Hawa sio wageni kombe la dunia la klabu
Muktasari:
- Wakati michuano hiyo iliyoanzishwa 2000 ikitarajiwa kufanyika kwa mara ya 21 kuna timu zina rekodi nzuri ya kushiriki mara nyingi kuliko nyingine. Katika makala haya zipo timu 10 ambazo zimefuzu mara nyingi zaidi kwenye Kombe la Dunia la Klabu pamoja na historia kwenye mashindano hayo na mafanikio ziliyoyapata.
FLORIDA, MAREKANI: KATIKA mwendelezo wa kuzifuta siku zilizosalia kabla ya michuano ya Kombe la Dunia la Klabu kuanza Juni 15, nchini Marekani, mambo yameanza kunoga.
Wakati michuano hiyo iliyoanzishwa 2000 ikitarajiwa kufanyika kwa mara ya 21 kuna timu zina rekodi nzuri ya kushiriki mara nyingi kuliko nyingine. Katika makala haya zipo timu 10 ambazo zimefuzu mara nyingi zaidi kwenye Kombe la Dunia la Klabu pamoja na historia kwenye mashindano hayo na mafanikio ziliyoyapata.
10. Internacional (Brazil) - Ushiriki: 2
Miaka: 2006, 2010
Timu hiyo ilishinda Kombe la Dunia la Klabu 2006 baada ya kuichapa Barcelona 1-0. Lakini, baada ya hapo ilipotea kwa miaka kadhaa na ilirudi 2010, lakini iliishangaza dunia kwa kufungwa na TP Mazembe kwenye nusu fainali.
9. Bayern Munich (Ujerumani)- Ushiriki: 2
Miaka: 2013, 2020
Bayern ilishinda mara zote iliposhiriki ikiwa bingwa wa Ujerumani na Ulaya. Mwaka 2020 ilishinda taji ikikamilisha mataji sita ndani ya msimu mmoja. Ni moja ya klabu bora zaidi kihistoria.
8. Guangzhou Evergrande (China) - Ushiriki: 2
Mwaka: 2013, 2015
Mwaka huo iliibuka kuwa timu tishio katika michuano ya Asia baada ya kupata wawekezaji tajiri na makocha wa kiwango cha dunia kama Marcello Lippi na Luiz Felipe Scolari. Ilifika nusu fainali 2015 lakini ilipoteza mbele ya Barcelona.
7. Kashima Antlers (Japan)- Ushiriki: 2
Mwaka: 2016, 2018
Mwaka 2016 ilikuwa timu ya kwanza ya Japan kufika fainali ikafungwa na Real Madrid katika muda wa ziada kwa mabao 4-2 katika michuano ambayo ilikuwa ni wenyeji. Kashima ni miongoni mwa timu zenye mafanikio katika Ligi Kuu Japan.
6. Al Hilal (Saudi Arabia)- Ushiriki: 03
Mwaka: 2019, 2021, 2022
Hii ni miongoni wa timu kubwa zaidi katika historia ya Asia,ikiwa na mataji mengi ya Ligi ya Mabingwa ya bara hilo.
Mwaka 2022 ilifika fainali, lakini ikapoteza mbele ya Real Madrid kwa mabao 5-3 mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.Miaka ya karibuni Al Hilal imewekeza katika usajili ikisajili mastaa kama Neymar ambaye ilikuwa inamlipa Pauni 2.5 milioni kabla haijaachana naye mwaka huu.
5. TP Mazembe (DR Congo) - Ushiriki: 3
Mwaka: 2009, 2010, 2015
Klabu hiyo ya DRC ilivunja rekodi 2010 kwa kuwa ya kwanza kutoka Afrika kufika fainali.
Ilizitoa timu kutoka Amerika Kusini na Asia kabla ya kufungwa na Inter Milan kwenye fainali.
Mafanikio yameifanya kuwa moja ya timu zilizoacha historia katika michuano hiyo.
4. CF Monterrey (Mexico)- Ushiriki: 5
Mwaka: 2011, 2012, 2013, 2019, 2021
Hii ni moja ya timu bora katika eneo la Concacaf ikitawala Ligi ya Mabingwa.
Mafanikio makubwa ni kumaliza kwenye nafasi ya tatu 2012. Inajulikana kwa kutumia idadi kubwa ya wachezaji kutoka Mexico na wachache nje ya nchi hiyo.
3. Real Madrid CF (HISPANIA)- Ushiriki: 6
Mwaka: 2000, 2014, 2016, 2017, 2018, 2023
Ni klabu iliyoshinda mataji mengi zaidi ya Kombe la Dunia la Klabu ikifanya hivyo mara tano. Imekuwa mwakilishi wa UEFA kila iliposhinda Ligi ya Mabingwa.
Mwaka 2018 iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kushinda taji mara tatu mfululizo wakati huo kikosi kilikuwa na nyota kama Cristiano Ronaldo, Luka Modric na Sergio Ramos na ilitawala kuanzia2014 hadi 2018.
2. Al Ahly SC (Misri)- Ushiriki: 09
Mwaka: 2005, 2006, 2008, 2012, 2013, 2020, 2021, 2022, 2023
Klabu hiyo ni malkia wa soka la Afrika ikiwa na mataji mengi ya Ligi ya Mabingwa. Imewakilisha Afrika mara nyingi zaidi kwenye michuano hiyo na imewahi kushika nafasi ya tatu 2020, 2021 na 2023, na inajulikana kwa nidhamu na uzoefu mkubwa wa kimataifa.Pia ni moja ya klabu zenye mashabiki wengi Afrika na duniani.
1. Auckland City FC (New Zealand)
Kushiriki: 11
Mwaka: 2006, 2009, 2011, 2017, 2022, 2023
Auckland City ndiyo klabu iliyoshiriki mara nyingi zaidi kwenye historia ya Kombe la Dunia la Klabu. Inashiriki kama bingwa wa Oceania. Mafanikio yake makubwa yalikuja 2014 ilipofika nusu fainali na kushika nafasi ya tatu ikizidiwa na Real Madrid.
Timu hiyo inatoka New Zealand, nchi yenye ushindani mdogo katika soka la klabu, jambo linaloirahisishia kufuzu mara kwa mara katika mashindano hayo.