaride la ubingwa Arsenal
Muktasari:
- Wakati hayo yakijiri, ratiba ya gwaride la kusherehekea ubingwa huo imetoka ambapo litafanyika Jumapili, Mei 31, 2026, siku moja baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain mjini Budapest.
LONDON, ENGLAND: SHANGWE zinaendelea kwa mashabiki wa Arsenal baada ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Premier League kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22.
Wakati hayo yakijiri, ratiba ya gwaride la kusherehekea ubingwa huo imetoka ambapo litafanyika Jumapili, Mei 31, 2026, siku moja baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain mjini Budapest.
Mpaka sasa, muda rasmi wa kuanza gwaride hilo bado haujatangazwa na Arsenal, lakini mipango ya awali inaonyesha kuwa basi litaanzia safari kutoka Uwanja wa Emirates kupitia maeneo ya Drayton Park, Aubert Park, Highbury Grove, St Paul’s Road na Upper Street kabla ya kurejea tena uwanjani hapo.
Sababu ya gwaride kufanyika Mei 31, 2026 ni kwamba baadhi ya nyota wa Arsenal wanaotarajiwa kushiriki Kombe la Dunia 2026 wanapaswa kujiunga na timu zao za taifa kuanzia Jumatatu ya Juni 1, 2026.
Mashabiki watakaosafiri kwenda Budapest kwa ajili ya fainali hiyo ya UEFA watapaswa kurejea haraka London ili wasikose shamrashamra hizo kubwa za kihistoria.
Iwapo Arsenal itaifunga PSG katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mei 30, 2026 huko Puskás Aréna, basi itasherehekea mataji yote mawili kwenye gwaride hilo la basi la wazi. Endapo itashindwa, gwaride bado litafanyika kwa ajili ya kusherehekea taji la Premier League pekee.
Arsenal ilijihakikisha ubingwa huo baada ya sare ya 1-1 kati ya AFC Bournemouth na Manchester City kwenye Uwanja wa Vitality, usiku wa Mei 19, 2026.
Bao la kuvutia la Eli Junior Kroupi kabla ya mapumziko liliiweka City kwenye presha kubwa, huku bao la kuchelewa la Erling Haaland dakika ya 90+5 likishindwa kuzuia Arsenal kutawazwa mabingwa.
Usiku mmoja kabla yake, kikosi cha Mikel Arteta kilipata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Burnley na kufikisha tofauti ya pointi tano kileleni huku mchezo mmoja pekee ukibaki.